Friday 24 July 2015

LOWASSA NA KAULI YA MSEMAJI WAKE KUHUSU KUJIUNGA UKAWA

LAYIII
BAADA ya vuta nikuvute katika vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuhusu kukubaliwa au kutokubaliwa kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa kujiunga na umoja huo ili kuongeza nguvu ya kisiasa, hatimaye mwanasiasa huyo maarufu nchini amekubaliwa na tayari amejiunga rasmi Ukawa akiwa mwanachama halisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imefahamika.
 

 

 Taarifa rasmi kutoka Ukawa na kwa msemaji wa Lowassa ambaye hakutaka jina lake litajwe, imeeleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa baada ya majadiliano ya kina katika Mkutano Mkuu wa Ukawa uliofanyika mapema wiki hii huku ajenda kubwa ikiwa ni kumpokea Lowassa ili kuimarisha kambi ya upinzani ikiwa ni pamoja na kumsimamisha kama mgombea urais wa umoja huo.
Taarifa rasmi zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa Lowassa anatarajiwa kutangazwa rasmi Jumapili hii hivyo maadalizi ya mkutano mkubwa wa aina yake yanaendelea. Chanzo chetu kutoka katika mkutano huo kilisema kwa moyo mmoja, wenyeviti wa vyama vyote vinavyounda umoja huo, yaani Freeman Mbowe (Chadema), Profesa

Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCRMageuzi) na Emmanuel Makaidi (NLD), wameridhia kuungana na Lowassa katika safari yao ya kuking’oa CCM madarakani huku wakiamini kuwa wakimsimamisha kuwa mgombea wa Ukawa watafanikisha azma ya vyama vya upinzani kuingia ikulu.
“Katika kikao chetu tulijadili mikakati kadhaa ya kuchukua dola lakini kubwa zaidi lilikuwa ni jinsi ya kuungana na Lowassa ili kutimiza azma hiyo, ikizingatiwa kwamba hivi sasa anaungwa mkono na Watanzania wengi na hasa jinsi ambavyo hawakuridhishwa na mchakato wa kumuengua kuwania urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo tuna uhakika kwa mkakati huu lazima tuking’oe CCM madarakani,” alisema mjumbe mmoja wa Mkutano Mkuu (jina limehifadhiwa).

TUNDU LISSU AFUNGUKA
Akizungumzia suala hilo, Mnadhimu Mkuu wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, aliliambia gazeti hili kuwa majadiliano kuhusu Lowassa yalikuwa ya lazima kwa kuwa katika muungano wa vyama kila kiongozi ana mtazamo wake hivyo, kila jambo la muhimu lazima lifanyike kwa majadiliano ili kufikia mwafaka kwani lengo ni kuhakikisha kwamba kunakuwapo na mkakati wa pamoja kuhakikisha kuwa CCM kinag’olewa madarakani ili makada wa chama hicho waelewe kuwa sasa Watanzania wanahitaji mabadiliko na si maneno matupu ya majukwaani.
LIPUMBA NAYE ANENA
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema kwamba Ukawa hivi sasa wamejipanga kimkakati kuhakikisha wanachukua dola na kuongeza kwamba waliokuwa wakieneza propaganda kuwa anawakwamisha wataendelea kuumbuka kwa kuwa vyama vyote vinavyounda Ukawa ni kitu kimoja.
Aliongeza kwamba, kamwe umoja huo hauwezi kusambaratika kwani ajenda kuu ni kuindoa CCM madarakani na kuongeza kwamba, mambo mengine kama mgawanyo wa ruzuku yatafuata baadaye kwani yanazungumzika katika ngazi ya uongozi.
MSIMAMO WA LOWASSA
Msemaji wa Lowassa ambaye kawa sasa ndiye gumzo la taifa ukiachana na Dk. John Magufuli aliyepitishwa na CCM kuwania kiti cha urais amelihakikishia gazeti hili kuwa Lowassa ameamua kuingia Ukawa ili kuendeleza siasa za kistaarabu kutimiza azma yake ya Safari ya Matumaini kama ambavyo amekuwa akiwaahidi Watanzania.
Alisema ameamua kuungana na Ukawa kwa kuwa anaamini kuwa lengo la vyama vyote vya siasa ni kuhakikisha vinatimiza malengo yao ya kuwahudumia wananchi, hivyo inapotokea katika chama kimojawapo, bado kuna nafasi ya kutumia vyama vingine kutimiza malengo ya kisiasa. Msemaji huyo aliongeza kwamba baada ya kuenguliwa alikuwa na kazi ngumu ya kubaini nini cha kufanya ili kutimiza azma yake ya kisiasa, ndiyo maana alikaa kimya ili kuepusha mivutano kati yake na CCM lakini hakuwa amekata tama kuhusu jinsi anavyoweza kuwakomboa Watanzania kutoka katika dimbwi la umaskini, jambo ambalo alikuwa akiwaeleza katika safari yake ya kusaka wadhamini nchi nzima.
MKAKATI WA KAMPENI
Msemaji huyo alisema kuwa akiwa katika Ukawa, Lowassa ameandaa mkakati kabambe wa uhamasishaji wananchi ili watambue kwamba azma ya kuwakomboa ipo palepale na kuongeza kuwa ana uhakika watamuunga mkono kwani anatambua kwamba wapo pamoja naye katika safari ya matumaini.
Alisema kwamba kazi iliyo mbele yake ni kuhakikisha kuwa anaisuka upya ‘Team Lowassa’ na atakuwa makini na baadhi ya watu waliomsaliti ili wasiharibu mkakati wake na kuongeza kwamba watazunguka nchi nzima kufanya kampeni za kistaarabu, zisizokashfu wanasiasa wengine ili wananchi wapime ni kiongozi gani anafaa kati ya yeye na wengine.

TATHMINI YA USHINDI
Chanzo chetu ndani ya Ukawa kilieleza kwamba, tathmini iliyofanywa hadi sasa inawapa uhakika wa kuchukua dola kwani katika maeneo mengi, Lowassa anaungwa mkono zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote yule. Kilisema kuwa katikamaeneo mengi CCM haikubaliki kutokana na kuendesha siasa za kibabe na mizengwe, jambo ambalo limekuwa likiwakera wananchi kwani kinachotokea ni kwamba wanachaguliwa viongozi badala ya wao kuchagua viongozi wanaowataka.
Kilisema Lowassa ana nguvu zaidi katika Mikoa ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kusini, Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar hivyo CCM kama inataka kushindana naye ijipange vyema.

ZITTO AJUMUISHWA
Katika mkakati huo wa ushindi, inaelezwa kwamba, umoja huo utamjumuisha kundini Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye chama chake nacho kitaongeza nguvu ya ushindi.
Lowassa alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM kati ya wagombea 38 ambao walichukua fomu lakini jina lake lilikatwa katika kikao cha Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM, jambo ambalo lilizua sintofahamu miongoni mwa wanasiasa wengi waliokuwa wakimuunga mkono, hatua ambayo ilisababisha mtikisiko wa kisiasa nchini.
  TUJIKUMBUSHE HAPA
 
Zipo taarifa za uhakika kwamba Edward Lowasa, Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya ufisadi wa Richmond anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari Jumapili tarehe 26 Julai 2015 Jijini Dar es Salaam. Katika mkutano huo, Lowasa anatarajiwa kueleza mambo mengi juu ya mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM uliopelekea jina lake kukatwa.
Pia katika mkutano huo, Lowasa anatarajiwa kutangaza rasmi kujivua uanachama wake ndani ya CCM na kujiunga na CHADEMA ambapo baadaye jioni ataelekea viwanja vya Mwembeyanga ambako ataungana na viongozi wengine wa CHADEMA kwenye mkutano wa hadharaza. Mtakumbuka kuwa uwanja huo wa Mwembeyanga uliopo Temeke Dar es Salaam ulitumika kutaja orodha ya mafisadi 11 na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Wilbroad Slaa mwaka 2007 ambapo jina la Lowasa lilikuwa miongoni mwa majina yaliyopo kwenye orodha hiyo.
Uamuzi wa Lowasa kwenda CHADEMA umetokana na kutimiza makubaliano ya kupeleka shilingi bilioni 10 ambapo fedha hizo zimekabidhiwa Jana Alhamis Tarehe 23 Julai 2015. Aliyekabidhi fedha hizo kwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ni Apson Mwang'onda na makabidhiano yamefanyika kwenye Hotel ya Sea Cliff huku tukio hilo likishuhudiwa na Kingunge Ngombale Mwiru na wengine ambao sitawataja kutokana na sababu maalum.
Taarifa zinasema kuwa kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa watu walioathirika na kukatwa kwa Lowasa hasa kutokana na fedha nyingi na muda kwa matumaini kuwa watakuwa "UPPER" baada ya Lowasa kushinda Urais. Miongoni mwao ni pamoja na Prof Juma Kapuya, Nazir Karamagi, Parseko Kone, Mgana Msindai, Kingunge Ngombale Mwiru, Mchungaji Gwajima, Andrew Chenge nk.
Hata hivyo, inadaiwa pia kuwa watu walio karibu na Lowasa akiwemo mfadhili wake mkuu Rostam Aziz ambaye amegoma kutoa fedha za kufadhili harakati za kwenda upinzani wanaendelea kumsihi kuwa asiende huko kwani atakuwa amejimaliza kabisa kisiasa. Pia inadaiwa kuwa mkewe Regina Lowasa amekuwa bitter sana na mpango wa mumewe kwenda upinzani na kwamba kwa siku kadhaa sasa amekuwa akiwafukuza wageni waliokuwa wanaenda nyumbani kwake hasa wale wa upinzani.
Hata hivyo, uamuzi wa Lowasa kwenda CHADEMA unatokana na msukumo wa maslahi binafsi baina ya Lowasa, Freeman Mbowe na wale waliomzunguka Lowasa na kwamba mpango huo ni hatari kubwa kwa ustawi wa CHADEMA. FREEMAN MBOWE anamtaka Lowasa kwa tamaa ya fedha ambapo matamanio yake yamekamilika baada ya kukabidhiwa shilingi bilioni 10 alizohitaji. Hata hivyo, upo uwezekano kuwa fedha hizo zikamtokea puani hasa pale atakaposhindwa kushawishi viongozi wa UKAWA kumteua Lowasa kupeperusha Bendera yao kwa mujibu wa makubaliano ya Lowasa na Mbowe.
Pia mtakumbuka kuwa Lowasa ameenguliwa CCM kutokana na kukiuka kanuni na taratibu za chama huku kashfa za ufisadi zikitumika kama kigezo kikuu cha kuenguliwa kwake. Lowasa huyu anayeenda CHADEMA ni Lowasa yule yule wa Kashfa za Richmond na kwamba CHADEMA wanapokea mtu ambaye taifa limemkataa.
Aidha, viongozi wa CHADEMA wamekuwa na kauli tofauti juu ya Lowasa huku Tundu Lissu na Wilbroad Slaa bila kumsahau Godbless Lema wakiongoza mashambulizi dhidi ya Lowasa. Mathalan, hotuba za viongozi hawa wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Arumeru Mashariki ambapo Nassari alikuwa anapambana na Sioi Sumari, Mkwe wa Lowasa zilitawala kashfa za Lowasa na kashfa hizo ndizo zilizopelekea Nassari kushinda. Pia, Dr Slaa amemtaja Lowasa kwenye list of shame na hajajitokeza kwenye vyombo vya habari na kutangaza kuwa amemuondoa kwenye Orodha hiyo.
Vilevile, shinikizo la Lowasa kwenda CHADEMA linafanywa na watu ambao image yao kwenye public ni mbaya. Watu kama Prof Kapuya, Nazir Karamagi, Andrew Chenge na wengineo hakika wanawakilisha kikundi cha watu ambao hawana taswira nzuri kwenye jamii.
CHADEMA wana wakati mgumu sana katika kumnadi Lowasa. Siku zote wamekuwa wakijipambanua kuwa chama chao kinapambana na ufisadi. Inashangaza kuwa wanaojinasibu kuwa wanapambana na ufisadi ndo wanapokea rushwa na wanakaribisha mafisadi kwenye chama chao.
Natambua kuwa CHADEMA wanataka kumtumia tu Lowasa katika uchaguzi Mkuu ujao na baada ya hapo watamtema. Hata hivyo watambue kuwa uamuzi huo si tu utakuwa na athari kwa Lowasa bali hata wao CHADEMA watakuwa wamejimaliza.
Nimalizie kwa kusema kuwa Lowasa huyu ambaye ameonekana mchafu ndani ya CCM hawezi kuwa msafi ndani ya CHADEMA.





No comments:

Post a Comment

advertise here