SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma imesema ipo tayari kuhakiki
mali za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, endapo watapokea
malalamiko kutoka kwa wanaomtilia shaka.
Hivi karibuni wakati akitangaza orodha ya watu wanaotuhumiwa kuuza,
kuagiza na kutumia dawa za kulevya, Makonda alijikuta akiingia katika
vita ya maneno na wabunge.
Msingi wa vita yenyewe ni hatua ya baadhi ya wabunge kupinga utaratibu
alioutumia Makonda kuwataja
kwa majina watuhumiwa hao na hata kwenda mbali zaidi wakimtuhumu na kuhoji alikopata utajiri wa ghafla.
kwa majina watuhumiwa hao na hata kwenda mbali zaidi wakimtuhumu na kuhoji alikopata utajiri wa ghafla.
Hatua ya kuhoji mali za Makonda ilichochewa na kauli ya Mkuu huyo wa
Mkoa ambaye alionekana kukerwa na ukosoaji wa wabunge hao na hivyo
kuwatuhumu wawakilishi hao wa wananchi kulala bungeni na kuitikia kila
kitu ndiyoooo.
Akizungumza ili kupata ufafanuzi kwa upande wa sekretarieti hiyo juu ya
madai hayo ya utajiri wa Makonda na iwapo aliziorodhesha kama sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma ya 1995 inavyoelekeza, Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano wa sekretarieti hiyo, Joseph Ishengoma, alisema chombo hicho
kipo tayari kufanya uhakiki endapo watapokea malalamiko rasmi kutoka
kwa wananchi au wabunge waliosikika hivi karibuni wakizungumzia suala
hilo bungeni.
Alisema kinachotakiwa ni kufuata utaratibu ambao ni kupeleka malalamiko
kwa sekretarieti hiyo kuomba kufanyika kwa uhakiki wa mali za kiongozi
huyo kutokana na tuhuma walizozitoa.
Kauli hiyo ya sekretarieti imekuja ikiwa imepita takribani wiki moja sasa tangu wabunge na Makonda washambuliane kwa maneno.
Miongoni mwa wabunge walioonekana kukerwa na kauli pamoja na utaratibu
alioutumia Makonda na hata kutaka naye achunguzwe ni Mbunge wa Rombo
(Chadema), Joseph Selasini, ambaye alikwenda mbali na kutaja mali
zinazodaiwa kumilikiwa na Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Akichangia taarifa za Kamati za Bunge za Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge na Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Selasini alisema Makonda
amenunua jengo (apartment) lenye thamani ya shilingi milioni 600.
“Makonda amenunua apartment pale Viva Towers kwa shilingi milioni 600,
Makonda amempa mke wake gari aina ya Mercedez Benz lenye thamani ya
Dola 250 za Marekani (shilingi milioni 550) kama zawadi ya birthday,”
alisema Selasini.
Siku moja kabla ya Selasini kusema hivyo, Mbunge wa Geita Vijijini,
Joseph Rushaku (Msukuma), naye aliibuka na tuhuma nyingine nzito dhidi
ya Makonda na kutaka vyombo husika vimchunguze.
“Mheshimiwa Spika, nasimama kwa kanuni ya 68(7) kuhusu jambo
lililojitokeza jana (juzi) wakati wa mjadala wa Bunge…naomba mwongozo
wako.
“Mimi binafsi naunga mkono jitihada za Rais kukamata wauza dawa za
kulevya, lakini dalili ya kwanza ya kuanza kumhisi mtu kama
anajishughulisha na biashara ambazo hazieleweki, kwanza ni mwenendo wa
mtu yeyote…si mbunge wala si nani.
“Anatumia Lexus ya petroli ya Sh milioni 400, lakini imekarabatiwa
ofisi (yake) ya RC Dar es Salaam kwa zaidi ya Sh milioni 400 bila
kufuata utaratibu wa manunuzi wa Serikali.
“Ana ma-V8 na Mwanza amejenga jengo la ghorofa…ni kina nani wanaotakiwa
kujadiliwa na kufanyiwa uchunguzi? Na hawa mawaziri tulionao humu
kwanini wamepigwa ganzi? Utawala bora, Mambo ya Ndani na Waziri wa
Sheria…kwanini mmepigwa ganzi?”
Msukuma pia alihoji anakopata fedha Makonda za kwenda Paris na Marekani
na kukaa siku 21 hasa ikizingatiwa kuwa tiketi moja ni Dola za
Kimarekani 14,000 huku yeye na mkewe jumla ikiwa ni dola za Kimarekani
28,000.
Kutokana na hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Sekretarieti hiyo,
Ishengoma, alisema wabunge hao baada ya kutoa malalamiko ya kutilia
shaka mali za Makonda, wanatakiwa kulipia kiasi cha shilingi 1,000 na
kisha watapewa faili kwa ajili ya kuangalia na kujiridhisha mali ambazo
Makonda alizitaja kwao.
Alisema na hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995.
Alisema kwa kuzingatia Katiba na sheria hiyo, Sekretarieti itakuwa na
wajibu wa kupokea hati za tamko rasmi zinazohitajika kutolewa na
viongozi wa umma kwa mujibu wa Katiba au sheria nyingine yoyote.
Alisema kifungu cha 18 (b) kinaeleza kuwa; Sekretarieti itapokea
malalamiko na taarifa za ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa
umma kutoka kwa wananchi.
Kifungu cha 18 (c) Sekretarieti itachunguza tuhuma yoyote ya kuvunjwa
kwa sheria ya maadili ya viongozi wa umma na viongozi wote wa umma
wanaopaswa kuwajibika chini ya sheria hiyo.
Alisema pia sekretarieti katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa
vipengele hivyo, itakuwa na mamlaka ya kupokea na kusikiliza malalamiko
yote kuhusu kiongozi yeyote wa umma yawe kwa mdomo au kwa maandishi
kutoka kwa si tu wabunge hao bali kwa mwananchi yeyote bila kuuliza
majina na anwani za watu waliopeleka malalamiko hayo.
Kwa mujibu wa sheria ya maadili ya mwaka 1995 (23) (1) endapo mtu
mwenye wadhifa wa waziri au wa mkuu wa mkoa amekiuka miiko hiyo
malalamiko yanaweza kuwasilishwa kwa rais na mtu yeyote kwa maandishi
yaliyotiwa saini, anwani na jina la mlalamikaji.
Zaidi, Ishengoma alisema taarifa ya mali za Makonda pamoja na viongozi
wengine ziliwasilishwa katika ofisi yao Desemba 31, mwaka jana kwa
mujibu wa sheria.
Alisema pamoja na hayo hatamzuia mtu kupeleka kile anachokijua ili waweze kufanyia kazi.
“Sheria hii yenyewe inampa mtu ‘Comsumption’ kama Kamishna wa Tume ya
Maadili ataangalia kama mali zake zina ushahidi na ofisi inaweza kufanya
uhakiki wa kupata taarifa sahihi kama alificha hizo mali hapo awali au
la na hatua ya kwanza atapewa kubadilisha.
“Na kama Kamishna akiridhia kuwa amedanganya basi atapelekwa katika
Baraza la Maadili na anayelalamika anakuwa ni miongoni mwa mashahidi na
kitakachofuata atajitetea na chombo hicho kitatoa mapendekezo,” alisema
Ishengoma.
SELASINI ANENA TENA
Akizungumza kwa njia ya simu jana na gazeti hili lililotaka kujua iwapo
atapeleka malalamiko katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
kutaka kuhakiki mali za Makonda kama alivyomtuhumu bungeni, Selasini
ambaye yupo jimboni kwake Rombo alisema hawezi kupeleka malalamiko kwa
kuwa viongozi wengi ni waongo.
Katika hilo wao wamekwishataja na kilichobaki ni vyombo vya uchunguzi kufanya kazi hiyo.
“Watu wamejaza mali zao majina ya shemeji zao, wake zao, watoto wao,
mahawara zao hivyo kupeleka malalamiko sisi ni kujidanganya tu.
“Sisi tumeshasema na si lazima tupeleke malalamiko, hapa kinachotakiwa
ni vyombo vya uchunguzi vifanye kazi zake, kwani havina watu wa
kuchunguza kuanzia safari ya Ufaransa siku 21 kwa kwenda Airport
kuchunguza alivyoondoka,” alihoji Selasini.
Alisema hakuna haja ya vyombo vya uchunguzi kutupia aliouita mzigo kwa
watu wengine huku akisema endapo atapeleka malalamiko shahidi atatakiwa
awe yeye mwenyewe na hana muda wa kupoteza katika hilo.
Alisema siku ambayo alimtuhumu Makonda kumiliki mali hizo alipomaliza tu
na kutoka alifuatwa na mtu aliyemtaja kuwa wa usalama na kumweleza kuwa
Makonda Dodoma ana viwanja 19 na vipo kwa jina lake.
“Hilo nalo watataka tupeleke malalamiko, hapana wanatakiwa kufika tu
Ardhi Dodoma na kuangalia jinsi ambavyo alivyoviandikisha vyote kwa
majina yake, lakini kwa kupeleka malalamiko hatutafika katika hili na
hutampata mtu, vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yake tu,” alisema
Selasini.
Alisema kuundwa kwa chombo hicho lengo lake nikuwa na viongozi wenye
maadili hivyo kama watashindwa kufanya hivyo itakuwa ni kwa sababu ya
kuingia katika siasa.
MSUKUMA
Alipotafutwa Msukuma kuelezea kama ana nia ya kupeleka malalamiko, alisema hiyo si kazi yake.
“Hizo ni kazi za Spika wa Bunge yeye ndiye anatakiwa kunipigia simu na
kuniambia nipeleke malalamiko au wanipe maelekezo nifanye hivyo na si
mwandishi,” alisema na kukata simu ghafla.
No comments:
Post a Comment