Tuesday, 7 February 2017

KUMBE HATA MAKONDA ANAUZA UNGA :JOSEPH KASHEKU

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku ameendeleza ‘vita’ yake dhidi ya Paul Makonda, akisema yupo tayari kusaidia vyombo vya dola kukamata vigogo wa dawa za kulevya na kuhoji ukimya wa mawaziri watatu dhidi ya kile alichodai utajiri wa mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Awali, Kasheku ambaye ni maarufu kwa jina la Msukuma, alitoa tuhuma dhidi ya Makonda juzi, alipotaka kujua wafadhili wa safari za mkuu huyo wa mkoa nje ya nchi na sababu za kubagua watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya kwa kutaja baadhi na kuwaacha wengine, huku mawaziri wakisita kuchukua
hatua.
Alitoa tuhuma hizo bungeni baada ya Makonda kuagiza watu 12, wakiwemo wasanii maarufu wa muziki na filamu, kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam, akiwatuhumu kuhusika na utumiaji au biashara ya dawa za kulevya.
Jana, Msukuma aliibuka na hoja nzito zaidi akihoji sababu za mawaziri kutochukua hatua na pia kutaja baadhi ya mali alizopata Makonda katika kipindi kifupi alichoshika madaraka ya mkuu wa mkoa baada ya kuwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni pia kwa muda mfupi.
Mbunge huyo alitoa tuhuma hizo nzito muda mfupi baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, wakati alipotumia kanuni ya 68 (7) kuomba mwongozo kutoka kwa Naibu Spika, Tulia Ackson.

No comments:

Post a Comment

advertise here