Thursday, 29 December 2016

KUTOKWA NA DAMU BILA MPANGILIO UKENI....


Tatizo hili huwasumbua wanawake wengi walio katika umri wa kuzaa na baadhi ya wanawake ambao tayari wameshafikia ukomo wa kuzaa. Kwa mwanamke aliyekwishafunga kupata hedhi kuendelea kupata damu ya hedhi au kutokwa na damu ukeni bila ya mpangilio siyo hali ya kawaida.
 
Mwanamke anaanza kuvunja ungo kuanzia umri wa miaka 12 na hufikia ukomo kuanzia umri wa miaka 45. Kupatwa na damu ukeni chini ya umri wa miaka 40 kuna vyanzo vingi kama tutakavyoona.
 
Chanzo cha tatizo
Damu kutoka bila ya mpangilio kwa mwanamke ambaye hajakoma hedhi husababishwa na mabadiliko katika mfumo wa homoni endapo hazipo sawa ‘Hormonal Imbalance.’ 

Uwepo wa uvimbe katika kizazi na matumizi ya dawa za homoni mfano sindano au vipandikizi. Kuweka kitanzi katika kizazi pia huwafanya wanawake wengine wapate hali hii ya kutokwa na damu bila mpangilio.
 
Mabadiliko ya mfumo wa homoni huweza pia kusababishwa na mshtuko wa mwili au hali ya mabadiliko ya mazingira.
 
Kuharibika kwa mimba pia ni mojawapo ya sababu kubwa. Mwanamke mwenye umri wa zaidi ya miaka 45 kupata damu ukeni bila ya mpangilio ni vema kuchunguza kwa undani kwani wana uwezekano mkubwa wa kuwa na saratani ya kizazi au shingo ya uzazi.
 
Dalili za tatizo
Mwanamke hulalamika kuona siku za hedhi zaidi kuliko kawaida yake, au kuona katikati ya mzunguko yaani aliona, ikaacha sasa inaanza tena.
 
Damu inaweza kuwa nyingi na mwanamke akabadilisha pedi mara nyingi kuliko kawaida  yake au akapata kidogokidogo lakini kwa muda mrefu.
 
Damu inaweza kuwa nyepesi au nyeusi au nzito na mabonge. Hutoa harufu isiyo ya kawaida endapo ata-bleed kwa muda mrefu. Ikiwa na mabonge huambatana na maumivu.
 
Mgonjwa huchukua muda mrefu hata zaidi ya majuma mawili akiwa anatokwa na damu, endapo hatapata tiba haraka huanza kuumwa tumbo chini ya kitovu ikiwa ni dalili za kupatwa na maambukizi ya kizazi kwa kuwa bakteria hupenda sana mazingira ya damu.
 
Hali inapoendelea mwanamke hupoteza uwezo wa kushika mimba na huathiri uzazi kwani hushindwa kufanya tendo la ndoa, homoni zinavurugika na maambukizi ya kizazi huathiri mirija ya mayai.
 
Uvimbe wa Fibroid ukiwa ndani ya kizazi husababisha damu zitoke bila ya mpangilio na kuzuia mimba kukua na hata ikiingia inaweza isiendelee.
 
Uchunguzi
Tatizo hili ni sugu na huleta athari kubwa katika mfumo wa uzazi wa mwanamke hivyo ni vema uchunguzi wa kina ukafanyika katika hospitali kubwa. Vipimo vya damu kuangalia mfumo wa homoni, kipimo cha Ultrasound kuangalia kizazi na vifuko vya mayai pia hufanyika.
 
Ushauri
Usidharau tatizo hili la kutokwa na damu bila mpangilio ukeni ukiwa bado binti au mtu mzima kwani madhara yake ni makubwa. Muone haraka daktari kwa uchunguzi na tiba

No comments:

Post a Comment

advertise here