LAYIII
NIPASHE
Kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu
mkoani Kigoma, imeelemewa baada ya idadi ya wakimbizi kutoka Burundi
kuzidi kuongezeka hivyo kuzidi uwezo wake kama inavyotakiwa na sheria za
Umoja wa Mataifa (UN).
Mkurugenzi Idara ya Wakimbizi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Harrison Mseke,
alisema bado wakimbizi wa Burundi hawajaanza kurudi nyumbani kwao bali
hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na idadi yao kuendelea kuongozeka.
Kwa mujibu wa Mseke, hadi sasa wakimbizi
katika kambi hiyo kutoka Burundi, wamefikia 71,000 na ndani ya wiki
moja iliyopita wameingia wakimbizi 10,000.
Alisema kwa sasa idadi ya wakimbizi wote kutoka Burundi na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), katika kambi hiyo ni takribani 100,000.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, idadi
hiyo ni kubwa kupita kiasi kwani sheria za UN kupitia shirika lake la
kuhudumia wakimbizi duniani (UNHCR) kambi moja inapaswa kuhudumia wakimbizi wasiozidi 50,000.
“Kuna
tatizo kubwa la eneo la kuwaweka kwani wakimbizi wote kutoka Burundi na
DRC, bado wanahifadhiwa katika kambi ya Nyarugusu. Kwa sheria za
Umoja wa Mataifa, kambi moja inatakiwa kuwa na wakimbizi 50,000, lakini
sasa wapo zaidi ya 100,000.
Mseke, alisema hadi sasa serikali
inafanya utaratibu wa kujenga kambi nyingine ili kupunguza idadi hiyo na
kuangalia uwezekano wa kuwatenganisha wakimbizi hao kutoka nchi hizo.
Ongezeko la wakimbizi kutoka Burundi,
limechangiwa na vurugu za kisiasa zinazoendelea nchini humo baada ya
Rais wake, Pierre Nkurunzinza, kutangaza kuwania urais kwa kipindi
kingine cha tatu hivyo kudaiwa kukiuka katiba ya taifa hilo.
NIPASHE
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
amelezea hofu yake juu ya kuwapo kwa fitina zinazofanywa na baadhi ya
watu kwa nia ya kuwaharibia wengine katika mchakato unaoendelea wa
makada 42 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaowania kuteuliwa kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho.
Pinda ambaye pia ni mmoja wa makada
waliochukua fomu kutaka kuteuliwa kuwa wagombea wa urais wa CCM, alisema
namna pekee ya kuwaepuka watu wanaofitinisha wenzao ni kutowaunga
mkono.
Aidha, Pinda aliwataka pia watangaza nia
wenzake watakaoshindwa katika kinyang’anyiro hicho kukubali matokeo na
kumuunga mkono yeyote atayeibuka mshindi na pia kutambua kuwa
‘asiyekubali kushindwa si mshindani’.
Pinda aliyasema hayo wakati akihutubia
kwenye viwanja vya Mashujaa mjini hapa wakati akifunga sherehe za
maadhimisho ya wiki ya Serikali za Mitaa.
Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwapo
kwa amani na utulivu nchini hata baada ya uchaguzi kumalizika, huku
akiwaasa wanasiasa wote kujiepusha na vitendo vya fujo kwani hazina tija
kwa taifa na kwamba siasa ni ushindani ambao kila mtu anatakiwa
akubaliane na matokeo.
“Acheni
kuweka chuki zisizo na tija, haitowasaidia. Acheni kutaka kuwafanyia
fujo wale watakaokuwa wamekubalika katika ngazi mbalimbali kutuongoza,
maana wengine kazi yao ni fitina tu na wanataka mambo yaende ovyo.
Mzalendo wa kweli ni yule anayekubali, kama kura hazikutosha hazikutosha
tu,”.
Alitoa wito pia kwa wakurugenzi wa
halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wanasimamia vizuri uchaguzi
mkuu pale mchakato utakapoanza. “Agizo
langu kwa wakurugenzi, tunakwenda katika uchaguzi mkuu. Tusifanye mzaha
na chaguzi hizi, hakikisheni mnasimamia vizuri kama sheria
zinavyoelekeza na kama kanuni zinavyoelekeza,” aliongeza.
Mwenyekiti wa Jumuia ya Umoja wa Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, alisema baadhi ya halmashauri nchini zimefanikiwa kupunguza tatizo la uhaba wa madawati kwa zaidi ya asilimia 80.
NIPASHE
Kwa mara nyingine tena Bunge lilichafuka
jana na kulazimika kuahirishwa kwa muda baada ya wabunge wa upinzani
kugomea nia ya kuruhusu miswada mitatu ya mafuta na gesi, kuingizwa
bungeni na kujadiliwa kwa hati ya dharura.
Kikao hicho cha 41 kilishindwa kuendelea baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, pale Mbunge wa Ubungo, John Mnyika,
alipoomba mwongozo baada ya kukabidhiwa orodha ya shughuli za jana,
ambayo alisema imekiuka kanuni za Bunge kwa kuweka miswada mitatu kwa
ajili ya majadiliano.
Miswada hiyo ni wa sheria ya Petroli,
usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi na wa sheria ya uwazi na
uwajibikaji katika tasnia ya uchimbaji Tanzania; yote ya mwaka 2015.
Mnyika aliomba muongozo huo kwa kutumia
kifungu cha 53(6), masharti ya uwasilishaji wa hoja kama hiyo bungeni,
na kanuni ya 86 inayoeleza siku ambayo muswada uliokwisha kujadiliwa na
kamati umepangwa kwenye orodha ya shughuli, Waziri, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Mwenyekiti wa Kamati au Mbunge mwenye muswada husika
atawasilisha hoja kwamba muswada wa sheria kusomwa mara ya pili.
“Kipindi
cha uhai wa Bunge hili na miswada iliyowahi kuja, hoja ikishatolewa ni
lazima ijadiliwe iamuliwe ndiyo ije nyingine, hapa tumeletewa orodha
yenye hoja juu ya hoja kwa vyovyote haipaswi kukubalika bali kuondolewa, “alisema na kuongeza:
“Uamuzi
wa kuileta miswada hii kwa hati ya dharura umekiuka kabisa msingi wa
mwelekeo wa makubaliano kwenye semina iliyofanyika Juni 30, mwaka huu,
wabunge kwa wingi walikataa miswada hiyo isiletwe kwa hati ya dharura na
utaratibu huu.” alifafanua na kuongeza:
“Naomba
mwongozo wako na naomba usiseme utautoa wakati mwingine, ndiyo mana
sikutaka kusema tangu mwanzo, kwa sababu ukisema wakati mwingine huku
shughuli zikiendelea kuharibika ni jambo lisilokubalika, tunahitaji
majibu sasa, kwanini tuendelee na ‘order paper’ iliyokiuka kanuni na
makubaliano ya wabunge.”
Aidha, Spika Anne Makinda, alihamaki na kumtaka Mnyika kufuta kauli zenye kumwamrisha ndipo aweze kutoa mwongozo juu ya jambo hilo.
Baada ya Mbunge huyo kuondoa kauli hiyo,
Spika Makinda alisema hakuna mtu yeyote anayeweza kumwamrisha na kwamba
kanuni zipo sahihi na zimefuatwa hivyo upinzani wanatumia kanuni
kudanganya umma.
Baada ya maelezo hayo, zilizuka kelele na Makinda aliwataka waamue wenyewe huku akisisitiza kuwa hakuna kanuni iliyovunjwa.
Palizuka kelele nyingine huku wengine
wakirusha maneno kuwa tokeni nje, lakini wapinzani walisisitiza hakuna
wa kutoka, hali iliyosababisha kutokusikikizana na Spika kutangaza
kuhairisha Bunge huku wabunge wa upinzani wakiimba hatutaki kuibiwa na
kutaka kukutana ukumbi wa Msekwa.
Hata hivyo, walishindwa kutumia ukumbi
huo baada ya wabunge wa CCM kukubaliana kukutana ukumbi wa Msekwa na
kuwalazimu upinzani kubaki ndani ya ukumbi wa Bunge.
Baada ya wabunge wa CCM na Mawaziri
kutoka nje, wabunge wa kambi rasmi ya upinzani kwa umoja wao walibaki
ndani ya Bunge na kutoa msimamo wa pamoja baada ya majadiliano ya dakika
20.
Tundu Lissu alisema
ndani ya siku sita tangu Juni 27, mwaka huu serikali imeleta miswada 10
yote kwa hati ya dharura, akisema ni kwa ajili ya kuigonga muhuri kwa
muundo wa funika kombe wanaharamu wapite.
JAMBOLEO
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,
imetupilia mbali pingamizi nne kati ya nane zilizowasilishwa na kampuni
ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL)
na nyingine mbili kupinga maazimio ya Bunge kuhusiana na sakata la
uchotwaji wa mabilioni ya fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow
iliyokuwa Benki Kuu Tanzania (BoT).
Maamuzi hayo yalitolewa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Gadi Mjemas,
akisema anatupilia mbali mapingamizi hayo kwa mujibu wa sheria Ibara
ya 100 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayokataza kulipeleka jambo
lolote mahakamani linalojadiliwa bungeni.
Jaji Mjemas alifafanua kuwa mihimili
miwili, Bunge na Mahakama, haiwezi kuingiliana katika utendaji wake wa
majukumu na ndiyo sababu imetupilia mbali pingamizi hizo
zilizowasilishwa na IPTL na wapeleka maombi wengine katika kesi hiyo,
Harbinder Singh Sethi na Pan Africa Power Solution Ltd (PAP).
Alisema pia kuna pingamizi nyingine nne
zilizowekwa na kampuni hizo zilishakataliwa, hakuna sababu ya kuendelea
na pingamizi zilizobaki.
Wajibu maombi katika kesi hiyo ya
kikatiba Namba 59 ya mwaka 2014, ni Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Spika wa Bunge na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wapeleka maombi hao walikuwa wakiitaka
Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama
kuwachukulia hatua stahiki za kisheria wote waliotajwa na taarifa
maalumu ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)) kuhusika na
kashfa ya uchotaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta
Escrow.
Pia wanadai kuwa kilichofanyika ndani ya Bunge ni kinyume cha Katiba na kina lengo la kugombanisha mihimili mitatu ya dola.
Wanadai Bunge lilijadili suala hilo bila ya kujali kesi zinazoendelea mahakamani.
Licha ya kampuni hizo kutoa pingamizi
hizo, Desemba 31 mwaka jana serikali nayo iliwasilisha mapingamizi nane
katika mahakama hiyo kupinga maombi ya IPTL juu ya maazimio
yaliyopitishwa na Bunge hilo.
HABARILEO
Tanzania imepiga hatua katika mapambano dhidi ya malaria baada ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn kuzindua kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu, jana.
Kiwanda hicho kinachojulikana kama Tanzania Biotech Products Limited
kilichopo Kibaha ni cha kwanza Afrika na kitakuwa kikizalisha viuadudu
vya viluwiluwi vya mbu katika mazalia yao bila kuleta athari kwa
wananchi.
Rais Kikwete katika hotuba yake wakati
wa ufunguzi wa kiwanda hicho ambacho ujenzi wake umesimamiwa na Shirika
la Taifa la Maendeleo (NDC), alisema kiwanda hicho kitaimarisha uwezo wa kukinga na kuzuia maambukizi ya malaria nchini.
Wahenga wamesema daima: “Kinga ni bora kuliko tiba”.
Sasa tuna uhakika kuwa mapambano yetu dhidi ya malaria tumeyafikisha
mahali pazuri. Nafurahi kuona leo (jana) tunatamka kwa vitendo kuwa
“Malaria Haikubaliki,” alisema.
Alisema anajivunia anaondoka madarakani
akiwa amehakikisha Watanzania wako mahali salama katika mapambano dhidi
ya malaria na kuongeza kuwa nchi imefanikiwa kupunguza maambukizi ya
malaria kutoka asilimia 18 mwaka 2007 hadi asilimia 10 mwaka 2012,
wakati vifo vinavyotokana na malaria vimepungua kwa asilimia 71.
Rais Kikwete aliieleza NDC kuwa jukumu
kubwa lililo mbele sasa ni kuhakikisha kiwanda hicho kinazalisha na
kujiendesha kibiashara na kwamba hatarajii kiwanda hicho kujiendesha kwa
hasara maana biashara yenyewe ni ya uhakika ndani na nje ya nchi yetu.
Alielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa kukitumia kiwanda hicho katika mipango
yake ya kutokomeza malaria katika halmashauri zao kwa kuhamasisha watu
na kaya zilizo kwenye maneo yao ya utawala kutumia dawa zinazozalishwa
na kiwanda hicho.
Alisema mradi wa kiwanda hicho ni matokeo ya ziara yake nchini Cuba 2009, ambapo alitembelea kiwanda cha Cuba LABIOFAM ambacho kinatumia teknolojia hiyo huharibu mazalia ya mbu.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dessalegn akiwa Mwenyekiti wa wa Umoja wa Marais wa Afrika walio katika Mapambano Dhidi ya Malaria (ALMA)
aliahidi kufanya kampeni kwa nchi za Afrika kutumia bidhaa kutoka
katika kiwanda hicho ili kupambana na malaria katika bara hilo.
“Naamini
kiwanda hiki ni muhimu na hatua ya kubwa katika mapambano dhidi ya
malaria barani Afrika. Hatua hii itatusaidia kupungua tatizo la malaria
mara moja na kwa bara zima,”.
Balozi wa Cuba nchini Jorge Luis Lopez alisema uzinduzi wa kiwanda hicho ni alama ya ushirikiano na urafiki mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Dk Chrisant Mzindakaya
alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha viuadudu wa viluwiluwi
vya mbu lita milioni sita kwa mwaka na kuongeza kuwa kiwanda hicho pia
kitakuwa kikizalisha aina mbalimbali za mbolea kwa ajili ya matumizi ya
ndani na kuuza nje.
HABARILEO
Watia nia wanne waliochukua fomu za
kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa wagombea wa kiti cha
urais wametupwa nje ya mchakato huo, baada ya kushindwa kurudisha fomu.
Walioshindwa kurudisha fomu hizo mpaka muda wa mwisho ulipofika saa 10.00 jioni jana ni Peter Nyalali, Helena Elinewinga, Anthony Chalamila na Dk Muzamil Kalokola.
Mmoja wa watia nia hao, Helena mara
baada ya kuchukua fomu Juni 25, mwaka huu, alikwenda kumtembelea mmoja
wa maofisa wa chama hicho akitafuta ushauri wa namna ya kufanya ili
kupata udhamini, lakini baadaye aliamua kutelekeza fomu hizo bila
kuondoka nazo.
Jumla ya wanachama 42 walijitokeza
kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba uteuzi huo ambapo walitakiwa kuwa na
wadhamini 450 kutoka mikoa 15, ikiwemo mitatu ya Zanzibar.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Rajab Luhwavi alisema zoezi la kuchukua fomu lilianza Juni 3, mwaka huu na lilitarajia kumalizika Julai 2 saa 10.00 jioni.
Alisema zoezi hilo limefanyika kwa
utulivu ambapo kati ya wanachama 42 waliochukua fomu na kutakiwa kuwa na
wadhamini kutoka mikoa 15 ikiwemo mitatu ya Zanzibar ambapo kati ya hao
ni 38 ndio waliofanikiwa kurejesha fomu.
Alisema hatua itakayofuata ni mchakato wa vikao vya chama kuanzia Jumanne wiki ijayo.
“Mmoja
wa wachukua fomu, Helena Elinawinga alitelekeza fomu hizo kwa mmoja wa
maofisa wa CCM baada ya kufika kuomba ushauri huku akitaka kupewa kwanza
elimu ya siasa kabla ya kuanza kutafuta wadhamini,”Luhwavi.
HABARILEO
Kikongwe Yohana Msumari
anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 80, ameuawa kikatili kwa
kutenganishwa mwili na kichwa na kisha wauaji hao kukihifadhi kichwa
hicho kwenye mfuko wa plastiki chini ya mwembe.
Hata hivyo mtu anayesadikiwa kufanya
mauaji hayo, alisakwa na wananchi wenye hasira na kisha kukamatwa na
kuonesha mwili wa marehemu huyo na yeye kupigwa na hatimaye kuuawa pia.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea
juzi, katika kijiji cha Mamboleo, Kata ya Bwembwera wilayani Muheza
mkoani Tanga, ambapo kikongwe huyo aliondoka na kijana ambaye naye
hakutambulika jina lake mwenye umri wa kati ya miaka 35-40 wa kabila la
Kinyaturu, ambaye alikuwa mfanyakazi za vibarua kwenye mashamba ya watu.
Akisimulia tukio hilo, Katibu Kata wa
Chama Cha Mapinduzi kwenye Kata ya Bwembwera, Achi Semhando alisema
tukio hilo la kusikitisha lilitokea kwenye kata yao na kwamba polisi
walifika baada ya kupewa taarifa hizo na kuchukia maiti.
“Kwa
kweli ni tukio la kusikitisha, huyu mzee aliondoka na huyo kijana na
kwenda kumuonesha sehemu ya kufyeka shambani kwake, ila hadi jioni huyu
mzee hakurudi na ndipo wananchi waliingiwa na wasiwasi na kuamua
kumtafuta huyo kijana aliyeondoka naye,” Semhando.
Kijana huyo alipatikana na wananchi
walimtaka aseme mzee huyo alipo na ndipo aliwapeleka hadi shambani na
kuona maiti ya mzee huyo na ndipo walianza kumpiga hadi umauti wake na
kisha kutoa taarifa polisi.
Hata hivyo maiti ya mzee huyo haikuwa na
kichwa na polisi walizichukua maiti zote mbili na kwamba ilipofika jana
asubuhi, watoto waliokuwa wakiokota maembe kwenye miti waliona mfuko
umefungwa na walipouchunguza waliona kichwa na kutoa taarifa kijijini.
HABARILEO
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imeshindwa kumsomea maelezo ya awali Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya kutumia lugha ya matusi na kushindwa kuhifadhi silaha.
Kesi hiyo ilitajwa jana kwa ajili ya
washitakiwa kusomewa maelezo ya awali lakini iliahirishwa kwa kuwa
Hakimu Mkazi Wilfred Dyansobera anayesikiliza kesi hiyo hakuwepo
mahakamani.
Hakimu Mkazi, Thomas Simba
aliahirisha kesi hiyo hiyo Julai 20, mwaka huu kwa ajili ya washitakiwa
hao kusomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Dyansobera.
Mbali na Gwajima washitakiwa wengine, ni Mlinzi wake, George Mzava, Msaidizi wake, Yekonia Bihagaze na Mchungaji Georgey Milulu wanakabiliwa na shitaka la kukutwa na silaha pamoja na risasi kinyume cha sheria.
Katika kesi ya kwanza namba 85, Gwajima
anadaiwa kati ya Machi16 na 25, mwaka huu katika Viwanja vya Tanganyika
Packers Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam alitoa lugha ya matusi dhidi
ya Askofu wa Kanisa Katoliki Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akimueleza Askofu kwamba ni mtoto, mpuuzi asiye na akili katika namna ya kwamba ingeleta uvunjifu wa amani.
Katika kesi nyingine namba 84 , Gwajima
anakabiliwa na mashitaka ya kushindwa kuhifadhi silaha na risasi jambo
ambalo ni kinyume cha sheria ya uhifadhi wa silaha za moto.
Anadaiwa kati ya Machi 27 na 29, mwaka
huu, ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, alishindwa kuhifadhi silaha
aina ya Beretta namba CAT 5802, risasi 3 za pisto na risasi 17 za
shotgun.
Katika mashitaka mengine yanayowakabili
washitakiwa wengine, inadaiwa Machi 29, mwaka huu katika Hospitali ya
TMJ Mikocheni ‘A’ walikutwa wakimiliki silaha na risasi hizo bila ruhusa
kutoka mamlaka husika.
MTANZANIA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo iliahirisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR)
katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani hivi karibuni, sasa
imesema utafanyika kuanzia Julai 7 hadi 20 kwa Mkoa wa Pwani na Julai 16
hadi Julai 25 kwa Jiji la Dar es Salaam.
Uboreshaji wa daftari hilo kwa Jiji la
Dar es salaam na Mkoa wa Pwani uliahirishwa kutokana na kuchelewa kwa
vifaa vya uboreshaji kutoka mikoani ambavyo vilipelekwa ili kuongeza
ufanisi kutokana na maeneo hayo kuwa na idadi kubwa ya watu wenye sifa
ya kuandikishwa kuwa wapiga kura.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Julius Mallaba
aliwataka wananchi wote wa mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye vituo
vya uandikishaji vitakavyokuwa kwenye vijiji, vitongoji na mitaa ili
kujiandikisha waweze kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka katika
Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.
Aliwataja watakaohusika na zoezi hilo
kuwa ni watu wote waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea na wale
watakaotimiza miaka 18 ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.
Wengine ni waliojiandikisha awali kwenye
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la zamani ili kuhuisha taarifa zao na
kupata kadi mpya za kupigia kura.
Aidha Mallaba aliwataja wengine wenye
sifa ya kujiandikisha kuwa ni wale wote wenye sifa za kujiandikisha
lakini hawajawahi kujiandikisha kwenye daftari hilo.
Alisema wale wote wenye kadi za kupigia
kura za zamani wanatakiwa kwenda na kadi zao ili kurahisisha uchukuaji
wa taarifa zao na kadi hizo zitarudishwa NEC na watapata vitambulisho
vipya.
Wananchi wanatakiwa kujiandikisha katika
vituo vilivyopo ndani ya kata zao ili kuweza kupata fursa ya kumchagua
diwani, mbunge na rais.
MWANANCHI
Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema kuwa ana imani vikao vya kuwachuja wagombea wa urais vitafanya uamuzi kwa msingi wa kujiamini na siyo kwa hofu.
Makamba alisema hayo mjini Dodoma jana baada ya kurejesha fomu za
kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
mwaka huu.
“Kama chama tumepata nafasi ya
kupitia michakato mingi migumu kuliko hata huu, tumefanya uamuzi katika
mambo mengi na makubwa na bado tumeendelea kubaki kuwa wamoja. Nina
imani hata katika hili pia tutavuka salama,” Makamba.
Alisema wananchi wengi hasa vijana wanaangalia CCM itamteua mgombea
wa aina gani na wanataka aina mpya ya uongozi ambao unaangalia mbele na
unaoakisi matarajio yao.
Makamba alisema wana-CCM, kama walivyo wananchi wote, wanachukizwa na
rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na wanachukizwa na chama chao
kuhusishwa na masuala hayo.
Alisema CCM wanataka wagombea kwa nafasi za ngazi zote ambao wana
mvuto kwa watu na ambao itakuwa rahisi kuwanadi bila kuwatolea maelezo
au utetezi kwanza.
Alisema katika kuomba nafasi hiyo ni vyema kutosahau kwamba bado yupo
Rais ambaye amefanya kazi nzuri na anaendelea kuifanya iwe nzuri zaidi.
“Tusizungumze kana kwamba
hakuna kilichofanyika. Yeyote atakayepata heshima ya kuliongoza Taifa
letu ataanzia alipoishia Rais Jakaya Kikwete,” alisisitiza.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema nafasi ya urais ni
ya hadhi, heshima na dhamana kubwa hivyo ni muhimu kujitafakari kwa kina
kabla ya kuiomba.
Lakini pia ni muhimu kuiomba kwa staha, unyenyekevu na hekima na kwa
namna inayoendana na hadhi, heshima na dhamana ya nafasi yenyewe.
No comments:
Post a Comment