Monday, 24 August 2015

Vipengele 25 vya MAGUFULI, Kadi feki za wapigakura, Maneno ya MKAPA, SUMAYE na wasomi je?..#StoriKUBWA {CONTENT ZOTE NA MILLARDAYO}

LAYIII

CLIK
HABARILEO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeweka historia na kujenga heshima ya taifa kwa kuweza kuandikisha wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Mfumo wa BVR kwa mafanikio makubwa na kuyashangaza mataifa makubwa duniani.

Katika kufanikisha hilo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF) vimetajwa kuwashawishi wanachama na wafuasi wake kwa kiwango kikubwa kujiandikisha katika BVR.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kufuatilia Masuala ya Uchaguzi Tanzania (TEMCO), ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Kufuatilia Masuala ya Uchaguzi, Dk Benson Banna, alisema Dar es Salaam jana kuwa Nec inastahili pongezi kubwa kwa hatua hiyo.
Alisema utafiti uliofanywa na Temco kwa kupitia vituo 8,398 vya uandikishaji ambavyo ni asilimia 80.5 ya vituo vyote, umedhihirisha kuwa kazi hiyo ilifanyika kwa ukamilifu kwa wananchi wengi kupata nafasi ya kujiandikisha huku asilimia 64 ya vituo vikizidisha hadi muda wa kufunga katika kuwawezesha wananchi kujiandikisha.
Kwa hatua hiyo, Dk Banna alisema NEC imefuta aibu kwa Taifa, kutokana na mataifa mbalimbali ya nje kubeza uwezo wa nchi katika kufanikisha uandikishaji huo kabla ya kuanza na kwamba sasa kama Taifa, Tanzania imeanza kuonesha uwezo mkubwa wa kujitegemea katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi.
“Hili lazima nilisema wazi, ni aibu kwa mataifa makubwa kufadhili shughuli za uchaguzi maana kitendo hicho ni hatari kwa nchi kuweza kujiamulia mambo yake na kukuza demokrasia ya kweli, hivyo Nec wanastahili pongezi,”  Dk Banna.
Akielezea mlolongo mzima wa uandikishaji, mwanazuoni huyo alisema, Temco katika ufuatiliaji wake huo ilibaini kasoro mbalimbali ikiwemo fedha kutolewa kidogo na kwa kuchelewa hatua iliyofanya tarehe ya kuanza kwa uandikishaji kuchelewa na kusababisha usumbufu kwa wananchi.
Alisema pia wakati tathimini ya awali ilikuwa ni kuhitajika kwa visanduku vya BVR zaidi ya 15, 000, serikali ilikataa pendekezo hilo na kusema visanduku vinavyohitajika ni 14,000, lakini hata hivyo havikuweza kununuliwa badala yake vilinunuliwa visanduku 8,000 tofauti na ushauri wa Nec ambayo ilishauli kiwango cha chini kiwe visanduku 10,000.
HABARILEO
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kinatarajiwa kufanya hafla ya aina yake ya kumuenzi Rais Jakaya Kikwete.
Kitamuenzi kama sehemu ya kutambua mchango wake wa hali na mali, uliofanikisha kuanzishwa kwa chuo kikuu hicho cha aina yake Tanzania na nje ya Tanzania.
Taarifa ya kusudio la chuo hicho kumuenzi Rais Kikwete, limetolewa mwishoni mwa wiki na Makamu Mkuu wa UDOM, Prof. Idris Kikula wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi na Maofisa wa Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Profesa Kikula na ujumbe wake yuko katika ziara ya kikazi nchini Marekani. Ziara hiyo ilimfikisha jijini New York, ambapo ujumbe ulipata fursa ya kukagua vifaa tiba na vitabu vya kiada na ziada, ambavyo vimetolewa na wadau mbalimbali wenye mapenzi mema na Tanzania.
Baada ya kukagua vifaa na vitabu hivyo na kujiridhisha, Makamu Mkuu wa UDOM ameushukuru Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwa kuwapatia fursa hiyo ya kujionea wenyewe aina ya vifaatiba na vitabu, ambayo amesema vitakuwa msaada mkubwa kwa Kitivo cha Sayansi ya Afya cha Chuo hicho.
“Waheshimiwa Mabalozi, mimi na ujumbe wangu napenda kwa moyo wa dhati kabisa kutoa shukrani zetu kwa kutuonesha vifaa na vitabu ambavyo kupitia kwenu wafadhili wamevitoa kuwasaidia watanzania nanyi mkaona bora kutushirikisha na kuona namna gani chuo chetu kinaweza kunufaika na misaada ya aina hii,” Profesa Kikula.
Aliongeza kuwa Kitivo cha Sayansi ya Afya na ambacho pia kina zahanati, kinahitaji sana misaada ya kila aina ili kiweze kutimiza lengo lake kuu la kuwaandaa madaktari na wataalamu mbalimbali, lakini pia kutoa huduma uchunguzi na matibabu siyo tu kwa wanafunzi na wafanyakazi wa UDOM bali pia kwa Watanzania wote.
“Uongozi wangu unapenda kutambua juhudi zenu hizi za kushirikiana na wadau mbalimbali kusaidia siyo tu vyuo vikuu vyetu, lakini na watanzania. Mmedhihirisha kwa vitendo na si maneno na hii imetupa faraja sana na kudhihirisha namna gani tunaweza kushirikiana kwa karibu zaidi.”
Alisema kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma ni ndoto na hatimaye mbegu iliyopandwa na Rais Kikwete, ndoto uliyoanzia kwenye kampeni yake ya urais mwaka 2005.
“Ilianza kama ahadi ya kampeni, ahadi ambayo haikuishia katika maneno matupu ya ahadi bali aliitekeleza ahadi ile na leo hii tunaiona mbegu aliyoipanda ikichanua na mavuno yanaonekana,” alisema Prof. Kikula kwa msisitizo wa aina yake.
Anasema haikuwa rahisi kuifanikisha ndoto ya Rais kutokana na pingamizi mbalimbali kutoka nje na ndani ya serikali.
Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ameushukuru uongozi wa UDOM kwa kuitikia mwito wa Uwakilishi wa kutumia ziara yao ya kikazi, kujionea kukagua vifaa na vitabu ambavyo vimepatikana kwa ushirikiano wa uwakilishi na wadau mbalimbali.
HABARILEO
Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema Tanzania ya sasa inahitaji kiongozi mwadilifu, mzalendo na mchapakakazi kama alivyo mgombea wa CCM, Dk John Magufuli.
Jaji Warioba akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM jana Dar es Salaam, alisema Dk Magufuli ni mchapakazi kweli kweli na hana masihara anapokuwa ofisini au nje ya ofisi.
“Wote mmemshuhudia akiwa Waziri wa Maendeleo ya Uvuvi, Ardhi na sasa hivi Ujenzi, amekuwa mchapakazi na amekuwa anawaelemisha wananchi wazifahamu haki zao,”Jaji Warioba.
Dk Warioba alisema wakati alipokuwa mwenyekiti wa Tume ya Rushwa wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, alibaini kuwa sekta ya ujenzi ilikuwa inaongoza kwa rushwa, lakini tangu Dk Magufuli apewe wizara hiyo hakuna ufisadi tena.
Alisema kama Dk Magufuli angeamua kuchukua hata asilimia moja tu ya ujenzi wa Daraja la Mkapa, Daraja la Malagarasi au Daraja la Kigamboni angekuwa tajiri wa kutupa, lakini hakuwahi kujihusisha na vitendo hivyo vya kifisadi na ndio maana hana utajiri wowote.
“Tumesikia ufisadi wa EPA, Richmond, Escrow lakini hatujasikia ufisadi kwenye ujenzi na hii inadhihirisha kuwa Dk Magufuli ni mwadilifu,”Jaji Warioba.
Jaji Warioba alisema mgombea huyo wa CCM ni mkali na hapendi kazi za ovyo ovyo, lakini pia anafuatilia kwa karibu.
Alisema chanzo cha ufisadi ni kutokana na viongozi kuwa karibu na matajiri, jambo ambalo mgombea huyo hana tabia hiyo.
Alisema mgombea huyo hana makundi badala yake kundi lake ni Watanzania wote hivyo akatoa mwito kwa Watanzania kumpa kura ili aweze kuwaongoza Watanzania na kuwaletea maendeleo ya kweli.
NIPASHE
Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC), linaendelea kuitafakari Serikali ya Tanzania kuhusu kuingizwa katika mkataba wa pili wa miradi ya shirika hilo.
Msemaji wa Ubalozi wa Marekani nchini, Marissa Maurer, aliliambia Nipashe kuwa hivi sasa mchakato wa maandalizi ya mkataba wa pili wa MCC na Tanzania unaendelea.
Hata hivyo, alisema mkataba huo hautawasilishwa mbele ya Bodi ya MCC ili kuidhinishwa hadi maandalizi yake yatakapokamilika.
Alisema mkataba huo pia hautaweza kuidhinishwa hadi pale Tanzania itakapoonyesha hatua ilizopiga  katika mageuzi ya uchumi katika sekta ya nishati kama ilivyoahidi kufanya hivyo hadi mwishoni mwa mwaka jana.
Desemba mwaka jana, ubalozi huo ulitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya MCC ilikutana Desemba 10, mwaka huo katika mkutano wake wa kila mwaka wa kuchagua nchi zitazopatiwa fedha na shirika hilo.
Katika mkutano huo, bodi hiyo ilipiga kura ya kuiruhusu Tanzania iendelee na maandalizi kwa ajili ya mkataba wa pili wa miradi ya MCC.
Aidha, bodi hiyo iliihimiza Serikali ya Tanzania kuchukua hatua thabiti za kukabiliana na rushwa kama sharti la msingi kwa MCC kufanya maamuzi ya mwisho ya kuidhinisha mkataba huo.
Kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kilikuwa kikwazo kingine kwa shirika hilo kuiingiza Tanzania katika mkataba huo hadi litakaporidhishwa na hatua ambazo zingechukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa kashfa hiyo.
Nchi ambazo zimekuwa zikiingizwa katika mikataba ya miradi ya shirika hilo, zimekuwa zikipewa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
NIPASHE
Katibu Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, wakati wasanii mbalimbali wakitumbuiza katika uzinduzi huo, alikuwa aliwapiga vijembe vyama vinavyounda na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwamba vimebeba makapi akidai kuwa wanadhani watangia Ikulu.
Nape alikuwa akimaanisha makapi ni waliokuwa makada wa CCM ambao wamekihama chama hicho kwa nyakati tofauti na kujiunga upinzani vya Chadema, na NCCR- Mageuzi na CUF.
Miongoni mwa makada hao walitimkia Ukawa ni waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa (Chadema) na Frederick Sumaye (NCCR-Mageuzi).
Baada ya Lowassa kujiunga na Chadema, aliteuliwa kuwania urais akiwalisha Ukawa wakati Sumaye juzi baada ya kuhama CCM alisema amekwenda kuimarisha upinzani.
Naye Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Makongoro Nyerere, aliponda  makada wa CCM waliohamia upinzani wakiwamo Mawaziri Wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Akizungumza katika mkutano huo, Makongoro ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara tangu mwaka 2007 hadi 2012, alidai kuwa Sumaye siyo mkweli kwani  alipokuwa CCM alinukuliwa akisema iwapo chama  hicho kitamteua Lowassa kugombea urais kwa  angekihama.
“Wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea urais Sumaye alisema hiki chama mkimpa Lowassa, atahama chama kwa kuwa tunamweshimu Sumaye hatukumpitisha Lowassa, lakini bado amehama na kwenda kumkumbatia fisadi,” alisema.
Alisema pale ambako mtu hazumgumzi ukweli anaitwa mwongo, hivyo kauli yake hiyo Sumaye hana tofauti na mwongo kwani katika kipindi cha miaka kumi iliyopita aliingia katika kinyang’anyiro cha urais na alifika tano bora, lakini kura hazikutosha badala yake zikatosha za Kikwete.
Alisema miaka kumi baadaye Sumaye ameingia katika kinyang’anyilo cha urais bahati mbaya hakuingia katika tano bora, lakini cha kushangaza anaanza kuishukutumu CCM kwamba ni chama kibaya wakati alipoingia tano bora alikisifia.
“Mnaufahamu mchezo wa chandimu, ambao huchezwa na vijana tu na mzee akiingia akija anataka nini?alihoji na kuongeza;
“Sumaye kaingia katika mchezo huu wa chandimu mwenyewe, tutamsema.”
Mbali na Sumaye na Lowassa, wapinzani wengine waliohama CCM na kuiunga na upinzani ni wagunge waliomaliza muda wao wa Kahama, James Lembeli; Viti Maalum, Ester Bulaya; Arumeru Magharibi, Ole Medeye; Segerea, Dk. Makongoro Mahanga na wa Sikonge, Said Mkumba.
Wengine ni wenyeviti wa CCM wa mikoa ya Arusha, Onesmo Ole Nangole; Singida, Mgana Msindai na Shinyanga, Khamis Mgeja pamoja Mwenyekiti wa zamani wa Dar es Salaam, John Guninita.
NIPASHE
Watu wa makundi kadhaa wametoa kauli tofauti kuhusiana na hatua ya Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na upinzani.
Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO), Danford Kitwana, alisema kuhama kwa viongozi waandamizi wa serikali na makada maarufu wa chama tawala, ni ishara ya mwelekeo mbaya kwa chama hicho kwani hadi Oktoba idadi kubwa wanahamia inaweza kuongezeka.
“Ni ishara ya mwelekeo mbaya kwa CCM, maana ndiyo kufunuliwa kwa siri za ndani za CCM ambazo upinzani wanazihitaji…..kunaongeza uwiano mzuri baina ya upinzani na CCM,” alisema.
Mkazi wa Dar es Salaam, Joseph Masaga, alisema hiyo ni ishara kwa chama tawala kuwa katika hatari ya kupoteza nguvu kutokana na malalamiko ya wananchi dhidi ya mfumo wa kupata viongozi wake.
Aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi ya Tiba cha KCMC, Prof. Watoki Nkya, alisema hatua ya Sumaye inaashiria kwamba umri wa kuishi wa CCM hicho umefikia ukingoni, kutokana na kukua kwa demokrasia nchini.
Mhadhiri Msaidizi wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Emanuel Damalo, alisema uamuzi huo unaweza kuwa ni ishara mbaya ya kuanguka kwa CCM, baada ya kukaa madarakani kwa zaidi ya miaka 50.
Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (RUCo), Rwezaura Kaijage, alisema: ”Mimi nawashauri CCM badala ya kuwakejeli na kuwasimanga wanaohama, wangekaa chini wakatafakari nini kinatokea, huu upepo siyo mzuri kwa watawala.
Alisema  haua ya kuhama kwa Sumaye na Lowassa (Edward) si ya kabeza, lazima ujiulize kuna nini ndani ya CCM.
Mwanasheria wa mjini Morogoro, Deo Niragira, alisema ni uamuzi wa busara kutokana na kutotendewa haki alipokata rufaa baada ya kupewa adhabu ya kifungo cha miezi 12 kwa madai ya kuanza kampeni za kuteuliwa kuwania urais kabla ya muda wake.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk. Joel Mmasa, alisema Sumaye ni mmoja wa viongozi wachapakazi ambaye alimsaidia kwa karibu Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ambaye mpaka sasa amebaki na kuwa na sifa kukuza uchumi, hivyo hatua yake inaweza kuiathiri CCM uchaguzi wa Oktoba.
Mwenyekiti wa Chama cha Biashara (TCCIA), Mkoa wa Mbeya, Dk. Luitico Mwakalukwa, alisema alichokifanya Sumaye ni jambo zuri kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha upinzani.
Mwenyekiti wa Mtandao wa wasomi Mkoa wa Mbeya, Prince Mwaihojo, alisema baada ya kukaa kwa muda mrefu ndani ya CCM tangu alipostaafu, Sumaye  ameona hasikiki na sasa anatafuta mahali ambako anaweza kusikika.
“CCM hawapaswi kupuuza suala hili kama kweli ni chama kinachojitambua na walipaswa kulifanyia kazi tangu alipoondoka Lowassa, lakini kuishia kupiga vijembe tu huku wanachama wakizidi kuwakimbia haisaidiii, bali wanajimaliza kisiasa,” alisema Sembuyagi Omary, Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria (OUT), jijini Tanga.
Dk. Lupa Ramadhani  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema ni jambo la kushtua katika siasa za nchi hii na linaonekana la kushangaza pale viongozi wakuu ambao waliwahi kushika nyadhifa kubwa ndani ya serikali kukihama chama tawala.
MTANZANIA
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeibua tuhuma mpya dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kikisema kimebaini shahada zaidi ya milioni mbili za kupigia kura zinazotarajiwa kuingizwa kinyemela katika Daftari la Wapiga Kura na  kugawiwa kwa wana CCM ambao hawakujiandikisha.
Chama hicho kimedai kwamba, mbali na shahada hizo pia wakimbizi zaidi ya 70,000 mkoani Kigoma wameandikishwa katika daftari hilo kwa ajili ya kupiga kura.
Tuhuma  hizo zilitolewa jijini Dar es Salaam jana mbela ya waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chadema (BAWACHA), Halima Mdee na kada wa chama hicho, Saed Kubenea.
Akizungumza katika mkutano huo, Kubenea aliwaonyesha takribani shahada 100 alizosema ndizo zitakazoingizwa kwenye dafatari hilo kinyume cha taratibu.
Shahada hizo hazina jina la mpiga kura, picha, tarehe ya kuzaliwa, sehemu na eneo alilojiandikisha pamoja na taarifa nyingine muhumu zinazowekwa kwenye shahada halali.
“Chadema tumebaini kuwepo kwa mpango wa kuingizwa kwa shahada za kupigia kura zaidi ya milioni mbili, ambazo zinatarajiwa kutumiwa na wana CCM ambao walikuwa hawakujiandikisha katika daftari la kupigia kura,” Kubenea.
“Inawezekana kabisa NEC kwa kushirikiana na CCM wamepanga kuingiza majina yao katika shahada hizi, na ndiyo maana hata kuna baadhi ya watu walikamatwa wakiwa na mashine nyumbani kwa watu,” alisema.
Kubenea alisema vitambulisho hivyo vimetengenezwa ili kuongeza kura za CCM kwa wanachama wake ambao hawakupata nafasi ya kujiandikisha.
“Nchi yenye idadi hiyo ya watu haiwezi kuwa  na wapiga kura milioni 23, kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Takwimu ya Taifa wanasema asilimia 60 ya Watanzania wako chini ya miaka 18, hivyo ukichukua nusu ya Watanzania milioni 45 itakuwa ni milioni 22.5 kama wote wangeingia kwenye sensa hivyo kwa tathmini hiyo nyongeza hiyo ni wizi,” alisema.
Kubenea alitoa wito kwa NEC kufanyakazi kwa uaminifu na uadilifu ili kuondokana na mipango ya kuongezwa kwa kura za watu ambao hawakujiandikisha katika daftari la wapiga kura.
Kwa upande wake Halima Mdee alisema kuwa chama hicho kimepata taarifa kutoka kwa wafanyakazi wa Tume wakisema kuwa kuna wakimbizi 70,000 walioandikishwa kutoka mkoani Kigoma.
“Kuna wafanyakazi wa tume ambao ni wasamaria wema wametupatia taarifa za ndani zinazosema kuwa katika kuhakikisha ushindi unapatikana wamewaandikishwa wakimbizi 70,000 kutoka mikoa ya kigoma,” alisema.
Mdee alisema kuwa ujanja wa kutafuta kura za kupata bao la mkono imekuwa sababu ya NEC, kuchelewa kufanya uhakiki wa daftari la kupigia kura kwa mkoa wa Dar es Salaam.
MTANZANIA
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alipopata wasaa wa kuhutubia maelfu ya wanachama wa CCM waliokuwa uwanjani hapo, alirusha kijembe kwa wapinzani na kusema wanaosema wanatafuta ukombozi ni wapumbavu na malofa.
“Kuna vyama vinajifanya vinataka kuleta ukombozi, ukombozi uliletwa na ASP na Tanu, hao wanaojiita vyama vya ukombozi ni wapumbavu, … ni malofa, nchi hii ilikwisha kombolewa na sasa inaendelea kuiomboa kwa kupambana ana umasikini, ujinga na maradhi na ndo kazi imekuwa ikifanywa na serikali zote zilizopita kuanzia ile ya awamu ya kwanza na hii inayokuja itafanywa na serikali ya Dk. Magufuli,” alisema.
Alisema kati ya wagombea urais wanane waliopitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), hakuna mwingine mwenye sifa nzuri kama Dk. Magufuli.
Katika hatua nyingine, alisema haitoshi kuchukia umaskini bali inatakiwa mtu aeleze ni namna gani ataweza kupambana na tatizo hilo.
“Eleza ni kwa namna gani utapambana na umasikini, ilani ya CCM inaonyesha namna ya kutekeleza kama alivyofanya Dk. Kikwete,”Mkapa.
Aliwataka wanachama wa CCM kuwashawishi Watanzania kuipigia kura CCM ili kuendeleza ukombozi wa maendeleo ya Tanzania na ushindi ni lazima kwa CCM.
Kwa upande wake Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, naye aliwarushia vijembe wapinzani kwa kusema kuwa ni CCM B na kwamba hakuna sababu ya kuwachagua kwa sababu CCM A ipo.
“Wanaohama wenyewe wamesema kwa nini wanaenda huko, siyo mimi ninasema, wanasema wanaenda kuwafundisha namna ya kuioandoa CCM, kwa hiyo dhamira inayowapeleka huko ni kutafuta namna ya kuishinda CCM hali iliyosababisha kutengeneza CCM mbili ambazo ni A ya kwetu na B ni ile ya upinzani mliyoisikia wenyewe, kama A ipo B ya kazi gani?, Mwinyi.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba, alisema sababu za ufisadi ni viongozi kuwa karibu na matajiri.
“Miaka 20 iliyopita Mkapa alinipakazi ya kuangalia ufisadi, katika taarifa ile tulisema chanzo cha ufisadi ni viongozi kuwa jirani na matajiri, ‘mmewahi kumwona Magufuli yupo karibu na matajiri?  “hapanaa”, wananchi walijibu.
Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema Magufuli ni mzalendo hasa kwa nchi yake akiwa pamoja na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan.
Alisema pia kwamba, Dk. Magufuli amechaguliwa na chama chake kumetokana na mgombea huyo kuwa na sifa za uadilifu, uchapakazi na uzalendo.
Kwa upande wa Rais wa Zanzibar, Dk. Mohammed Shein, alisema Wazanzibari wapo pamoja na Dk. Magufuli kama ambavyo waliwaunga marais wengine waliopita.
Hata hivyo Dk. Sheni alisema ushindi wa CCM uko wazi huku akijigamba kuwa vyama vya upinzani haviwezi kufurukuta kwa upande wa Zanzibar.
MTANZANIA
Mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia  Chama cha Wananchi (CUF)  chini ya mwamvuli wa Ukawa, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema wamejipanga kushinda uchaguzi wa mwaka huu na CCM hakitakuwa na sehemu ya kutokea.
Maalim Seif aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar ikiwa ni mara yake ya tano tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi.
Akiwa amesindikizwa na mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMa), chini ya mwamvuli huo Edward Lowassa, Maalim Seif alisema safari hii wamejipanga vya kutosha.
“Safari hii tumejipanga CCM hawana pakutokea na ikiwa uchaguzi wa huru na wa haki akishinda yoyote nitakuwa wa kwanza kumpongeza na kutambuwa ushindi wake,” alisema.
Alisema Ukawa ni imara na yeye kama mgombea yupo tayari kupambana na mgombea yoyote kati ya waliojitokeza kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar akiwemo Hamad Rashid Mohamed ambaye ni mmoja wa waasisi wa CUF anayewania urais wa visiwa hivyo kwa tiketi ya ADC.
Alisema CUF inashangazwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kushindwa kufanya mabadiliko makubwa kwa watendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kama alivyokuwa ameahidi baada ya matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Zanzibar mwaka 2010.
“Nimeandika barua mara tatu kukumbusha ahadi yake hakuna chochote kilichofanyika, Secreteriet ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ipo vile vile watendaji walioharibu chaguzi zote ndio wale wale waliokuwepo sasa”, alisema Maalim Seif akiwa ameshika mikono kichwani.
Alisema  anaamini ni vigumu kwa Dk. Shein kutekeleza ahadi yake kwa sababu inamnufaisha yeye na chama chake ndo maana hadi sasa hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika kwa watendaji wa tume hiyo.
Alisema kwamba iwapo wananchi wa Zanzibar watampa ridhaa ya kuingia Ikulu vipaombele vyake vikubwa ni kupambana na umasikini, kuweka msingi wa elimu bora, kufunguwa milango ya Uwekezaji na kutumia rasilimali za nchi kuwanufaisha wananchi kwa kuimarisha uchumi kupitia sekta ya mbali mbali ikiwemo uvuvi wa bahari kuu, anga, pamoja na nishati.
Kuhusu vigogo wa CCM wanaoendelea kujiunga na timu ya UKAWA alisema Chama Cha Mapinduzi kimepoteza mwelekeo na sio kile chama cha CCM cha zamani kwa vile kimeshindwa hata kuheshimu taratibu, kanuni na katiba ya chama chake.
“Lowassa na Sumaye wameamua kukiacha chama hicho kwa sababu wamefika pahali wameshindwa na uvumilivu na mwisho wake na sio chama tunachokijuwa kimeshindwa kupata katiba na kanuni zake”, alisema Maalim Seif na kuongeza hata mwalimu Nyerere alisema CCM sio mama yake au baba yake na wananchi wakikosa mabadiliko ndani ya chama watatafuta njia.
Katika mapokezi hayo mgombea wa urais wa muungano Edward Lowassa amewafunika viongozi wenzake kila alipokuwa akionekana na kushangiliwa kwa kishindo.
Wagombea wengine waliochukuwa fomu katika kituo cha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni mgombea wa Chama cha DP Abdalla Kombo Khamis, ambae alisistiza umuhimu wa kuwa na uchaguzi huru na wa haki, pamoja na kuahidi wananchi kushuhudia mabadiliko makubwa ya kiutawala na kiuchumi iwapo wananchi watampa ridhaa ya kuingia Ikulu.
Kwa upande wake mgombea wa Jahazi Asilia Kassim Bakari Ali amesema kwamba Zanzibar inahitaji mabadiliko ndio maana amemuwa kuchukuwa fomu kugombea nafasi hiyo ili kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi na kujenga Zanzibar yenye uchumi imara.
MWANANCHI
Wasomi mbalimbali nchini wamesema kitendo cha Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kuhamia upinzani kutakiathiri Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu ya nguvu ya ushawishi aliyonayo katika jamii.
Juzi, Sumaye alitangaza kuihama CCM na kujiunga na upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa kile alichoeleza kuwa ni kutaka kuimarisha upinzani na kujenga chama mbadala ambacho wananchi wanaweza kukichagua.
Hatua hiyo ni mfululizo wa wanachama wa CCM kuhamia upinzani kwa madai ya kutoridhishwa na mchakato wa kuwapata wagombea katika nafasi mbalimbali za urais na ubunge.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala alisema hatua hiyo ya Sumaye hiyo ni ishara kuwa chama hicho kimepoteza mvuto kwa watu wake.
Alisema ilizoeleka kwamba wapinzani ndiyo waliokuwa wakikikosoa chama hicho tawala kutokana na mfumo wake mbovu wa kiutawala, lakini wanapohama vigogo wake, wanatia msisitizo kuhusu ubovu huo.
“Kuhama kwa Sumaye kunashawishi pia wananchi kwa sababu alikuwa kwenye mfumo wa utawala. Pia, kutaathiri upigaji kura dhidi ya CCM. Kwa hiyo, hilo siyo jambo dogo kwa CCM,” alisema.
Profesa Mpangala alisema katika siasa, kuna wakati kinakuja kimbunga cha watu kutaka mabadiliko. Alisema hiki ni kimbunga cha mabadiliko ambacho kitaufanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa na ushindani mkubwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema Sumaye alikwa na nafasi kubwa serikalini na ndani ya chama, hivyo lazima athari ziwepo kwa sababu kimepoteza mtu muhimu ambaye angesaidia kumnadi mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli.
Alisema Sumaye anajua mambo mengi ya chama chake na siri zilizokifanya kiendelee kutawala na kwamba atatumia ujuzi huo kuusaidia upinzani kushinda kwenye uchaguzi wa Oktoba 25.
“Uchaguzi huu utakuwa na ushindani mkubwa kwa sababu wananchi wameamka na upinzani umeimarika. Hakuna upande wa kumbeza mwenzake, hapa ni kufanya siasa kwa umakini mkubwa,”  Salim.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema Sumaye hakuwa na nafasi yoyote ndani ya chama tangu alipoondoka madarakani mwaka 2005, hivyo hakuna athari zozote kwa CCM.
Dk Bana alisema Sumaye hakupata washauri wazuri na wapo mawaziri wakuu wastaafu waliokuwapo kabla yake lakini wamekuwa wakikikosoa chama kupitia vikao vya ndani.
MWANANCHI
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amefungua pazia la kampeni za chama hicho kwenye Viwanja vya Jangwani katika tukio lililohudhuriwa na maelfu ya wananchi, huku akieleza mambo 25 atakayoyafanya iwapo Watanzania watamchagua kuwa Rais wa Awamu ya Tano.
Huku akitumia maneno: “Mimi kazi tu”, “Tanzania ya Magufuli ni ya viwanda”, Dk Magufuli aliyetumia dakika 53 kueleza sera zake, kuanzia saa 11.40 hadi 12.33 jioni alisema Watanzania wanataka kitabu kipya cha mabadiliko na yeye na mgombea mwenza, Samia Suluhu ndiyo wanaoweza kuyaletea.
Mgombea huyo wa urais wa CCM aliahidi kuanzisha mahakama maalumu ya kusikiliza kesi za rushwa na ufisadi, kumaliza tatizo la wanafunzi wa elimu ya juu kukosa mikopo, kuhakikisha mama lishe hawabughudhiwi, kusimamia haki za wasanii, kulinda Muungano na usalama wa nchi.
Aliahidi kutoingilia utendaji kazi wa Bunge na Mahakama, kuheshimu mawazo ya vyama vingine vya siasa, kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama, wafanyabiashara wadogo na wakubwa wote kulipa kodi, kuendeleza kilimo, mifugo, uchimbaji wa madini, majisafi na elimu bora.
Nyingine ni kusimamia nishati ya gesi, ujenzi wa barabara, reli, kuboresha sekta ya utalii, kuimarisha uwekezaji, kuwasaidia walemavu na kusimamia uhuru wa habari.
Mkutano huo ulioanza rasmi saa 9.30 alasiri ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na CCM, wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa. Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba na Salim Ahmed Salim.
Mgombea huyo alitoa ahadi mbalimbali ikiwamo ajira akisema: “Ninataka Watanzania wapate ajira, kazi ya Serikali itakuwa kukusanya kodi tu. Viwanda vinaweza kutengeneza ajira kwa asilimia 40 hasa kwa vijana wanaohitimu vyuo mbalimbali nchini.”
Kuhusu ubinafsishaji, alisisitiza: “Kuna viwanda vilibinafsishwa sasa wahusika wasipoviendeleza wajiandae kuvirudisha haraka.”
Mbali na kurejesha viwanda vilivyobinafsishwa, alisema akipewa ridhaa hiyo atahakikisha chini ya uongozi wake, anajenga viwanda vingi vipya, akiainisha vile mahsusi kwa shughuli za kilimo, mifugo, kusindika nyama na madini.
Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni kilimo na kwamba atahakikisha sekta hiyo ambayo ndiyo mhimili wa uchumi inaendelezwa.
“Tutaleta vitendea kazi, pembejeo na vifaa vingi vya kisasa na vya kutosha kwa wakulima… kama nilivyosema hapo awali, tutajenga viwanda kwa ajili ya wakulima pia.
Mbunge huyo wa zamani wa Chato alisema pia kipaumbele kingine katika Serikali yake ni kuhakikisha kuwa wananchi wa mjini wanapata majisafi na salama kwa asilimia 95 na wananchi wa vijijini wanapata maji kwa asilimia 85.
Kuhusu afya alisema: “Tutahakikisha tunakuwa na vituo vya afya, zahanati na hospitali katika maeneo mbalimbali kwa sababu tunaamini maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana kama wananchi hawana afya bora.”
Kipaumbele kingine ni mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu akisema watakuwa wanapata mikopo kwa wakati bila kuchelewa na kwamba watajikita pia katika kujenga hosteli kwa wanafunzi wa vyuo.
“Mishahara ya walimu na wafanyakazi wote tutaishughulikia. Hata madereva haki zao za msingi lazima ziangaliwe,” alisema huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Mgombea huyo alisema anafahamu kero ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam na kwamba maendeleo ya kweli yatapatikana kama changamoto hiyo itafanyiwa kazi.
Alisema akipewa ridhaa hiyo itashughulikia suala la reli  kwa kujenga reli ya kisasa kwa viwango vya Standard Gauge” na kuboresha bandari na usafiri wa anga.
Kuhusu maliasili, alisema ni kipaumbele katika Serikali yake endapo akipewa ridhaa ya kuongoza nchi huku akieleza kukerwa na ujangili… “Ninapata shida sana ninapoona meno ya tembo yanauzwa Ulaya halafu unaambiwa yanatoka Tanzania… sasa unajiuliza yanapitaje?”
Alisema ili kushughulikia suala hilo atahakikisha watendaji wa sekta hiyo wanaboreshewa masilahi yao ili wachangie mapato ya nchi.
Aliahidi Serikali yake kuwa rafiki wa wawekezaji na kwamba italinda masilahi ya wafanyabiashara.
Mgombea urais huyo aliahidi kuwa atalinda uhuru wa habari na atafanya kazi na waandishi wa habari siyo tu wakati wa kipindi cha kampeni, bali hata baada.
Katika ahadi zake, Dk Magufuli hakuwaacha wasanii, alisema atahakikisha wanapata hakimiliki na kuhakikisha wao pamoja na wanamichezo wanaanzishiwa mfuko kwa ajili ya kuwasaidia katika mambo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

advertise here