LAYIII
Makamu wa pili wa rais nchini Burundi,
Gervais Ruyikiri ametangaza kuwa hatorurudi nchini kama usalama wake
utakua haujalindwa ipasavyo. Akizungumza kwenye televisheni ya Ufaransa
France 24, Gervais Rufyikiri, amesema ameamua kufanya hivyo akihofia
usalama wake kutokana na jinsi hali invyoendelea nchini Burundi.
Burundi: makamu wa pili wa rais ahofia usalama wake
Makamu wa pili wa rais wa Burundi, Gervais Rufyikiri, ambaye ametangaza kujiuzulu kwenye wadhifa wake.
AFP PHOTO / Fabrice Coffrini
Gervais Rufyikiri, ambaye ni mmoja wa vigogo wa chama tawala
cha Cndd-Fdd amesema amemuandikia barua rais wa Burundi Pierre
Nkurunziza, akimuomba kuachana na mpango wake wa kuwania muhula wa tatu,
akibaini kwamba ni kinyume na Katiba ya nchi pamoja na Mkataba wa amani
na maridhiano wa Arusha.
Gervais Rufyikiri amesema rais Nkurunziza amekua hasikii hata nasaha
anazopewa na taasisi za kimataifa pamoja na washirika wake wa karibu.
Wakati huo huo Spika wa Bunge la Burundi, Pie Ntavyohanyuma ameondoka
nchini humo Jumatano Juni 24, akielekea nchini Ubelgiji. Haijafahamika
iwapo kiongozi huyo wa taasisi muhimu nchini ameitoroka nchi hiyo au la.
Lakini habari ambazo zimeendelea kusambaa mjini Bujumbura zinabaini
kwamba Pie Ntavyohanyuma ameitoroka nchi.
Hayo yakijiri serikali ya Bujumbura ikiwakilishwa na waziri wake wa
mambo ya ndani, Edouard Nduwimana, imeshiriki katika mazungumzo
yanayolenga kutafutia ufumbuzi mgogoro unaoendelea kushuhudiwa nchini
Burundi.
Mazungumzo hayo yameingia Jumatano wiki hii katika siku yake ya pili, baada ya kuanza Jumaanne Juni 23.
Katika siku yake ya kwanza, mazungumzo hayo yaliitikiwa na upinzani,
mashirika ya kiraia pamoja na viongozi na wawakilishi wa dini
mbalimbali.
Serikali ya Bujumbura na chama tawala pamoja na baadhi ya washirika
wake walisusia mazungumzo hayo, wakibaini kwamba hawatashiriki
mazungumzo hayo ambayo yanakuja kuwapotezea muda wakati ambapo wako
katika siku za mwisho za kampenzi za uchaguzi wa wabunge na madiwani.
Jumatatu wiki hii timu ya usuluhishi iliwatolea wito wadau wote
katika mgogoro wa Burundi kushiriki mazungumzo kwa minajili ya kutafutia
suluhu mgogoro huo. Lakini Chama tawala cha Cndd-Fdd na serikali
vimesusia kikao cha kwanza cha mazungumzo hayo.
Jumanne Juni 23 chama hicho cha rais Pierre Nkurunziza kilitangaza
kuwa hakitashiriki kutokana na kampeni ya uchaguzi wa wabunge na
madiwani ambayo kinaendesha wakati huu zikisalia siku zisiozidi sita ili
ufanyike uchaguzi wa wabunge na madiwani.
Chama cha Uprona kinachotambuliwa na utawala wa Pierre Nkurunziza hakikushiriki mazungumzo hayo.
Kwa mujibu wa katibu mkuu wa chama cha Uprona, Gaston Sindimwo, huu siwakati wa mazungumzo. " Mazungumzo yanakaribishwa baada ya uchaguzi, hapana wakati huu", amesema gaston Sindimwo.
Itafahamika kwamba chama cha Cndd-Fdd kimekua kikifutilia mbali
uwezekano wowote wa kuandaa kwa makubaliano ya wadau wote katika
mchakato wa uchaguzi kalenda ya uchaguzi, pamoja na kuanzisha mazungumzo
yatakayowashirikisha wadau wote.
Timu ya usulihishi wa kimataifa ilikutana Jumatatu wiki hii kwa mara
ya kwanza mjini Bujumbura. Timu hii inaundwa na Ibrahima Fall kutoka
Umoja wa Afrika, Abdoulaye Bathily kutoka Umoja wa Mataifa, Katibu mkuu
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Richard Sezibera pamoja na Katibu
Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR ).
Hayo yakijiri hali ya usalama imeendelea kudorora katika maeneo mbalimbali nchini Burundi, hususan katika mji mkuu wa Bujumbura.
Hali ya hofu imeendelea kutanda katika mji wa Bujumbura, huku kila
upande ukiutuhumu mwengine kuhusika na mdororo wa usalama unaoshuhudiwa
wakati huu nchini Burundi.
No comments:
Post a Comment