Thursday 5 January 2017

SHERIA YA OBAMACARE TRUMP KUITUPILIA MBALI KWA KISHINDO

Rais Barack Obama amewahimiza wanachama wa chama cha Democratic kupigania sheria yake ya bima ya afya ambayo utawala wa Donald Trump umeahidi utaibatilisha upesi baada ya kuingia madarakani.
Kwenye mkutano wa faraghani wa saa mbili, Bw Obama aliwahimiza wabunge wa chama hicho kuitetea sheria hiyo, huku wanachama wa Republican nao wakichukua hatua kufuta sheria hiyo.

Makamu wa rais mteule Mike Pence pia alikuwa katika bunge la Congress, ambapo alisema chama chake kitafuta sheria hiyo ambayo hufahamika sana kama Obamacare.
Sheria hiyo iliwezesha takriban Wamarekani 20 milioni zaidi kupokea huduma ya afya.
Hata hivyo, sheria hiyo imekabiliwa na changamoto za kupanda kwa malipo ya wanaopokea huduma ya bima na pia kampuni nyingi za bima zimejitoa kutoka kwa mpango huo.
Hilo limewaacha Wamarekani wakiwa hawana njia nyingi mbadala za kujipatia bima ya afya.Trump
Baada ya Rais Obama kufanya ziara hiyo nadra sana makao makuu ya bunge Capitol Hill siku ya Jumatano, mbunge wa chama cha Democratic Elijah Cummings aliambia wanahabari kwamba Bw Obama aliwahimiza kupigana kulinda sera hiyo kuu iliyotimizwa na utawala wake.
Baadhi ya waliokuwepo waliwaambia wanahabari Marekani kwamba rais huyo anayeondoka pia aliwahimiza "kuwa na nguvu" huku Republican wakijiandaa kuchukua udhibiti wa ikulu ya White House na mabunge yote mawili ya Congress - Bunge la Wawakilishi na Bunge la Seneti - kwa mara ya kwanza katika mwongo mmoja.
Alisema hayo huku bunge la Seneti likichukua hatua ya kwanza ya kufuta sheria hiyo ya Obamacare.
Walipiga kura 51 dhidi ya 48 kujadili azimio la bajeti ambalo lengo lake ni kunyima ufadhili kwa mpango huo wa Obama.


No comments:

Post a Comment

advertise here