Saturday 11 February 2017

KAMISHNA MPYA DAWA ZA KULEVYA AFUNGUKA




Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemteua Rogers Sianga kuwa kamishna mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

Baada ya kuteuliwa Sianga alizungumza na Mwananchi na kusema kwanza anamshukuru Mungu kwa uteuzi huo na akaahidi kushughulikia kwa karibu kesi za vinara wa ‘unga’.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais jana, Gerson Msigwa ilisema Sianga atasaidiwa na Mihayo Msikela atakayekuwa Kamishna wa Operesheni na Fredrick Kibuta atakayekuwa Kamishna wa Intelijensia.

Uteuzi huo umekuja siku chache baada ya Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema) kumtaka
Rais Magufuli kuteua kamishna mkuu wa tume hiyo, ambayo imekaa bila kiongozi tangu Sheria ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ilipotungwa mwaka 2015.

“Tusifanye siasa kwenye vita hii ya madawa ya kulevya, tusimwongopee Rais kwa kutaka kuhakikisha vyeo vyetu tumwambie ukweli.

“Ili kumsaidia Rais anapaswa kumteua kamishina wa hii tume maana tangu tulipopitisha sheria hiki chombo hakina kamishna, tutakapohakikisha hicho chombo kinapata kamishna kwa kumsaidia Rais tutakamata wale wanaoingiza dawa za kulevya, wale mapapa na si hao wanaokamatwa sasa hivi,” alisema Bulaya.Mbali na Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alishauri bungeni kuwa mapambano ya dawa za kulevya hayatafanikiwa bila kuiwezesha tume hiyo kifedha.



Sianga afunguka

Akizungumza na Mwananchi Sianga alisema kwanza anashukuru Mungu kwa uteuzi huo, akaahidi kushughulikia kwa karibu kesi za vinara wa ‘unga’.

Kuhusu vigogo na wafanyabiashara maarufu walitajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Sianga aliyekuwa Moshi mkoani Kilimanjaro, alisema akifika Dar es Salaam atakutana na watendaji wengine waangalie cha kufanya.

“Ndiyo kwanza nimeteuliwa bado nipo Moshi nikifika Dar es Salaam, nitazungumza na wenzangu naamini tutashirikiana na tutashughulikia kwa msingi wa sheria.

Pia, alitoa onyo kwa watu wanaolima mirungi au bangi nchini.

“Dawa hizo nyingine za kulevya ni ghali na zinaletwa kutoka nje ya nchi, lakini mirungi na bangi tunajua inalimwa nchini hao wakulima waache walime mazao ya vyakula, maana dawa hizo zinaleta madhara makubwa kwa maendeleo ya taifa,” alisema.Uteuzi huo umekuja ikiwa pia ni siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuanza kutangaza majina ya watu anaotaka waripoti polisi kuhusiana na vita hiyo.

Huku kukiwa na maoni tofauti kuhusu hatua hiyo, Makonda ameahidi kutangaza orodha nyingine ya tatu ikiwa ni sehemu ya mapambano yake ya dawa za kulevya.

Washukiwa hao wamekuwa wakiripoti katika kituo kikuu cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kabla ya kupelekwa mahakamani.

Mbali na uteuzi huo, Rais Magufuli pia amemteua Dk Anna Makakala kuwa kamishna mkuu wa idara ya Uhamiaji.

Kabla ya uteuzi huo, Dk Makakala alikuwa mkuu wa chuo cha Uhamiaji mkoani Kilimanjaro.

Taarifa hiyo imesema wateule hao wataapishwa kesho Ikulu ya Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

advertise here