LAYIII
Wakati baadhi ya wabunge wa upinzani wakishikiliwa na polisi ama
kutafutwa kutokana na chaguzi kile kinachoelezwa ni vurugu kwenye
chaguzi za Meya na wenyeviti wa halmashauri zinazoendelea, wale
waliotolewa Bungeni kwa nguvu Januari 27, wote wametakiwa kufika Dar es
Salaam wahojiwe.
Mpaka sasa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, anashikiliwa na polisi kwa
kile kilichoelezwa ni vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi wa Meya wa
Dar es Salaam kuahirishwa Februari 27, mwaka huu.
Mbali na Mdee ambaye jana ilidaiwa kuwa polisi walifanya ukaguzi
nyumbani kwake pamoja na ofisini kwake huku kile wanachokitafuta kikiwa
hakijulikani, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) na wa Ubungo,
Saed Kubenea, pia inadaiwa wanatafuwa kwa sababu ya vurugu hizo.
Mbunge mwingine wa Chadema anayetafutwa na polisi ni Peter
Lijuakali, wa Kilombero, aliyedaiwa kukamatwa kwa kile kilichoelezwa ni
kuingia kwenye mkutano wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Kilombero uliofanyika jana, ambapo yeye alisema ni mjumbe huku
wasimamizi wakisema siyo mjumbe.
MBOWE
Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chadema, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa wabunge
na madiwani wa kutoka vyama vinavyounda Ukawa, wanadhalilishwa na
kunyanyaswa kila kona nchini na kwamba hizo ni juhudi za kurudisha nyuma
kazi kwa viongozi hao.
Mbowe alisema baadhi ya wabunge kutoka kwenye vyama vinavyounda
Ukawa, wamepokea barua kutoka kwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas
Kashilillah, ili kuonana na Kamati ya Haki, Madaraka na Kinga ya Bunge.
Alisema kosa linalowakabili ni kubishana na Mwenyekiti wa Bunge,
Andrew Chenge, kuhusu usitishwaji wa matangazo TBC kwenye mijadala ya
Bunge.
Akizungumzia kamatakamata ya wabunge wao, alisema licha ya Mdee
kukamatwa tangu juzi na kulala rumande, polisi walifika nyumbani kwa
Mbunge huyo wa Kawe na kupekua nyumba yake, hatua ambayo ameitaja ni
udhalilishaji.
“Kumekuwa na mizengwe tangu awali katika maeneo hayo, lakini Umeya
wa Jiji, CCM inafahamu kuwa kuna ufisadi mkubwa kuanzia, nyumba za jiji,
viwanja, usafiri wa Kampuni ya Usafishaji Dar es Salaam (Uda) pamoja na
kandarasi nyingi za kutoa huduma za kijamii ikiwamo maji na
nyinginezo,” alisema Mbowe.
Alisema mbali na Mdee, Mbunge wa Ukonga, Waitara na baadhi ya
madiwani wao wanatafutwa na polisi na wengine wameshikiliwa na jeshi
hilo.
Alisema mbali na kuwashikilia wabunge hao, kuna njama za kuwawekea dawa za kulevya ili wabambikiziwe kesi nyingine.
Mbowe aliwabebesha lawama viongozi wakuu wa nchi kuhusika na mambo hayo.
“Hana mamlaka ya kuvunja sheria kwamba wananchi wasipige kura na
ameonyesha udhaifu Dar es Salaaam, Kyerwa, Kilombero na maeneo yote
yaliyo na Ukawa wengi,” alisema.
Alisema watumishi ambao wanasababisha uchaguzi wa meya kukwama
akiwamo, Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando,
achukuliwe hatua na si kuwakamata viongozi wa Ukawa, kwani RAS alizuia
uchaguzi kufanyika, huku ikifahamika kuwa zuio lililotumika ni batili.
Aidha, alisema kuna mkakati wa kuvunja baraza la madiwani ili
kuunda Tume kwa lengo la kuvunja nguvu ya Ukawa kupitia baraza hilo.
Mbowe aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kabla ya kufanyika
kwa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, ili kujadili ajenda mbalimbali
ikiwamo suala la kukamatwa kwa wabunge na madiwani, uchaguzi wa umeya wa
jiji la Dar es Salaam na wenyeviti katika halmashauri ikiwamo Kyerwa
Mkoa wa Kagera na Kilombero mkoani Morogoro.
KUBENEA
Kubenea alipotafutwa na gazeti hili, alisema japo hajapata wito
rasmi kutoka kwa jeshi hilo, lakini amesikia kwamba anatafutwa na kwamba
yuko tayari kwenda endapo atapata barua rasmi ya wito huo.
“Ninaomba wananchi wanielewe, mimi siogopi polisi, nimesikia bado
wananitafuta, nataka aniite `officially’ nitakwenda. Nafahamu kwamba
kuna njama ambazo wamepanga kwa ajili ya kunibambikia kesi kwa sababu
wameshajua kwamba ninafahamu mambo mengi ambayo wanajua nikienda bungeni
nitawalipua,” alisema na kuongeza:
“Niko tayari kwa lolote, siogopi, nitahakikisha ninaendelea
kutetea ukweli na haki za wanyonge, hata kama watanibambikia kesi, mimi
naamini Mungu yupo upande wangu atanitetea, kama kosa langu ni
kusimamia ukweli wasifikiri kwamba wanaweza kuniziba mdomo kwa
kunikandamiza. Kwa nini wanaacha kuhangaika na watu wanaodanganya badala
yake wanahangaikana sisi ambao hatuna hatia.”
KAULI YA BUNGE
Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema ni kweli
kwamba baadhi ya wabunge wa waliotolewa kwa nguvu Bungeni wakati
kutokana na kupinga Televisheni ya Taifa (TBC), kutorusha moja kwa moja
mijadala ya Bunge wametakiwa kufika Dar es Salaa ili wakahojiwe na
Kamati ya Maadili ya Bunge.
Alisema kamati hiyo inatarajia kukaa Machi 7 hadi 11, mwaka kuhoji
wabunge hao ambao alisema idadi yake haijui kwa sababu bado
hajawasiliana na itakuwa na kazi ya kuwahoji wabunge hao ambao
walitolewa kwa amri ya Mwenyekiti wa Bunge, Chenge.
“Ni kweli wabunge wa upinzani wameandikiwa barua ya wito wa kwenda
kuhojiwa, lakini sifahamu idadi kamili ya wabunge hao kwa sababu
sijawasiliana na Mwenyekiti wa kamati hiyo,” alisema.
Alisema sababu ya wabunge hao kuhojiwa ni kutokana na kutolewa nje kwa amri ya Mwenyekiti wa Bunge na siyo kutoka kwa hiari yao.
“Kuna mambo mawili mnayochanganya. Kuna wale waliotoka wenyewe kwa
hiari yao, hawawezi kuhojiwa, lakini kwa wale wanaotolewa na Spika wa
Bunge, Sheria za Kanuni za Bunge zinaeleza kuwa watatakiwa kuhojiwa na
Kamati ya Maadili,” alisema Joel.
Alisema kanuni ya 71 kifungu cha 1 na 2 kinaeleza kuhusu Kamati ya Maadili kuwaita na kuwahoji wabunge waliotolewa nje na Spika.
“Maana Spika anapowatoa nje wabunge ili kutuliza vurugu, ina maana
anarejesha Bunge na kutoa taarifa ya kupeleka jambo hilo Kamati ya
Maadili,” alifafanua.
KAMATA KAMATA MOROGORO
Mkoani Morogoro, Mbunge wa Kilombero (Chadema), Lijualikali,
anashikiliwa na Polisi kwa kile kilichoelezwa ni kutokana na kukaidi
agizo la kutoingia katika uchaguzi huo la Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kilombero.
Mbali ya mbunge huyo, pia dereva wake, Steven Mdata na dereva wa
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Devota Minja (Chadema),
aliyetambuliwa kwa jina moja la John, alikamatawa.
Katika sakata la Mbunge Lijualikali ambaye alifika eneo la tukio
saa 3:30 asubuhi na kuzuiwa na askari waliokuwa wakilinda na kumueleza
kuwa haruhusiwi kuingia ukumbini kwa kuwa hawana taarifa zake, huku
mbunge huyo akidai yeye ni Mbunge na ana kibali cha kuhudhuria mkutano
huo kwa mujibu wa sheria.
Majibizano ya Mbunge na askari hao yalidumu kwa nusu saa na
hayakuzaa matunda licha ya kutaka kwenda kupata ufafanuzi wa kuzuiliwa
kwake kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi huo, lakini askari hao
waliendelea na msimamo huo.
Kufuatia hali hiyo, Mbunge huyo aliamua kuingia kwenye gari lake na
kuendesha mwenyewe na kuingia na kukata uzio uliowekwa na polisi hadi
katika eneo la ukumbi kwa kasi na kushuka kutaka kuingia ukumbini.
Kabla ya kuingia, ndipo askari zaidi ya 10 walipomkamata kwa nguvu
na kumuingiza katika gari la polisi kumpeleka katika Kituo Kikuu cha
Polisi Kilombero pamoja na dereva wake, Mdata na dereva wa Mbunge wa
Viti Maalum, John.
Habari hii imeandaliwa na Christina Mwakangale, Mary Geofrey Dar na Ashton Balaigwa, Morogoro.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment