MWANANCHI
Wakati Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye akitangaza kuihama CCM, alidokeza kuwa siku moja chama hicho kitaona umuhimu wake, na jana alianza kuonyesha hilo alipopangua hoja dhidi ya mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa huku akianika uozo wa Serikali.
Sumaye, ambaye hadi sasa hajatangaza anajiunga na chama gani, jana alikuwa kivutio kwenye uzinduzi wa kampeni za urais za Ukawa, ambayo inaundwa na vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, kiasi cha maelfu ya watu waliofurika kutaka aendelee kuzungumza licha ya muda kuwa finyu.
Akizungumza mbele ya umati huo mkubwa kwenye viwanja vya Jangwani, Sumaye alirejea tena sababu zilizomfanya aingie Ukawa kuwa ni haja ya kufanya mabadiliko wanayotaka Watanzania ambayo alinyimwa nafasi na CCM.
“CCM wanawajaza Watanzania kitu kinaitwa woga wa usilolifahamu au woga wa usilolijua kwa hiyo kila siku wanawaambia Watanzania mkiwapa wapinzani nchi itaingia kwenye vita,”Sumaye.
“Baada ya Lowassa kuliona hilo, na kujiridhisha kuwa Watanzania wanamfahamu akienda kuwasaidia, woga huo hautakuwepo tena.
“Hata mimi nimeingia upinzani kwa ajili ya kushirikiana na Lowassa kuleta mabadiliko nchini ili wananchi waanze kufurahia maisha bora.”
Lakini kelele za shangwe ziliongezeka wakati alipoanza kujibu hoja mbalimbali zinazotolewa na makada wa CCM dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani.
Sumaye, ambaye alishika nafasi ya uwaziri mkuu kwa kipindi chote cha miaka 10 ya Serikali ya awamu ya Tatu, alisema Rais Jakaya Kikwete alimteua Lowassa kuwa Waziri Mkuu katika Serikali yake, akisema ni jambo la kushangaza kuona leo mkuu huyo wa anamwona hafai.
“Kuna mtu anamuweka Waziri Mkuu asiyefaa? Lakini ni Lowassa huyu huyu aliyemwingiza Kikwete Ikulu,” alisema na kusababisha mlipuko wa kelele za shangwe.
Kuhusu kumhusisha Lowassa na ufisadi na kula rushwa, Sumaye alisema kama mbunge huyo wa Monduli ni fisadi na mla rushwa, mbona hakukimbia nchi tangu alipotoka madarakani mwaka 2008.
“Angekuwa fisadi si wangeshamweka mahali? Lowassa amechukua ustaarabu wa kujiwajibisha baada ya tatizo kuingia katika Serikali. Hivi nani mkubwa wa Serikali? Tangu lini waziri mkuu akawa mkubwa wa serikali?” alihoji.
Sumaye alieleza kuwa baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati fulani alitoa machozi kwenye kikao cha Halmashauri Kuu kuwa hajaona mtu mvumilivu kama Rashid Kawawa kwa sababu alikuwa akibeba mizigo ambayo ilipaswa kubebwa na Nyerere.
Lowassa alijiuzulu wadhifa huo mwaka 2008 baada ya Bunge kuunda kamati kuchunguza sakata la Serikali kuingia mkataba wa ufuaji umeme wa dharura na kampuni ya Richmond Development ya Marekani iliyobainika baadaye kuwa haikuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo.
MWANANCHI
Mgombea wa urais kupitia CCM, Dk John Magufuli amesema serikali yake itaimarisha masilahi ya wafanyakazi wote wakiwamo polisi, ili wasiwe wanalinda na kukosa fedha za kula nyumbani na hatimaye kusinzia vituoni na kunyang’anywa silaha.
Hii ni mara ya kwanza kwa Dk Magufuli kuzungumza kwa kina mpango wake wa kudhibiti wimbi la uvamizi wa vituo vya polisi, linalozidi kukua nchini na kuhatarisha maisha ya polisi na wananchi.
Akiwahutubia wakazi wa Makete, Dk Magufuli alisema anataka polisi wawe wanakwenda kazini wameshiba, hata jambazi akivamia wanamwua hapohapo bila kusubiri polisi jamii.
“Nazungumza kwa ukweli kwa sababu jeshi letu linatakiwa liheshimike, siyo mnakaa kwenye kituo watu wanachukua silaha wakati na ninyi mna silaha, “ alisema na kushangiliwa.
“Ninataka jeshi ambalo likimuona jambazi linamwasha kwa sababu yeye alikuja kuwawasha. Nataka iwe jiwe kwa jiwe, moto kwa moto, mguu kwa mguu, kichwa kwa kichwa, sikio kwa sikio, hayo ndiyo tunayoyataka.”
Dk Magufuli alisema maneno hayo huenda yakaonekana makali kwa baadhi ya watu lakini “hilo ndilo jibu”, na kwamba suala hilo linatakiwa kufanywa kwa kuzingatia sheria na utu wa binadamu.
Kauli hiyo aliirudia tena Njombe Mjini akisisitiza wakati wake “jambazi akija mchape risasi,” ili nchi iwe na amani na kuwafanya wananchi wafanye biashara zao kwa usalama kama nchi nyingine zilizoendelea.
Dk Magufuli aliahidi kujenga barabara ya lami kuanzia Njombe kupitia Makete hadi Mbeya, na kueleza kuwa usanifu na upembuzi yakinifu vimeshafanyika na kilichobaki ni kuanza ujenzi akiingia madarakani.
Pia, aliahidi kuboresha maisha ya wasanii nchini, akiahidi kuwaanzishia mfuko maalumu hivyo kuwataka wasihofu kuwa anawatumia tu kwa sasa wakati wa kampeni, bali atawajali hata baada ya kushinda.
Mgombea huyo aliyeingia mkoa wa tano wa kampeni zake alizungumzia ilani ya CCM, hasa suala la elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, mikopo ya Sh50 milioni kwa kina mama na vijana kila kata, kuboresha huduma za umeme, afya, maji, pembejeo na kuimarisha masoko kwa wakulima.
Waziri huyo wa Ujenzi, jana alikutana na Naibu wake, Gerson Lwenge katika mkutano uliofanyika Makoga, Njombe Magharibi na kila mmoja kumnadi mwenzake.
Lwenge alisema Dk Magufuli kuwa amefanya naye kazi na kwamba ni mfanyakazi na “mkali kwelikweli anayetenda haki.”
Akizungumzia afya yake, aliwataka Watanzania kutohofia akisema yupo imara. Aliwaambia wakazi wa Makoga wilayani Wanging’ombe kuwa yuko timamu na atapambana hadi mwisho.
Alieleza kuwa kuna uzushi umezuka kwenye mitandao ya kijamii kuwa anaumwa na amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), jambo ambalo siyo kweli.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amesema baadhi ya kauli zinazotolewa na Umoja wa Vyama vya Upinzani (Ukawa), zinaashiria uvunjifu wa amani pindi matokeo ya kura yatakapoanishwa baada ya zoezi la upigaji kura Oktoba 25 mwaka huu.
Rais Kikwete alisema baadhi ya kauli hizo zimekuwa zikionyesha wazi viashiria vya uvunjifu wa amani na upotoshaji kwa kundi kubwa la vijana ambao wanapiga kura kwa mara ya kwanza.
Akizungumza wakati akizindua Kampeni ya Mama Ongea na Mwanao jijini Dar es Salaam Rais Kikwete alisema;
“Wamediriki kusema wazi bila kificho kwamba patakuwa hapatoshi, hizi ni kauli zinazoashiria uvunjifu wa amani. Tunachokisema CCM ushindi kwetu ni lazima na tutashinda kwa kishindo na kwenda nginja nginja mpaka Ikulu.”
Kikwete alisema CCM imejipanga kuhakikisha inapata ushindi katika Uchaguzi Mkuu ujao na kuongeza kuwa ili kufanikisha hilo wamepanga kikosi kazi ambacho kitatembea nyumba kwa nyumba, chumba kwa chumba, mtu kwa mtu ikiwa kwa sasa tayari wameshaanza kufanya kampeni zao kupitia mtandao ya simu za mkononi.
Katika hafla hiyo ya kuzindua kampeni hiyo inayoratibiwa na msanii wa filamu na Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu, Rais Kikwete aliwataka wanawake kaungalia mazuri yote yaliyofanywa na Serikali ya CCM katika kumuinua mwanamke.
JAMBOLEO
Chama cha ACT – Wazalendo leo kinazindua kampeni zake za uchaguzi kwa kuwatambulisha wagombea wote wa ubunge waliosimamishwa kwenye majimbo ya Tanzania –Bara na Zanzibar.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika katika Uwanja vya Zakhem Mbagala, wilayani Temeke kuanzia saa nne asubuhi.
Hivi karibuni, Katibu wa Mipango na Mikakati wa ACT – Wazalendo, Habibu Mchange aliwaambia waandishi wa habari kwamba hafla hiyo itahudhuriwa na viongozi wote wa kitaifa wa chama hicho wakiwamo Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wake, Anna Mghwira ambaye pia ni mgombea urais.
“Baada ya mwenyekiti wetu, Mama Mghwira kuchukua fomu ya kugombea urais, Watanzania wamekuwa na shauku ya kutaka kujua mustakabali wetu kuelekea Uchaguzi Mkuu,” alisema na kuongeza: “Hivyo basi tunawakaribisha wananchi wote siku hiyo waje kushuhudia kampeni za kisayansi. Ndiyo maana tumeamua kuwaita wagombea ubunge wote kuhudhuria na kuwatambulisha rasmi kwa Watanzania.”
Alisema ACT – Wazalendo imejipanga kuchukua dola na kuleta siasa safi, tofauti na vyama vingine akisisitiza kuwa kina nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo ya Watanzania. Hivyo kuwataka wananchi kuhudhuria.
Alisema katika siku ya uzinduzi, kwa mara ya kwanza wabunge waliohama kutoka vyama vya CCM, CUF na Chadema watazungumza, pia wataendelea kuinadi ilani ya uchaguzi wa chama hicho. Alisisitiza kuinadi kaulimbiu ya chama hicho ya utu, uadilifu na uzalendo.
Katibu wa Fedha na Rasilimali ya chama hicho, Peter Mwambuja alisema pia kimejipanga kufanya siasa za malengo na masuala kwa maendeleo ya Watanzania siyo kupiga propaganda.
HABARILEO
Serikali ijayo, kama itaendelea kuongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) itajenga viwanda viwili kwa ajili ya kusindika mafuta ya alizeti na pamba katika mkoa wa Singida.
Mbali na kiwanda hicho, serikali ijayo ya CCM pia itajenga hospitali mkoani humo yenye ukubwa kama Hospitali ya Taifa ya Muhimbili itakayokuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa wananchi wa Kanda ya Kati na mikoa ya jirani.
Ahadi hiyo ilitolewa jana na mgombea mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza na wananchi wa Iramba Magharibi waliojitokeza katika kijiji cha Kyengege. Samia alisema kila kiwanda kitaajiri zaidi ya vijana 600 hivyo kutoa fursa ya ajira kwa vijana.
Iramba Magharibi ni ngome ya mgombea kiti cha ubunge kwa tiketi ya CCM, Mwigulu Nchemba. Samia alisema hatua za awali za mradi huo wa ujenzi wa hospitali zimekwishaanza katika mkoa huo.
Akiwahamasisha wananchi kujitokeza kwa idadi kubwa kuipigia CCM kura, Samia alisema hiyo ndio itakuwa njia pekee ya kumpa fursa ya kutekeleza ilani ya CCM mkoani humo.
Akimzungumzia mgombea ubunge wa CCM katika jimbo hilo la Iramba Magharibi, Samia aliomba wapigakura walioandikishwa kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi na kupiga kura kwenye vituo husika.
“Nina uhakika wote waliojiandikisha kupiga kuwa mtaipigia kura CCM na yeyote atakayepiga kura upande mwingine, ngoja niwaambie mtakuwa mmepoteza kura zenu,” alisisitiza.
Aliongeza: “Hakikisheni mnakamilisha majukumu yenu ya kila siku mapema na muache siku ya kupiga kura kwa ajili ya kufanya kazi hiyo moja. “ Mapema mgombea huyo wa Urais kwa tiketi ya CCM alifanya mkutano wa kampeni Singida Vijijini, kata ya Msange ambayo mgombea ubunge katika jimbo hilo ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Akiwa Singida vijijini, Samia aliahidi kushughulikia matatizo ya maji na kuwezesha upatikanaji dawa mahospitalini, kwenye vituo vya afya na zahanati pamoja na kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa. Alisema Mfuko wa Taifa wa Maji utakaoanzishwa utaongeza nguvu katika juhudi za kupeleka maji vijijini na kukabiliana na matatizo ya maji.
Alisema serikali yake itajenga mabweni kwa ajili ya shule za sekondari, hasa kwa ajili ya wasichana ili kuwalinda dhidi ya wanaume wanaonyemelea mabinti wadogo na kuwasababishia mimba za utotoni.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Singida Vijijini, Nyalandu alisema jimbo lake limekuwa na maendeleo makubwa chini ya chama tawala. Alisema visima vya maji vimeongezeka kutoka 14 hadi 100 chini ya miradi ya maji inayotekelezwa na CCM, zahanati pia zimeongezeka hadi kufikia 40 kutoka 14.
Katika elimu, Nyalandu alisema kulikuwa na shule mbili tu za sekondari wakati anaingia madarakani lakini sasa kuna shule za sekondari 28. Nyalandu alisema jimbo jirani lililo mikononi mwa mpinzani lina maendeleo kidogo na kuongeza kuwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu mkoa wote wa Singida utakuwa mikononi mwa CCM.
HABARILEO
MgombeaUrais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, amekanusha madai ya kuugua na kulazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), Katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.
Dk Magufuli alisema hayo jana wakati akishukuru uongozi wa CCM wa mkoa huo, kwa mapokezi mazuri tangu alipoingia katika mkoa huo Alhamisi wiki hii akitokea Rukwa.
Madai ya kuugua na kulazwa kwa Dk Magufuli, yalianzia juzi katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, alipokwenda kumjulia hali Meya wa Mbeya, Athanas Kapunga, aliyepata ajali Alhamisi wiki hii alipojiunga na msafara wake kwenda Makambako.
Meya huyo alipokuwa akitoka katika kijiji cha Nzoka kwenda Makambako baada ya kumpokea Dk Magufuli, akiwa nyuma ya msafara wa mgombea huyo, gari alilopanda liliacha njia na kupinduka ambapo mtu mmoja aliyekuwa amepewa lifti, alikufa na wengine akiwemo Meya huyo kujeruhiwa.
Kutokana na ajali hiyo, Dk Magufuli kabla ya kuanza ziara yake juzi mkoani Mbeya alikwenda kumjulia hali Meya huyo katika hospitali hiyo, ambako amelazwa Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), ndipo kukasambaa uongo huo kwamba amelazwa.
Mbali na kukanusha uvumi huo, Dk Magufuli aliushukuru uongozi wa CCM Mkoa wa Mbeya na wananchi kwa ujumla kwa makaribisho mazuri.
Katika mkoa huo amekuwa akipokewa na maelfu ya wananchi katika mikutano mikubwa na mamia katika mikutano midogo, ambako amekuwa akisimamishwa mara kwa mara na wananchi njiani, ambapo Dk Magufuli alisema mapokezi hayo yameonesha kuwa Watanzania wengi wanataka mabadiliko bora na si bora mabadiliko.
Mbali na shukrani hizo, pia aliupa pole uongozi huo wa CCM Mbeya na wananchi kwa msiba wa kada mmoja wa chama hicho, aliyekufa katika ajali hiyo iliyomjeruhi Meya.
HABARILEO
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la zabuni ya mabilioni ya pesa iliyopewa kampuni ya kufua umeme ya Richmond, Dk Harrison Mwakyembe, ametoa siri za kilichofanyika wakati wa sakata hilo la kifisadi.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa kampeni za mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli katika Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe jana, Dk Mwakyembe alielezea kushangazwa na kauli ya mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kuwa alipokea amri kutoka juu kuruhusu ufisadi wa Richmond.
Lowassa ambaye anaungwa mkono na vyama vya CUF, NLD na NCCR-Mageuzi katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili awanie urais, alipozungumzia kisa cha kujiuzulu uwaziri mkuu, baada ya kashfa hiyo kumgusa moja kwa moja, alidai alitaka kusitisha mkataba na kampuni ya Richmond, lakini akasitishwa kutokana na amri kutoka juu.
Kwa mujibu wa madai ya Lowassa, aliitisha kikao cha wataalamu wa serikali na kueleza nia yake ya kuvunja mkataba na kampuni hiyo, lakini katibu mmoja akatoka nje kuzungumza na simu na kurejea kikaoni na ujumbe kwamba mkuu ameruhusu iendelee.
Akielezea kushangazwa kwake na kauli hiyo jana, Dk Mwakyembe alisema kama Katibu Mkuu kamletea amri Waziri Mkuu na akaikubali, basi hicho cheo cha Waziri Mkuu, kilikuwa kikimpwaya.
Siri zaidi Alisema wakati akiongoza Kamati Teule ya Bunge kuchunguza ufisadi huo, alimuomba Rais Jakaya Kikwete, nyaraka za Baraza la Mawaziri, ili afuatilie mwenendo wa suala hilo.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, katika nyaraka hizo, alibaini Rais alikataa katakata, kukiukwa kwa Sheria ya Manunuzi wakati wa mchakato wa kutoa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura, kwa wazabuni walioomba kazi hiyo.
Pamoja na Rais kukataa kukiukwa kwa sheria hiyo, Dk Mwakyembe alisema kampuni hiyo iliyokuwa ya 18 kwa sifa, ilitolewa chini na kupewa nafasi ya kwanza na kupewa zabuni hiyo ya mabilioni ya fedha.
Dk Mwakyembe alisema analizungumzia hilo ili Watanzania waelewe na kumpa kura zote mgombea urais wa CCM, Dk Magufuli kwa kuwa ufisadi huo umelinyonya Taifa mpaka leo.
Juzi mkoani Mbeya, Dk Mwakyembe alikumbusha kuwa walikwenda mpaka Marekani kuchunguza uwepo wa kampuni hiyo iliyodaiwa kutoka katika nchi hiyo, na kukuta ni kampuni ya kuchapisha kadi za harusi.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, baada ya kubaini ubadhirifu huo, Lowassa alishinikizwa kujiuzulu, lakini hatua ya kiongozi huyo kutaka kwenda Ikulu, wazalendo hawawezi kuikubali.
Kuhusu madai ya Ukawa kwamba kwa nini kama kuna ushahidi hakupelekwa mahakamani, Mhadhiri huyo wa Sheria alisema kosa la jinai, halina ukomo na wakati wowote linaweza kufunguliwa mashitaka, huku akiapa kuwa anaweza kumfungulia mashitaka hata kesho.
Dk Magufuli Akizungumza katika mkutano huo, Dk Magufuli alishukuru kuendelea kupata mapokezi ya wananchi wa vyama vyote, wakiwemo wa Chadema na vyama vingine vinavyounda Ukawa vya NCCR-Mageuzi, CUF na NLD.
Alisema anataka kuongoza Tanzania yenye umoja na amani, ndio maana anaomba kura kutoka vyama vyote, kwa kuwa sasa ushindani wa vyama hivyo umeanza kuelekea katika uadui jambo ambalo si sahihi.
NIPASHE
Vioja katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu vimezidi kujitokeza ambapo jana mgombea ubunge katika Jimbo la Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba, amejikuta akimwaga sera kwa kutumia lugha ya Kinyiramba badala ya Kiswahili kama Sheria za uchaguzi zinavyosema.
Nchemba alitumia lugha ya Kinyiramba kwa madai ya kuwa anaweka msisitizo kwa wapiga kura ambao walikusanyika katika kijiji cha Kengege katika jimbo la Iramba Magharibi mkoani Singida.
Akizungumza na wapiga wananchi hao, Nchemba alisema, atakayeacha kujitokeza kupiga kura wenzake watamsaka ili kujua kwa nini hakujitokeza siku ya kupiga kura.
Alisema mwaka huu idadi kubwa ya wapiga kura kuwa wamejitokeza kujiandikisha na kwamba atashangaa kama siku hiyo watu watalala majumbani mwao badala ya kwenda kupiga kura.
Mwigulu alisisitiza kwamba kila kitu amemalizana na wapiga kura wake na kwamba wanachosubiri ni kwenda kuichagua CCM siku ikifika.
Hata hivyo, alisema bado kuna tatizo kubwa la maji jimboni kwake jambo ambalo awamu ya tano ya serikali kama itakuwa ya CCM italimaliza.
Kwa upande wake, mgombea ubunge katika Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyarandu, alitumia helikopta (Chopa) yenye namba za usajili, 5H-FCG, ambayo iliwavuta wananchi wengi kila ilipotua kwa kuikimbilia.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Msange jimbo la Singida Kaskazini, Nyarandu alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita mambo mbalimbali yalifanyika ikiwamo kuboresha huduma za maji, afya na shule.
Alitoa mfano katika kipindi chake cha miaka mitano ameweza kuongeza shule kutoka mbili hadi 28 pamoja na kusambaza huduma ya maji na vituo vya afya.
NIPASHE
Shirika la Umeme nchini (Tanesco), limetoa sababu ya kukatika kwa umeme katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam kuwa imetokana na uunganishaji wa mitambo katika gridi ya taifa.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Msemaji wa Tanesco, Adrian Severin, alisema Shirika hilo lilitoa taarifa kwa umma mapema kuhusu kukatika kwa umeme. Alisema katika eneo la Kinyerezi Wilaya ya Ilala, mkandarasi alikuwa akitengeneza mtambo wa umeme ambao utaunganishwa kwenye gridi ya taifa.
Alisema kukatika kwa umeme hakuhusiani na mkutano wa uzinduzi wa kampeni za mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa ambaye pia anaungwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Shirika letu halina uhusiano na siasa na wala halina nia ya kuhujumu Ukawa,” alisema.
Alisema mkandarasi alipewa muda wa kukamilisha kazi hiyo ifikapo Septemba, mwaka huu kinyume na muda huo, Shirika litaingia hasara.
NIPASHE
Mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Peter Msigwa, amesema hatavumilia propaganda zinazosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ya kumchafua yeye na mgombea urais kupitia chama hicho, Edward Lowassa.
Msigwa alisema kuwa kuna watu wanaozusha kwenye mitandao ya kijamii kuwa amepewa pesa za kununua watu ili waweze kufika kwenye mkutano wa Chadema utakaofanyika leo mjini hapa.
Nasikitika kwa yaliyotolewa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa mimi nimepewa milioni 200 kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kununua, kusomba, kuwapatia madereva bodaboda ili waweze kufika kwenye mkutano wa hadhara wa Edward Lowassa utakaofanyika siku ya Jumapili Agosti 30, alisema.
Ni dhahiri kuwa maneno hayo yaliandikwa pengine na watu wanaotumiwa na wapinzani wangu kufifisha hali na moyo wa kujitolea kwa viongozi wa chama, wafuasi na wananchi na wapiga kura wetu wa jimbo la Iringa mjini, alisema Msigwa.
Aidha, alisema Chadema hakijawahi wala hakina mpango wa kusomba wananchi au kutoa fedha ili wahudhurie mikutano yao bali chama hicho kimekuwa kikichangiwa fedha na wananchi na wamekua wakijitolea bila kulipwa hata senti tano.
Alisema kuwa chama hicho kimejipanga kufanya kampeni za kistaarabu zisizo na matusi na zinalenga na kujikita kwenye kuendeleza na kuwaambia wananchi ni kitu gani kinatakiwa kufanyika ili waweze kuondokana na umasikini na ndio imekuwa hoja yake kwa wananchi.
Alisema kuwa kwa sasa Chadema kimeshashinda na mbinu pekee waliyobaki nayo CCM ni kutaka kufanya kampeni chafu za kukichafua chama hicho na kilitahadharisha jeshi la polisi kuchukua hatua pindi watakapoona vurugu.
Alisema kuwa jimbo la Iringa Mjini litazindua kampeni zao rasmi Septemba 12 ili kueleza wananchi sera na dira ya jimbo la Iringa na taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa jimbo la Iringa mjini limepewa fursa kubwa ya kutembelea na mgombea urais atawahutubia wananchi wa mkoa huo.
Alisema Lowassa ataanza kuhutubia wananchi wa Ilula, Mafinga, Pawaga, Kalenga na baadaye Jimbo la Iringa Mjini.
NIPASHE
Rais wa Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu, Jaji Agustino Ramadhani, amesema hajawahi kupatwa na wazimu wa kufikiria kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aliyasema kuhusu taarifa zilizoenea kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, kwamba yeye na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, wapo katika mipango ya kuhamia kambi ya upinzani.
Jaji Ramadhani ambaye alikuwa mmoja kati ya makada 42 waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM, jina lake lilikatwa na Kamati ya Maadili kabla ya kufikishwa mbele ya Kamati Kuu (CC) ya chama hicho.
Jaji Ramadhani ambaye alikuwa kimya tangu mchakato huo umalizike, alisema taarifa hizo na yeye ameziona kwenye mitandao.
Hizo taarifa hata mimi niliziona kwenye mitandao ya kijamii, kwamba mimi na Mh. Bilal tutazungumza na vyombo vya habari kutangaza kuhama chama na kwamba tutasindikizwa na mzee Warioba (Jaji Joseph Warioba), wanaoeneza hayo ni watu wasiyo na adabu, sijawahi kupatwa na wazimu wa kufikiria kuhama CCM, alisema.
Alisema yanayoenezwa kwenye mitandao dhidi yake, kuhusiana na kuhama chama hayana ukweli wowote.
No comments:
Post a Comment