Tuesday, 16 June 2015

KILICHO MPONZA DIAMOND TUZO ZA KILI HIKI HAPA

Waandishi Wetu
Tuzo za Muziki za Kili 2015, Jumamosi ya wiki iliyopita zilitimua vumbi kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Mwenge jijini Dar es Salaam ambapo maelfu ya Watanzania wanaopenda burudani walikuwa wakifuatilia mwenendo mzima wa tuzo hizo, ambapo msanii Ali Kiba aling’ara baada ya kunyakua tuzo tano na kumuacha mbali hasimu wake mkubwa, Nasibu Abdul ‘Diamond
Platinumz’ aliyeambulia tuzo mbili tu.
Staa wa Bongo Fleva, Linah Sanga 'Lina' (kushoto) akiwa samabamba na 'Boss Mtoto'.
Mpango mzima ulianza, mishale ya saa tatu za usiku ambapo wasanii pamoja na wadau mbalimbali walijumuika kwenye zulia jekundu na kupiga ‘mapichapicha’ ya ukumbusho kabla ya mchakato wa kutoa tuzo haujaanza.
Vanesa Mdee na Jux wakifuatilia tuzo hizo kwa karibu.
Baada ya hapo, pazia la burudani lilifunguliwa na msanii chipukizi, Ruby anayetamba na ngoma yake ya Na Yule, akafuatiwa na Ommy Dimpoz, baadaye akapanda jukwaani Barnaba Elias sambamba na Vanessa Mdee, akapanda Christian Bella kisha Weusi wakiongozwa na Joh Makini na Nikki II wakafunga pazia la burudani kwa kukamua ile mbaya.
 ALI KIBA ANG’ARA
Ali Kiba.
Baadaye ulifuatia mchakato wa kutoa tuzo ambapo msanii Ali Kiba, alizoa tuzo tano; Mtumbuizaji Bora wa Mwaka, Wimbo Bora wa Mwaka (Mwana), Mtunzi Bora wa Mwaka (Bongo Fleva), Wimbo Bora wa Afro (Mwana) na Mwimbaji Bora wa Kiume (Bongo Fleva) huku hasimu wake Diamond Platinumz akiambulia tuzo mbili tu; Wimbo Bora wa Zouk/ Rhumba (Nitampata Wapi) na Video Bora ya Muziki ya Mwaka (MdogoMdogo).
 KILICHOMPONZA DIAMOND NI HIKI
Diamond Platinumz.
Kutokana na matokeo hayo, inaelezwa kuwa kilichomponza msanii Diamond Platinumz ni ujumbe wake aliowahi kuutuma kwenye mitandao ya kijamii, akiziponda Tuzo za Kili kwamba hazizingatii vigezo, kwa kuwaacha wasanii wanaofanya vyema kwenye tasnia ya muziki na badala yake, ‘kuwapendelea’ baadhi ya wasanii kutokana na sababu binafsi za waandaaji.
“Unajua Diamond alikosea sana kuziponda Tuzo za Kili kwa sababu ndizo zilizompaisha mwaka jana, matokeo yake amempa nafasi mpinzani wake, Ali Kiba kung’ara kwa kunyakua tuzo kibao, nafikiri atakuwa amejifunza jambo,” alisema Bruno Sanga, mmoja kati ya wadau waliohudhuria utoaji wa tuzo hizo.
 WASHINDI WENGINE
Ukiachilia mbali Ali Kiba na Diamond, wengine walioziteka tuzo hizo ni mwanadada Vanesssa Mdee aliyenyakua tuzo mbili; Mtumbuizaji Bora wa Mwaka (Kike) na Mwimbaji Bora wa Kike (Bongo Fleva), Mzee Yusuph; Mwimbaji Bora wa Kiume Taarab, Mtunzi Bora wa Mwaka (Taarab) na Kundi Bora la Taarab (Jahazi).
Wengine ni Jose Mara aliyenyakua tuzo mbili, Isha Mashauzi, Joh Makini, Baraka Da Prince (Msanii Bora Chipukizi), Nahreel (Mtayarishaji Bora wa Mwaka) na Mrisho Mpoto aliyeondoka na Tuzo ya Wimbo Bora Wenye Vionjo vya Asili (Waite).
Sauti Sol walinyakua Tuzo ya Wimbo Bora wa Afrika Mashariki (Sura Yako), Profesa Jay (Wimbo Bora wa Hip Hop - Kipi Sijasikia), Jux (Wimbo Bora wa R&B- Sisikii) na Wimbo Bora wa Bendi wa Kiswahili iliyokwenda kwa FM Academia (Vijana wa Ngwasuma) na Bendi Bora ya Mwaka (FM Academia) huku Yamoto Band wakinyakua tuzo ya Kikundi Bora cha Mwaka (Bongo Fleva).

No comments:

Post a Comment

advertise here