Shahidi wa nne katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi inayomkabili Salum Njwete, ameieleza Mahakama kuwa mtu aliyehusika kumtoa macho Said Mrisho alikuwa ni mzoefu wa vitendo hivyo na siyo wa kawaida.
Shahidi huyo, Dk Christine Mataka (52) ambaye ni daktari bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alitoa maelezo hayo katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala alipotoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa Njwete (34) katika kesi iliyopata umaarufu wa ‘kesi ya Scorpion’ kutokana na maelezo kwamba aliyefanya uhalifu huo ni Scorpion.