KATIKA makala ya afya wiki hii tuangalie sababu zinazosababisha mimba kuharibika.
Kuharibika kwa mimba ni hali ya mwanamke kupata ujauzito na ukatoka
kabla ya muda wake ambapo tatizo hili huangaliwa kabla ya kutimiza wiki
20 tangu kutungwa kwake.
Hali hiyo inapotokea huitwa kuwa mimba imetoka au imeharibika (Miscarriage).
Hali hii ya mimba kuharibika inakuwa tofauti kabisa na utoaji mimba
ambapo kitendo cha kutoa mimba kinafanywa na binadamu kwa makusudi na
huwa amedhamiria kufanya hivyo.
Akielezea tatizo la mimba kuharibika Daktari Msaidizi wa Kituo cha Afya
Nkwenda Wilayani Karagwe, Dk Aristides Ruhikula anasema kuwa katika hali
hiyo mtoto anakuwa hawezi kujitegemea mwenyewe kwa mahitaji
yanayotakiwa ikiwa ni pamoja na kupumua, hivyo hali hiyo ya
kutojitegemea husababisha kifo.
Sababu za mimba kutoka
- Anasema kuwa miongoni mwa sababu zinazosababisha mimba kutoka ni pamoja na umri mkubwa ambapo kwa kawaida mwanamke anapofikisha umri wa miaka 35 au zaidi misuli(sphencters) ya mji wa uzazi hulegea na kupunguza nguvu za kuweza kuhimili na kutunza kiumbe kinachokuwa ndani ya mji wa uzazi, hivyo kusababisha mimba kutoka.
- Hitilafu katika kizazi ambayo huwa katika mfuko wa mimba(uterus) ambao muundo wake siyo wa kawaida.Wanawake wenye tatizo kama hili huwa na hatari kubwa ya mimba kuharibika kabla ya miezi tisa.
- Aidha maambukizi ya fangasi au bakteria husababisha misuli ya kizazi kushambuliwa hivyo kupoteza uwezo wake wa kuhifadhi ujauzito hivyo mimba kuharibika. Miongoni mwa sababu zinazosababisha mimba kuharibika ni matatizo ya vinasaba(genetic factors)
- Hali hiyo hutokana na hitilafu katika kromosomu(cromosomal abnormalities) ambayo husababisha vinasaba kuwa katika hali isiyo ya kawaida ambayo hali hiyo ni miongoni mwa sababu kubwa zinazosababisha mimba kutoka kabla ya kutimiza wiki 13.
- Hii husababisha damu ya mama kushindwa kuendana na damu ya mtoto hivyo kutokea kwa madhara ambayo humdhuru mtoto na kumfanya ashindwe kuhimili hali ya tumboni kwa mama hivyo kutoka nje.
- Pia ukosefu wa homoni ya progesterone ambayo hufanya kazi kubwa tangu kutungwa kwa mimba hadi mtoto kuzaliwa ambayo huchochea uimara wa ukuta wa placenta ambao mtoto hujishikiza.
- Upungufu wa homoni hii husababisha ukuta wa mji wa mimba kushindwa kuhimili uzito wa mtoto, hali ambayo husababisha ujauzito kuharibika kabla ya muda wake.
- Sababu nyingine ni utumiaji wa pombe kali, sigara na dawa za kulevya.
- Utumiaji wa vitu hivi huchangia mimba kutoka kutokana na kemikali nyingi zilizomo.
- Hivyo mwanamke mjamzito hushauriwa kutotumia vitu vyenye kemikali, ili kulinda afya yake na mtoto aliyeko tumboni.
- Pia baadhi ya vyakula na vipodozi huwa vina kemikali ambazo hupelekea shingo ya kizazi kulegea na kadiri mimba inavyozidi kukua huendelea kuachia na kusababisha mimba kushuka,hali inayosababisha mimba kuharibika.
Dalili za mimba kuharibika(symptoms of a miscarriage)
- Dk Ruhikula anaeleza kuwa dalili zinazojitokeza wakati wa mimba kuharibika ni pamoja na kutokwa na damu sehemu za siri. Hiyo ni dalili kubwa ya mimba kuharibika ambapo damu hiyo hutoka sawa na mwanamke anayekuwa kwenye siku zake.
- Maumivu katika viungo ambayo huwa makali katika kiuno, nyonga na tumbo chini ya kitovu ambapo maumivu hayo huanza taratibu, lakini huongezeka kadiri muda unavyozidi kusonga mbele ambapo hali hiyo huambatana na kutokwa damu sehemu za siri.
- Dalili nyingine ni kutokwa na uchafu sehemu za siri. Hii ni dalili kubwa ya mimba kutoka. Mama mjamzito kuanza kutokwa na uchafu mwingi wenye rangi sambamba na mabonge ya damu.
- Kupata maumivu ya kiuno huku ukisikia maumivu hayo yanashuka chini kwa nguvu fahamu fika mimba yako inaweza kutoka muda wowote.
Madhara yatokanayo na kuharibika kwa mimba
- Iwapo mama mjamzito amepata tatizo hili na hajapata tiba sahihi kama kuna mabaki tumboni yanaweza kusababisha madhara mengine ikiwemo kizazi kuoza au kusababisha matatizo mengine kwenye mji wa mimba.
- Miongoni mwa madhara yanayoweza kumpata mama ambaye mimba imeharibika ni pamoja na kizazi kuharibika ikiwa mama hatasafishwa vizuri tumboni baada ya mimba kuharibika.
- Madhara mengine ni kuugua mfululizo baada ya ujauzito kuharibika pamoja na kushambuliwa na madhara mfululizo baada ya ujauzito kuharibika.
- Pia mama anaweza kupata madhara ya kisaikolojia ambayo yanachukua muda mrefu kusahaulika hasa pale wanapokutana na wanawake wajawazito au wenye watoto.
Matibabu
- Mwanamke mwenye tatizo la kuharibika kwa mimba anaweza kupata matibabu kwa njia mbalimbali kutegemea na mgonjwa husika.
- Matibabu hayo hupatikana hospitalini ambapo mwanamke anatakiwa kuwahi pale anapoona dalili hatarishi.
- Kwa yule mwenye historia ya kuharibika kwa mimba na tayari ana mimba atapata matibabu tofauti na yule mwenye tatizo hilo, lakini hana mimba kwa muda huo.
Ushauri
Dk anasema kuwa dalili zilizotajwa hapo juu peke yake hazitoshi
kuonyesha kuwa mimba imeharibika bali mama mjamzito anapoona dalili moja
kati ya hizi au zote hata hali ambayo haielewi anatakiwa kuwahi
hospitalini ili kuweza kupata vipimo.
Endapo mama huyo atachelewa atakuwa anajiweka katika hali mbaya kutokana
na sumu inayotokana na kiumbe kilichoharibika na kusababisha matatizo
kwenye mfuko wa uzazi ikiwemo ugumba.
Mwanamke yeyote ambaye hajapata tatizo hilo anashauriwa kula vyakula
kama maboga, mboga za majani na vyakula vyote vinavyojenga mwili.
No comments:
Post a Comment