Sunday, 12 February 2017

PAUL MAKONDA AFUNGUKA KUHUSU KUHOJIWA NA BUNGE



MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema hawezi kufika mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kuhojiwa kwa kuwa hajapokea barua ya kuitwa.

Akizungumza  jana jijini Dar es Salaam, Makonda alisema hatoweza kwenda mbele ya kamati hiyo bila barua rasmi iliyomtaka kufanya hivyo.

Bunge lililokuwa likiendelea na vikao vyake Dodoma kabla ya kuahirishwa juzi, lilipitisha uamuzi wa kuwataka Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alaxander Mnyeti, kufika mbele ya kamati hiyo na kuhojiwa kutokana na kauli walizozitoa, zinazodaiwa kuudharau mhimili huo wa dola.

Lakini Makonda alisema jana “hilo suala la mimi kuitwa kwenye kamati nalisikia na kulisoma kwenye magazeti."

"Sina uhakika ni lini wamefikia uamuzi huu wa kuniita na hata kama wamefikia uamuzi huo, sijaletewa barua rasmi.”


Baada ya Bunge kupitisha uamuzi huo wa kuitaka Ofisi ya Bunge iwaandikie barua viongozi hao, juzi baadhi ya wabunge walihoji kauli ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, kwamba azimio la chombo hicho cha kutunga sheria kumtaka Makonda kufika mbele ya kamati kujieleza kuhusu tuhuma za kuudharau mhimili huo, halikufuata utaratibu.

Hatua hiyo iliamsha hasira kwa baadhi ya Wabunge na kuomba mwongozo kuhoji kwa nini Katibu wa Bunge ametoa kauli ambayo inakinzana na makubaliano ya Bunge.

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara na mwezake wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa (wote Chadema) walihoji kuhusu kauli ya Dk. Kashililah.

Waitara alisema, “Asubuhi ya leo ( juzi) nimetumiwa ‘clip’ ya sauti ya Katibu wa Bunge akikosoa uamuzi wetu hapa na pia gazeti la Habari Leo, Ukurasa wa 25, kuna habari imeandikwa.

Katika taarifa hii, Katibu wa Bunge anasema maazimio ya Bunge yalikosewa na hayakufuata utaratibu,” alisema na kuongeza kuwa: “ Kwa maana nyingine, hatatekeleza kile tulichokubaliana.”

Mchungaji Msigwa wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, alieleza kuwa hajafurahishwa na kauli ya Katibu wa Bunge.

Alisema Katibu wa Bunge amekosea kwenda katika vyombo vya habari na kudai chombo hicho cha kutunga sheria kimekosea kwa kuwa anafanya kazi ya Bunge na kwamba hajaajiri wabunge na anapaswa kufuata maagizo yao.

Hoja ya kutaka kina Makonda washughulikiwe iliwasilishwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) katikati ya wiki na ilijadiliwa na kuungwa mkono na wabunge wote, wakiwamo mawaziri kwa kusema ‘ndiyo’.

No comments:

Post a Comment

advertise here