WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Manispaa ya Kigamboni
kuhakikisha unasimamia ujenzi wa kisasa na kutenga maeneo maalumu ya
wazi katika manispaa hiyo, ili kuepusha makosa ya ujenzi holela
yaliyofanyika katika maeneo mengine jijini Dar es Salaam.
Pamoja
na hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa amesema manispaa
hiyo mpya kwa sasa inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa majisafi na
salama na wakazi wake wanatumia maji ya visima pekee ambayo si safi na
salama.
Akizungumza
na watumishi wa Halmashauri na Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es
Salaam juzi katika ziara yake ya siku moja ya kujitambulisha na
kukumbushana kuhusu uwajibikaji, Majaliwa alisema kwa sasa mji wa Dar es
Salaam umejaa na eneo la Kigamboni ndio pekee la kukimbilia.
“Tunataka
turekebishe makosa tukiyoyafanya katika mipango miji jijini Dar es
Salaam, zingatieni matumizi bora ya ardhi, jengeni Manispaa ya Kigambo
iwe ni mji wa kisasa, tengeni fukwe za jamii. Ikibidi hata muelekeze
watu wajenge nyumba za aina gani,” alisisitiza.
Alisema
kwa sasa mji wa Dar es Salaam umejengwa bila kuzingatia mipango miji
kiasi cha kukosa maeneo nyeti kama bustani za kupumzikia wananchi pamoja
na fukwe.
“Wenzetu
wana hizi bustani za kumpumzikia watu wake zinasaidia hata kuchangamsha
akili zao. Pale Dar es Salaam ufukwe wa jamii umebaki mmoja tu, Coco
ambao kila mtu anakimbilia huko,” alisema.
Kwa
upande wa Mgwandilwa, alisema manispaa hiyo imejipanga kuhakikisha
miaka hiyo wilaya hiyo inakuwa ni wilaya iliyojengwa kwa kuzingatia
mipango miji na kuwa na miji ya kisasa.
Alisema
kwa kuzingatia mipango miji hiyo, tayari halmashauri ya Kigamboni
imetenga jumla ya viwanja 456 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ikiwa ni
moja ya hatua ya kuunga mkono jitihada za serikali za kuijenga Tanzania
ya viwanda.
Akizungumzia
changamoto za manispaa hiyo, Mgandilwa alisema pamoja na kwamba wilaya
hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika maeneo ya elimu,
afya na miundombinu, hali ya ukosefu wa majisafi na salama ni tishio na
inahatarisha maisha ya wakazi wa eneo hilo.
Alisema
wilaya nzima ya Kigamboni inategemea maji ya visima ambapo hadi sasa
vipo visima 83 vinavyomilikiwa na taasisi mbalimbali na jamii ambavyo
navyo maji yake si safi na salama.
Aidha,
alisema kwa upande wa sekta ya afya alisema pamoja na kwamba wilaya
hiyo ina zahanati 17, kituo cha kimoja na hospitali kubwa moja, bado
haijatimiza lengo la serikali linalotaka kila kata kuwa na zahanati
moja.
Mkuu
huyo alibainisha changamoto nyingine zinazoikabili wilaya hiyo kuwa ni
uwepo wa mamlaka mbili zinazosimamia na kutawala eneo la ardhi ya
Kigamboni hali inayosababisha mvutano na kuifanya wilaya hiyo ishindwe
kuendelezwa kwa muda wa miaka nane sasa.
Alitaja
mamlaka hizo kuwa ni Mamlaka ya Kuendeleza Mji wa Kigamboni (KDA)
inayotawala na kusimamia asilimia 12 na Manispaa ya Kigamboni
inayosimamia na kutawala asilimia 88 ya ardhi ya wilaya hiyo ya
Kigamboni.
Kuhusu
ubovu wa barabara, Mgandilwa alisema kwa sasa wilaya hiyo ina barabara
mbili tu kuu na zote ziko katika hali mbaya ambazoni ni barabara
Kimbiji-Pembamnazi na Kibada- Mkuranga.
Waziri
Majaliwa, akijibu hoja ya muingiliano wa mamlaka katika eneo la ardhi,
alitaka mamlaka hizo zikutane na kujadili suala hilo ikiwa ni pamoja na
kulitafutia ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment