Friday, 17 February 2017

BARABARA YA KONGWA ARUSHA KUJENGGWA KWA KIWANGO CHA LAMI

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaanza kufanya upembuzi na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Arusha – Kiteto – Kongwa ili ijengwe kwa kiwango cha lami.

Alitoa kauli hiyo juzi wakati akizumgumza na mamia ya wakazi wa mji wa Orkesumet, wilayani Simanjiro akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara.

Alisema serikali imepanga kuiombea fedha za kazi ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa km 430 kwenye mkutano ujao wa bajeti na kwamba imepanga kutafuta wakandarasi wengi na kuwagawa kwa vipande ili barabara hiyo ijengwe kwa kipindi kifupi.

“Barabara yenu nimeiona. Imo kwenye Ilani ya CCM. Ujenzi wake utaanzia Arusha –Mbauda –
Simanjiro – Kiteto hadi Kongwa. Rais John Magufuli ameahidi kuwa Serikali hii haitawaangusha na itawahudumia wananchi wote bila kujali itikadi za kisiasa,” alisema.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa maji kwenye mji wa Orkesumet ambao ni Makao Makuu ya wilaya ya Simanjiro, Waziri Mkuu alisema serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji kutoka Ruvu hadi kwenye mji huo.

Kuhusu upatikanaji wa umeme, Waziri Mkuu aliwahakikishia wakazi hao nia ya Serikali ya kufikisha umeme katika vijiji vya wilaya hiyo.

“Serikali imeamua kupeleka umeme kwenye vijiji 8,000 na kati ya hivyo, vijiji vya Simanjiro vimo… serikali imepanga kufikisha umeme kupitia miradi ya REA.

Wakandarasi wameshapewa kazi, na sasa wameenda kutafuta vifaa.

Tumeamua hivi sasa kama kuna vijiji vya mbali na line ya umeme, au ni gharama sana kuwapelekea umeme kwa sababu ya umbali, hao ni lazima wapatiwe umeme wa sola na tutaweka sola katika kila nyumba,” alisema.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo Mei 30, mwaka huu kazi hiyo iwe imekamilika katika wilaya ya Simanjiro.

Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi ambayo iliandikwa kwenye mabango, Waziri Mkuu alimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Zephania Chaula afuatane na Ofisa Ardhi wa Wilaya na waende kwenye vijiji husika kusikiliza malalamiko ya wananchi hao.

Akifafanua kuhusu baadhi wa watu kujimilikisha maeneo makubwa ya ardhi, Waziri Mkuu alisema Sheria ya Ardhi namba 5 inaainisha kuhusu umiliki wa ardhi na kwa Serikali ya Kijiji hairuhusiwi kutoa ardhi zaidi ya ekari 50.

No comments:

Post a Comment

advertise here