Thursday, 2 July 2015

Serikali kununua Helikopta za zimamoto? na maneno ya Lowassa kwa wanaomuhukumu…#Magazetini July2

layiii
MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana aliwataka wanaomhusisha na ufisadi kuacha mara moja kwa sababu hakuna hata chembe ya ukweli katika tuhuma hizo.
Lowassa, aliyeonekana kuzungumza kwa hisia, alisema hayo jana mara baada ya kurejesha fomu ya kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.

Serikali kununua Helikopta za zimamoto? na maneno ya Lowassa kwa wanaomuhukumu…#Magazetini July2

HM
MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana aliwataka wanaomhusisha na ufisadi kuacha mara moja kwa sababu hakuna hata chembe ya ukweli katika tuhuma hizo.

Lowassa, aliyeonekana kuzungumza kwa hisia, alisema hayo jana mara baada ya kurejesha fomu ya kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Mbunge huyo wa Monduli alikuwa mmoja kati ya makada tisa waliorudisha fomu jana, ikiwa ni siku moja kabla ya kuisha kwa muda uliowekwa na chama hicho.
Wengine waliorejesha fomu jana ni Elidephonce Bilohe, Mwigulu Nchemba, Luhaga Mpina, Dk Hamisi Kigwangalla, Hassy Kitine, Mariki Marupu, Dk Asha Rose Migiro na Lazaro Nyalandu.
Hadi sasa, tayari wanachama 32 kati ya 42 wa CCM walioomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wamerudisha fomu na kazi hiyo itahitimishwa leo.
Hakuna mtu ambaye amejitokeza hadharani kumtuhumu Lowassa kwa ufisadi, lakini tuhuma hizo zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, hasa kutokana na mbunge huyo wa Monduli kujiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu mwaka 2008 baada ya kuibuka sakata la mkataba wa ufuaji umeme wa dharura baina ya Serikali na Kampuni ya Richmond RDC ya Marekani ambayo ilionekana haina uwezo.
Wakati huo, Lowassa alisema kwenye hotuba yake ya kujiuzulu kuwa amefanya uamuzi huo “ili kuonyesha dhana ya uwajibikaji, lakini kutokubaliana na utaratibu uliotumika wa kusema uongo ndani ya Bunge kwa kumsingizia mtu.”
Lowassa alirudia wito wake wa kutaka wenye ushahidi wa tuhuma hizo wajitokeze hadharani.
“Nataka nitumie fursa hii kuwataka wale wote ambao wamekuwa wakinituhumu kwa miaka kadhaa sasa na kunihusisha na suala zima la rushwa, nawaambia waache mara moja, kwani hakuna chembe hata ya ukweli wa maneno hayo,” .
“Natoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma hizo za kipuuzi, autoe na aeleze kwa ushahidi rushwa yoyote inayonihusu, aseme nimechukua lini, kwa nani, kwa lipi na kiasi gani?”
Alisema yeye ni mwadilifu na anaposema atasimamia vita dhidi ya rushwa atafanya hivyo kwa vitendo bila kumuonea mtu na bila kumuonea haya yeyote.
Ukumbi wa Whitehouse, jana ulijaa wana-CCM ambao walifika kushuhudia Lowassa akirudisha fomu tofauti na idadi iliyowahi kutokea kwa wagombea wengine kadhaa waliomtangulia. Hali hiyo ilisababisha foleni kwenye Barabara ya Mtaa wa Kuu unaopita mbele ya ofisi za CCM, na kusababisha usumbufu kwa wapita njia.
MWANANCHI
Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara imezidi kupata pigo baada ya Mahakama kutengua matokeo ya uchaguzi wa wenyeviti wa vitongoji 16 vya mji mdogo wa Mirerani, kwa maelezo kuwa ulikiuka sheria na utaratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha mwezi mmoja kwa Mahakama kutengua matokeo ya uchaguzi huo ambao uliwaweka madarakani makada wa CCM.
Awali, Mei 30 Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kiteto ilitengua matokeo ya uchaguzi wa mwenyekiti wa Kijiji cha Lobosireti kwa kukiuka sheria na utaratibu.
Chadema ilifungua kesi kadhaa mahakamani hapo kupinga kitendo cha wagombea wa CCM kupewa ushindi bila kufanya uchaguzi Desemba 14, mwaka jana.
Hukumu hiyo ya jana, inatokana na kesi zilizofunguliwa na Chadema wilayani Simanjiro kwenye kata za Endiamtu na Mirerani, wakipinga wagombea wa CCM kupewa ushindi bila kupigiwa kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana.
Hakimu Mkazi Mfawidhi mahakama hiyo, Elimo Massawe aliagiza kurudiwa kwa uchaguzi wa viongozi wa vitongoji vya Zaire, Kisimani, Tenki la Maji, Endiamtu, Kairo na Kazamoyo vilivyoko Kata ya Ediamtu.
Hakimu Massawe alitaja vitongoji vingine kuwa ni Sekondari, Kilimahewa, Tanesco, Kazamoyo Juu, Mji mpya, Tupendane na vitongoji vya Kata ya Mirerani ambavyo ni Kangaroo, Songambele A, Getini na Songambele B.
Katika kesi hiyo, Chadema iliwakilishwa na mawakili James Millya, Shadrack Kimomogoro na Daudi Haraka na Mahakama iliamuru walipwe Sh160 milioni za gharama za kesi hiyo ambayo ilichukua takribani miezi sita hadi kutolewa hukumu.
Katibu Mwenezi wa Chadema mkoani Manyara, Ambrose Ndege alisema Mahakama imetenda haki kwa kutoa hukumu sahihi na wanajipanga ipasavyo kuhakikisha watashinda vitongoji vyote pindi uchaguzi huo utakaporudiwa.
“Tuliwaeleza tangu awali kuwa uchaguzi ukifanyika tutawashinda saa nne asubuhi hivyo tunawasubiri uwanjani na tutaongoza Mamlaka ya Mji wa Mirerani kwani wananchi wanatukubali,” Ndege.
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa CCM wa Kata ya Endiamtu, Mashaka Jeroro alisema wanatarajia kukata rufaa kupinga hukumu hiyo akisema wagombea wa Chadema walikosea kujaza fomu ndiyo sababu wakawekewa pingamizi.
MWANANCHI
Jiji la Mwanza jana ‘lilisimama’ kwa takriban dakika 10 wakati risasi na mabomu viliporindima kutokana na mapambano kati ya wafanyabiashara ndogondogo na polisi katika mitaa ya Lumumba, Rwagasore, Makoroboi na Barabara ya Nyerere.
Mapambano hayo yalitokea kuanzia saa 5.00 asubuhi baada ya wafanyabiashara hao, maarufu kwa jina la Wamachinga kuamua kutunishiana misuli na polisi waliokuwa kwenye operesheni ya kuwaondoa kwenye mitaa hiyo.
Wamachinga waliokuwa eneo la Hekalu la Wahindi lililopo Mtaa wa Makoroboi, ambalo limekuwa likitawaliwa na vurugu za kila mara baina ya pande hizo na eneo la Stendi ya Tanganyika, waliwatupia mawe polisi waliokuwa kwenye operesheni hiyo na ndipo walipoamua kupambana nao kwa kutumia risasi za moto na mabomu.
Tukio hilo limetokea zikiwa zimepita siku nne tangu Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kumsifia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kuwa amepunguza vurugu zilizokuwa zinatokea Mwanza mara kwa mara, akisema siku hizi hawasikii tena purukushani ya polisi, mgambo na wamachinga.
Mwandishi wa Mwananchi alishuhudia wamachinga wanaofanya biashara zao wakitoa vitu walivyopanga pembezoni mwa barabara, huku wengine wakikimbia.
Polisi mmoja alishambuliwa na wamachinga hao kabla ya kuokolewa na wenzake.
Wakati polisi wanapiga risasi za moto hewani, wamiliki wa maduka waliyafunga haraka huku wapita njia wakijipenyeza kwenye baadhi ya vichochoro ili kujinusuru.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo alisema walikuwa na operesheni ya kawaida ya kuwaondoa watu wasiofuata utaratibu wa kufanya biashara kwenye maeneo yasiyotakiwa.
Mkumbo alisema baadhi ya wafanyabiashara hao walitaka kuwagomea askari waliokuwa kazini na kwamba, polisi walilazimika kupiga risasi hewani ili kuwatawanya.
“Ni kweli kulikuwa na taharuki, lakini naomba niseme hakukuwa na madhara yoyote na hali hiyo ilitokea baada ya baadhi ya vijana kutaka kujaribu kutunishiana misuli na askari,”Mkumbo
NIPASHE
Serikali imeshauriwa kununua helikopta (Chopa) katika kila mkoa kwa ajili ya kufanya shughuli za zimamoto badala ya kutumia magari ambayo hayafiki kwa wakati katika maeneo ya matukio kutokana na msongamano wa magari barabarani.
Ushauri huo ulitolewa jana bungeni na Mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), Muhammad Ibrahim Sanya, alipokuwa akiuliza swali la nyongeza.
Katika swali lake, mbunge huyo alihoji kwanini serikali isiwe na utaratibu wa kununua Chopa kwa ajili ya kuwezesha vikosi vya zimamoto kutokana na miundombinu ya sasa kuwa mibaya ambayo pia inasababisha magari ya zimamoto kutofika katika maeneo ya matukio kwa wakati.
 “Tumekuwa tukishuhudia mara kadhaa moto unapotokea magari ya zimamoto yanashindwa kufika kwa wakati na hiyo ni kutokana na miundombinu kuwa mibovu. Ni kwanini serikali isione umuhimu wa kununua Chopa ili zitumike kuzima moto kuokoa maisha na mali za watu?,” alihoji.
Akijibu, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, alisema wanakubaliana na ushauri huo na kwamba fedha zitakapopatikana watanunua Chopa hizo na kuziweka katika miji mikubwa.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum, Fakharia Shomari Khamis (CCM), alisema wananchi wengi hawajui kuwa Kikosi cha Zimamoto ndicho chenye wajibu wa kuzima moto na badala ya yake hukimbilia polisi hivyo kukosa msaada wa haraka kuzima moto.
Aliitaka serikali kutoa elimu kwa wananchi ili matukio ya moto yanapotokea watoe taarifa haraka kwenye vikosi hivyo.
Akijibu, Silima alisema Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji ndicho chenye wajibu na dhamana ya kupewa taarifa za ajali na majanga.
Alisema katika kuhakikisha wananchi wanafahamu juu ya utoaji wa taarifa za ajali na majanga, kikosi hicho kinaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
NIPASHE
Zaidi ya madereva 100 wa treni ya Reli ya Kati, wameanzisha mgomo baridi kuanzia jana wakishinikiza madai yao mbalimbali kwa uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).
Hali hiyo imeelezwa kuwa inahatarisha maisha ya mamia ya abiria wanaotumia usafiri huo kutokana na dereva mwenye umri wa zaidi ya miaka 60, sasa kutumiwa kuendesha treni kwa muda mrefu.
Treni inayoendeshwa na mzee huyo mstaafu anayefanya kazi kwa mkataba, aliyefahamika kwa jina moja la Kisanga, iliondoka jana jijini Dar es Salaam kuelekea Mwanza na Kigoma.
Ilitarajiwa aendeshe treni hiyo mpaka Tabora, tofauti na utaratibu wa kawaida wa dereva mmoja kuendesha treni kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na kupokewa na mwingine.
Dereva anayepokea treni Morogoro hutakiwa kuendesha hadi Dodoma na mwingine huichukua hadi Tabora ambako madereva wa kuifikisha treni Kigoma na Mwanza huingia kazini.
Taarifa zilielezea jinsi Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ilivyojipanga kukabiliana na mgomo baridi huo wa madereva, kwamba ni kumuandaa Mkaguzi (Inspector) wa madereva hao, Zabron Kanuti, kupokea treni kwa Kisanga pindi itakapofika Tabora na kuifikisha Kigoma.
Treni iliyotakiwa kwenda jijini Mwanza, hadi kufikia jana saa 9:00 alasiri, haikuwa na dereva.
Aidha, treni iliyokuwa inatoka Kigoma kwenda Dar es Salaam nayo ilikwama Morogoro kwa muda mrefu kutokana na kukosekana kwa dereva aliyetakiwa kumalizia safari.
Treni iliyokwama Morogoro ni ile mpya inayofahamika kwa jina la Delux iliyotoka Kigoma kuelekea jijini Dar es Salaam, ilifika mjini Morogoro jana Saa 5:00 asubuhi lakini mpaka majira ya mchana haikuwa imeendelea na safari kutokana na kukosekana kwa dereva wa kuiendesha.
Taarifa za uhakika zilibainisha kuwa idadi kubwa ya madereva nchini kote hawapo kazini kutokana na sababu mbalimbali wengi wakitumia kisingizio cha kuumwa.
“Wengi wao wamepata vibali vya kupumzika kutoka kwa madaktari, ikielezwa kuwa wana matatizo kiafya lakini ukweli ni kwamba jamaa wanakatishwa tamaa na mazingira magumu kazini,” kilieleza chanzo muhimu cha habari.
Imeelezwa kuwa chanzo cha mgomo huo ni madereva hao kudai maslahi bora, usalama wa maisha yao, abiria na mizigo wanayosafirisha.
NIPASHE
Wakati leo ikiwa ni siku ya mwisho ya kupokea fomu za wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanaoomba kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kugombea kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu; wagombea 33 pekee ndiyo waliorejesha fomu hadi kufikia jana jioni huku wagombea tisa wakiwa bado.
CCM ilifungua pazia kwa makada wake kuanza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Juni 3, mwaka huu.
Wagombea ambao hawajarejesha fomu mpaka sasa, ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Ritha Ngowi, Hellena Dina Elinawinga, Anthony Chalamila, Banda Sonoko, Peter Nyalali na Mussa Mwapango.
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa CCM, Rajab Luhwavi, alisema kuwa wagombea tisa ambao hawajarejesha fomu hiyo, watapaswa kuzikabidhi kabla ya muda wa mwisho wa kupokea fomu za wagombea urais kufungwa rasmi leo saa 10:30 jioni.
“Mpaka sasa tumepokea fomu za wagombea wa urais 33 kati ya 42 waliochukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015. Muda wa mwisho kupokea fomu hizo kwa waliobaki ni kesho (leo) saa 10:30 jioni, tutakapochora mstari wa mwisho,” Luhwavi.
Baada ya kukamilika kwa kazi ya urejeshaji wa fomu, makada hao 42 watasubiri kufanyika kwa vikao vya juu vya maamuzi.
Vikao hivyo ni pamoja na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa itakayokutana Julai 7 na Kamati Kuu (CC) itakayokutana Julai 8, chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, ikifuatiwa na kikao cha Nec Julai 9, mwaka huu.
Mchakato wa kumpata mgombea urais atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, utahitimishwa Julai 11, mwaka huu na Mkutano Mkuu wa Taifa CCM ambao ni maalum kwa ajili kulipigia kura jina la mgombea mmoja kati ya watatu.
HABARILEO
Mwalimi wa Shule ya Msingi Kibumaye iliyopo tarafa ya Inchage wilayani Tarime mkoani Mara, Nelson Zachma  amekufa kwa kujitosa Ziwa Victoria.
Ilidaiwa kuwa mwalimu huyo alifanya uamuzi huo wa kujitosa majini alipokuwa safarini akitokea eneo la Kinesi kwenda Musoma mjini kwa kutumia usafiri wa kivuko.
Kaimu Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Sweetbert Njewike alisema kuwa tukio hilo la mwalimu Zachma kujitosa ziwani lilitokea Juni 24 mwaka huu majira ya mchana wakati mwalimu huyo akisafiri kwa kutumia kivuko kutoka Kinesi kwenda Musoma mjini.
“Kuna tukio la mwalimu mmoja wa shule ya msingi Kibumaye aliyejulikana kwa jina la Nelson Zachma (50) kujitosa majini, na tukio hili lilitokea Juni 24 mwaka huu majira ya mchana wakati akisafiri kuelekea Musoma mjini akitokea eneo la Kinesi,” Njewike.
Alisema mara baada ya kujitosa majini, juhudi za uokoaji zilifanywa na wapiga mbizi wa kivuko hicho lakini hazikuzaa matunda ndipo marehemu alipozama ndani ya maji na mwili wake kuopolewa siku tatu baadaye yaani Juni 30 katika mtaa wa Rebu Tarime.
Alisema sababu za mwalimu huyo kuchukua uamuzi wa kujitosa majini hazijajulikana na polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini nini chanzo cha mwalimu huyo kuamua kujiua.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo aliyejulikana kwa jina la Lucia Kibacho (40) alisema kuwa walipofika katikati ya kivuko, Zachma alimpatia namba za simu za ndugu zake na kumwomba awapatie taarifa zake na ndipo akajirusha ndani ya maji.
“Mimi nilikuwa nimekaa karibu naye, tulipofika katikati ya ziwa, akaniambia chukua hizi namba ni za ndugu zangu uwajulishe kuwa mimi nimejitosa majini na nimekufa, mara akajirusha majini,” Kibacho.
Lakini taarifa za awali zinaonesha kuwa, baadhi ya waombolezaji waliokuwa nyumbani kwa marehemu walisikika wakisema kuwa Zachma alikuwa na mgogoro wa ndani na mke wake na huenda ikawa ni moja ya sababu za yeye kuchukua uamuzi huo.
JAMBOLEO
Watu wanne, akiwamo baba na mtoto wake mwenye umri wa miaka sita, wamekufa papo hapo na wengine 33 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Fahisan Huwel,  walilokuwa wakisafiria kugonga treni la abiria mali ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) katika Kijiji cha Kibaoni wilayani hapa,  Mkoa wa Morogoro.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa mkoa huo, Musa Malambo, ajali hiyo ilitokea jana saa 1.30 asubuhi, wakati basi hilo aina ya Isuzu Jouney  likitokea Kijiji cha Tindiga wilayani humo kwenda mjini Morogoro.
Malambo alisema basi hilo lilipofika katika eneo hilo, liligonga treni hilo lililokuwa likitokea jijini Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Kigoma kisha kupinduka mara mbili na kusababisha vifo hivyo na majeruhi hao.
Alitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe wa dereva wa basi hilo lenye namba T837 CTN, Bakari Salehe Nyange, Mkazi wa Kilosa, kushindwa kuchukua hadhari alipofika kwenye eneo la makutano ya reli na barabara.
Aliwataja waliokufa kuwa ni Sarehe Gomba (35), Mkazi wa kijiji cha Tindiga; Mama Husna (33),  wa Mamoyo; mtoto huyo Surati Mwajili (6) na baba yake aliyefahamika kwa jina moja na Mwajili (38),  wakazi wa Pugu jijini  Dar es Salaam .
Alisema wanamshikilia dereva wa basi hilo ambaye ni mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, ambako amelazwa kwa matibabu.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya hiyo, Dk. Dennis Ngaromba, amethibitisha kupokea maiti wanne na majeruhi hao, akisema baadhi ya wametibiwa na kuruhusiwa kutokana hospitalini kutokana na hali zao kuwa nzuri.
Alisema majeruhi watano hali zao mbaya kutokana na kujeruhiwa vibaya kifuani na kichwani huku wengine wakiwa hawana fahamu na kuwahamishia   Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.
Mmoja wa abiria wa basi hilo, Rajabu Abdallah,  alisema tangu walipoanza safari katika kijiji cha Tindiga,  dereva wa basi hilo alibadili njia ya kawaida ya Kibaoni, Mamoyo, Mabwegere na kupitia Kimamba na kwamba kutokana na mvua kunyesha, aliamua kutumia njia fupi ya Kipolelo yenye makutano na reli.
Alisema akiwa katika njia hiyo alikuwa kiendesha basi hilo kwa mwendo kasi bila ya kuchukua tahadhari ya alama kwenye makutano ya reli na barabara na kuligonha treni hilo.

 


No comments:

Post a Comment

advertise here