Tuesday 7 July 2015

KATIKA MAGAZETI YA LEO 7/7/2014

LAYIII

Polisi wazuia wageni Dodoma, Lowassa asukiwa zengwe na hukumu ya kina Yona, Mramba…#MAGAZETINI JULY7

GOOO 
MWANANCHI
Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM itakutana kesho mjini Dodoma kuanza shughuli yake ya kupitia taarifa za wagombea 38 wanaoomba kuwania urais na kisha kuwasilisha ushauri wake kwenye kikao cha Kamati Kuu inayokutana keshokutwa.
Habari kutoka ndani ya CCM zinasema kuwa kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete wakati mwingine hukasimisha shughuli zake kwa kamati ndogo inayoketi chini ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.

Mangula amekaririwa mara kadhaa akisema chama hicho kitatumia vigezo 13 vilivyowekwa na chama kuwachuja wagombea hao, akisisitiza kuwa watateua mgombea mwadilifu, mwenye uzoefu na atakayeuzika kwa wananchi.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walioko tayari mjini hapa kwa kazi hiyo walilieleza gazeti hili kuwa jukumu kubwa la kamati hiyo ni kuishauri Kamati Kuu juu ya masuala yote yanayohusu maadili ya wanachama na wagombea wa nafasi mbali ndani ya chama na kwenye vyombo vya Dola.
Mjumbe mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa kuwa si msemaji alieleza kuwa kama kuna jambo kubwa, kamati ndogo huwa haikutani, badala yake kamati kubwa ikiwa chini ya Rais ndiyo hukutana na kuandaa taarifa za kuwasilisha kwenye Kamati Kuu.
Alitolea mfano wa mambo makubwa kuwa ni kama vile kupitia majina ya wanaowania kuteuliwa kugombea urais, kwamba kazi ya kamati ni kueleza taarifa za kila mwombaji, mazuri yake, mabaya yake na ushauri inaoutoa kwa wajumbe wa Kamati Kuu.
Mjumbe huyo alisema, Kamati ya Maadili na Usalama haina mamlaka ya kukata au kuongeza majina ya wagombea na kwamba mambo yanayopelekwa kwenye Kamati Kuu ni yale mazito tu.
Kuhusu mambo ya madogo yanayoishia kwenye kamati ndogo, alisema ni yale yanayoonekana yana viashiria vya majungu.
Mangula hakupatikana jana kuzungumzia majukumu ya kamati hizo lakini Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alipoulizwa kwa simu alisema majukumu na mipaka ya Kamati ya Maadili na Usalama vimeelezwa ndani ya Katiba ya CCM.
MWANANCHI
Historia inaelekea kujirudia, kama ilivyokuwa wakati Rais Jakaya Kikwete akizindua Bunge la 10 na wabunge wa Chadema kususia hotuba yake, ndivyo itakavyokuwa atakapolihutubia Bunge kwa mara ya mwisho Alhamisi bila kuwapo wabunge hao na wenzao kutoka NCCR – Mageuzi na CUF wanaounda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB).
Wabunge wa Chadema wakati huo wakiunda KUB peke yao, walisusia hotuba ya Rais Kikwete Novemba 30, 2010 wakipinga matokeo ya uchaguzi uliomweka madarakani.
Safari hii wakati Rais Kikwete akitarajia kulihutubia Bunge hilo kwa mara ya mwisho kabla ya kulivunja rasmi kwa tangazo la Serikali (GN) litakalotolewa baadaye, hali inaelekea kuwa vilevile, lakini kutokana na sababu tofauti.
Kiongozi wa KUB, Freeman Mbowe alisema jana kwamba wabunge wanaounda kambi hiyo hawatahudhuria vikao vilivyosalia kwa sababu ya Serikali kupitisha miswada mitatu ya petroli na gesi kinyume cha kanuni na sheria.
“Miswada hii inahitaji umakini mkubwa kabla ya kuigeuza kuwa sheria,” alisema Mbowe na kufafanua kuwa utaratibu uliotumika utazaa sheria mbaya.
Alisema KUB na viongozi wote wa vyama vinavyounda Ukawa walikubaliana kuishauri Serikali, uongozi wa Bunge na wabunge wa CCM wasiwe na haraka katika kuipitisha miswada hiyo lakini hawakusikilizwa.
Mbowe alisema walikubaliana kuiacha miswada hiyo ipitishwe na Bunge la 11 litakaloanza Novemba ili kufanya uchambuzi wa kina kwa kuzingatia masilahi mapana ya Taifa.
Alisema licha ya semina mbalimbali kati ya wabunge wa pande mbili, kwa sababu wanazozijua wenyewe, Serikali na uongozi wa Bunge waliamua kuendelea kuvunja kanuni za Bunge kwa kupitisha miswada hiyo kwa utaratibu wa “voda fasta.”
“Tunatambua kuwa pamoja na maudhui mengine katika miswada hii, kuna kipengele muhimu ambacho kinalazimisha mikataba yote iliyosainiwa awali, ya gesi na mafuta, isibatilishwe.
“Mikataba ambayo leo hii ipo katika utekelezaji imekuwa ikilalamikiwa na watu wengi kuwa ina mapungufu makubwa na hivyo inalikosesha Taifa mapato mengi,” alisema Mbowe katika mkutano uliohudhuriwa pia na baadhi ya wabunge wa CUF na Chadema.
Alisema kwa sababu uongozi wa Bunge umewadhalilisha kwa kuwatoa wabunge 43 bungeni kinyume cha taratibu, ni dhahiri ulikusudia kuipitisha miswada yote bila kujali ushauri.
Mbowe alisema uongozi unaomaliza muda wake una agenda ya siri inayoufanya kulazimisha sheria hizo kupitishwa katika utaratibu huo.
MWANANCHI
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime amewataka wageni wasiokuwa na shughuli muhimu ya kufanya mkoani hapa kutokuja katika kipindi cha juma hili ili kuepusha usumbufu utakaojitokeza.
Misime alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu wiki hii ambayo inatarajiwa kuwa na ugeni mkubwa wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM ambao amesema kuwa unakadiriwa kuwakusanya watu takribani 10,000.
Alisema ili kuepusha usumbufu utakaojitokeza kama vile kukosa mahali pa kulala, ni vyema kama mtu hana shughuli ya muhimu ya kufanya mjini hapa asije mpaka mkutano huo utakapokwisha.
“Kuna wengine wanataka kuja kwa ajili ya ushabiki tu au kuja kushuhudia tukio zima na hata kama hawatakuja haitawaathiri kitu hivyo ni vyema wasije ili kuepusha usumbufu,”  Misime.
Alisema Jeshi la Polisi limejipanga kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi wote watakaofika katika mkutano huo na kuwataka wananchi kutoa taarifa za viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.
Aliwataka wamiliki wa nyumba za kulala wageni kuhakikisha kuwa vitu vyote vyenye thamani vya wateja wao vinatunzwa vizuri ili kuepusha usumbufu au kupotea kwenye mikono yao.
Jana, Polisi waliimarisha ulinzi bungeni kwa kuongeza idadi ya askari na pia kufunga kipande cha barabara kuanzia kwenye mzunguko wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani kupitia eneo la Bunge hadi mwanzo wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Tawi la Dodoma.
Kulikuwa na idadi kubwa ya polisi wa usalama barabarani, utepe mweupe uliofungwa katika barabara hiyo huku kukiwekwa kibao kilichoandikwa kwa maandishi mekundu, “barabara hii imefungwa.”
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema kufungwa kwa barabara hiyo ni miongoni mwa shughuli za usalama.
NIPASHE
Wakati joto la uchujaji wa majina ya wagombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) likizidi kuongezeka, taarifa zimezidi kuzagaa mitaani na kwenye mitandao ya kijamii kwamba, mikakati ya kumuondoa Edward Lowassa kwenye orodha ya watia nia nayo imezidi kupamba moto.
Ofisa mmoja wa CCM makao makuu mjini hapa, alisema kuwa wanachofanya wao kama watendaji ni kuandaa majina ya wagombea wote na fomu zao za udhamini na kisha kukabidhi kwa sekretarieti itakayopanga ajenda za vikao vya Kamati Kuu na baadaye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya taifa.
Ofisa huyo alipoulizwa kama ana taarifa za kuwako kwa mizengwe dhidi ya Lowassa alisema kwa ujumla kwa sasa kuna maneno mengi sana yanazungumzwa juu ya mchakato wa uteuzi wa mgombea, ila akasisitiza kuwa la msingi ni kusubiri vikao vya maamuzi.
“Ndugu yangu ukiyatazama haya makundi (ya urais) ni vigumu kuamini kama wanatoka chama kimoja. Yaani kuna kukamiana kweli kweli…Kila mmoja anataka kumwangusha mwenzake ili yeye apite,” alisema na kuongeza kuwa:
“Hata kama kuna mizengwe, si unajua uchaguzi huu ni wa vyama vingi. CCM haishindani pekee yake, kwa hiyo mgombea anayekubalika ndiye anatakiwa.”
Hata hivyo, kwa muda sasa kumekuwa na mfululizo wa habari za kupikwa kwamba jina la Lowassa litaishia Kamati Kuu kwa madai kwamba kuna ushahidi wa matumizi ya fedha kwa timu yake, tuhuma ambazo binafsi (Lowassa) amezikanusha mara kadhaa.
Julai mosi mwaka huu siku anarejesha fomu za kuwania urais kupitia CCM alitoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa kuhusika kwake na rushwa ajitokeza na kusema alitoa lini, wapi na kwa nani.
Lowassa alisema amechoka kwa tuhuma za kipuuzi za kuhusishwa na rushwa na kusisitiza kuwa hakuna mwanachama yeyote miongoni mwa zaidi ya nane waliomdhamini aliyefanya hivyo kwa kishawishi cha fedha au fadhila yoyote.
Mgombea anayetajwa kutumiwa zaidi na kundi linalompinga Lowassa ni pamoja na Makongoro Nyerere, ambaye alifanya mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni na kuporomosha kauli kali za ukakasi dhidi ya Lowassa.
Wakati mizengwe ikizidi kusukwa dhidi ya Lowassa, ripoti ya kura zote za maoni ambazo zimekuwa zikitolewa katika miezi ya hivi karibuni zimeonyesha kuwa Lowassa anaongoza kwa mbali kama chaguo la wananchi wengi kwenye nafasi hiyo.
Miongoni mwa tafiti hizo ni ule wa Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, uliofanywa mwezi uliopita na matokeo yake kutolewa mwishoni mwa wiki unaonyesha kuwa Lowassa ni changuo la kwanza la wengi kwa kujipatia asilimia 27.0 ndani ya chama hicho, huku Bernard Membe akishikilia nafasi ya pili kwa kupata asilimia 8.2.
Katika utafiti huo ambao REDET walisema kuwa unaweza kuchukuliwa kwa ujumla wake kama maoni ya Watanzania endapo masuala yaliyoulizwa uchaguzi ungefanyika katika kipindi cha utafiti, wahojiwa walikuwa 1,250 kutoka wilaya moja moja katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Wakati mkakati wa mizengwe ukiendelea kupamba moto, wajumbe wa sekretarieti ya Kamati Kuu ya chama hicho wanaanza vikao mjini hapa leo kundaa pamoja na mambo mengine ajenda na taarifa kwenye vikao vya Kamati Kuu itakayokaa Alhamisi mjini hapa.
Kikao cha Kamati Kuu kinatarajiwa kuchuka majina ya watia nia 38 waliojitokeza kutafuta ridhaa ya chama hicho na kubakisha majina matano tu yatakayopelekwa NEC kwa kupigiwa kura.
NEC inayotarajiwa kukutana Ijumaa wiki hii, itatoa majina matatu kwenda Mkutano Mkuu unaotarajiwa kukutana Jumamosi kwa ajili ya kupata jina moja la mgombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
NIPASHE
Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeongeza majimbo ya uchaguzi kwa Zanzibar kutoka 50 hadi 54.
Hata hivyo, majimbo yaliyoongezwa ni ya upande wa Unguja wakati Pemba imeendelea kuwa na majimbo 18 kama ilivyokuwa awali.
Hatua hiyo ya Zec kuongeza majimbo ya uchaguzi inatokana na tume hiyo kupewa mamlaka ya kuchunguza mipaka na majimbo ya uchaguzi na baada ya uchunguzi inaweza kubadili idadi, mipaka na majina ya majimbo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari visiwani hapa kuhusiana na mabadiliko ya idadi, mipaka na majina ya majimbo ya uchaguzi jana, Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salum Jecha, alisema tume hiyo imetumia vigezo na maoni ya wadau wa uchaguzi vikiwamo vyama vya siasa katika ugawaji wa mipaka ya majimbo.
Jecha alisema tume hiyo pia katika ugawaji huo imezingatia idadi ya watu na zaidi katika kuhakikisha uwakilishi unaofaa katika miji mikubwa na miji ya mashamba yenye idadi ndogo ya watu, njia za usafiri na mipaka ya sehemu ya utawala.
Majimbo mapya yaliongozeka kwa upande wa Unguja katika wilaya ya Magharibi ni Chukwani, Pangawe, Kijitoupele na Welezo.
Aliyataja majina mapya ya majimbo kwa Unguja kuwa ni Mahonda, Kiwengwa, Kijini, Tunguu, Paje, Shaurimoyo, Malindi, Mtopepo na kwa upande wa Pemba ni jimbo la Wingi.
Utaratibu huo wa tume ya uchaguzi umefanya Unguja kuwa na majimbo 36 ambapo awali kulikuwa na majimbo 32 na kisiwani Pemba idadi ni ileile ya wali ya majimbo 18.
Majina ya majimbo ya awali ambayo kwa sasa hayatatumika tena ni jimbo la Kitope ambalo linashikiliwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, kwa nafasi ya ubunge. Mengine ni la Rahaleo, Mjimkongwe, Magogoni, Mkanyageni, Matemwe, Muyuni na Koani.
 Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chama cha Wananchi (CUF), Ismail Jussa Ladhu, alisema chama hicho kimepokea kwa furaha kubwa sana taarifa ya tume hiyo ya mapitio ya majimbo kutoka majimbo 50 ya sasa hadi 54.
“Ushindi katika uchaguzi mkuu unapatikana kwa wananchi kujiandikisha na kwenda kupiga kura, sio ukataji wa majimbo kwani mkato huo wa mipaka ya majimbo umeturahisishia sana kazi ya kushinda katika uchaguzi mkuu,” Jussa.
Jussa ambaye pia ni mwakilishi wa Jimbo la Mjimkogwe ambalo sasa litakuwa ni jimbo la Malindi, alisema licha ya tume hiyo kumaliza kazi ya mapitio ya majimbo, lakini haikuzingatia maoni ya wadau na badala yake imejiamulia kuongeza majimbo wakati hakukuwa na sababu ya kuongeza majimbo hayo.
Alisema: “Tume haijazingatia mipaka ya utawala, idadi ya watu katika miji mikubwa ya mijini na miji midogo ya shamba.”
Hata hivyo, alisema licha ya tume hiyo kuamua kuongeza majimbo 54, lakini bado CUF kina uhakika wa kushinda majimbo 34 ya uchaguzi katika uchaguzi mkuu na kuigaragaza CCM.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibae, Vuai Ali Vuai, alisema wameridhika na maamuzi ya tume kuongeza majimbo manne, lakini akaeleza kuwa tume hiyo haikutenda haki kwa majimbo ya Pemba.
Alisema kuwa kwa mujibu wa idadi ya watu iliyopo Pemba, ilipaswa tume hiyo kupunguza majimbo kisiwani humo badala ya majimbo 18, yawe majimbo 16.
“Licha ya tume kuamua, lakini sisi hatuna pingamizi na tume hiyo kwa sababu tume hiyo ndio waamuzi,” alisema Vuai.
Alisema CCM itaanza kutoa fomu za kuwania ubunge, udiwani na uwakilishi kuanzia Julai 15 na  ana imani kubwa kuwa CCM itashinda kwa kishindo kikubwa katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Oktoba, mwaka huu.
Ali Makame kutoka chama cha ACT Wazalendo, alisema chama hicho kimepokea kwa hisia nzuri maamuzi hayo ya Zec kutokana na uwezo waliopewa.
“Licha ya taarifa hiyo ya tume ya uchaguzi kuongeza majimbo 54, lakini haki haikutumika kama tulivyotegemea kwani baadhi ya majimbo tumeona kuwa na shehia nyingi na baadhi kuwa na shehia kidogo,” alisema Makame.
Aidha, alisema kwa kuwa hakuna sheria inayoruhusu kuwa na pingamizi kutokana na maamuzi ya tume hiyo katika uchunguzi na ugawaji wa majimbo, inabidi wakubali matokeo.
Zec ilianza kazi ya uchunguzi wa idadi, mipaka na majina ya majimbo ya uchaguzi Juni 9, mwaka 2014 kwa kupokea na kusikiliza maoni ya wadau wa uchaguzi kwa mujibu wa kifungu cha 120(3) ya Katiba ya Zanzibar.
Kabla ya tume hiyo kufanya kazi hiyo na kuamua kuongeza majimbo 54 kutoka 50 kazi kama hiyo ilifanyika mwaka 2004 na Pemba ilipunguzwa majimbo matatu na kuwa na majimbo 18 kutoka ya awali 21 na Unguja ikaongezewa majimbo mawili kutoka majimbo 29 ya awali.
NIPASHE
Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kitaitisha maandamano kwenye mikoa yenye gesi ili kulishinikiza Bunge kupinga muswada wa mafuta na gesi uliopitishwa juzi.
Akihutubia wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji na viunga vyake, Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema haoni mantiki na hakuna sababu ya kufanya haraka kupitisha muswada huo.
“Suala hili linahitaji mjadala wa kina utaohusisha wadau mbali mbali, wataalamu na wananchi kwa ujumla wake,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“CUF inaunga mkono jitihada za wabunge wa kambi ya upinzani kwa hatua zao kupinga muswada huo, ambao haukujali na wala haukuzingatia maslahi ya Taifa.”
Alisema CUF inatoa angalizo kwa Rais Jakaya Kikwete kwamba kwa hali inavyoenda huenda akaenda kufunga Bunge litalokuwa na Wabunge wa CCM pekee.
“Hiyo inatokana na ukweli kwamba Spika wa Bunge amepoteza muelekeo na ameshindwa kabisa kuliongoza Bunge kwa mujibu wa kanuni walizojiwekea katika kutimiza wajibu,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Kwa hiyo  basi, Rais Kikwete atakuwa amefuata nyayo za Rais wa Zanzibar.”
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein Juni 26, mwaka huu alilivunja Baraza la Wawakilishi bila Wawakilishi wa CUF kuwapo barazani.
Wajumbe hao walisusia Baraza hilo kutokana na kutoridhishwa na uandikishaji wa wapigakura katima daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo wa kielektroniki unaojulikana kama Biometric Voters Registrarion (BVR), wakisema kuwa uandikishaji huo ulitawaliwa na ubabe.
Profesa Lipumba alionya kuwa kama Bunge litaendelea na mpango wake huo, basi CUF  ataitisha maandamano ili kupinga muswada huo.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alisema kuwa Mkoa wa Kigoma unaweza kuendelea kiuchumi ikiwa utatumia vizuri rasilimali zilizoko akitolea mfano Hifadhi ya Taifa ya Gombe kwamba ikitumika vizuri inaweza kuingiza mapato mengi.
Alisema kwamba jiografia ya Mkoa wa Kigoma inauruhusu kupata fursa nyingi za kuendelea kiuchumi kwa kuwa wananchi wake wanaweza kufanya biashara na nchi zinazouzunguka za Burundi Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
HABARILEO
Vilio na simanzi vilitawala katika eneo la mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona, kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela.
Wake wa Mramba na Yona na waliodaiwa kuwa ni watoto wao walionekana wakilia kila wakati mahakamani hapo, huku ndugu, jamaa na marafiki wakiwa wanawabembeleza na kuwaambia wamuachie Mungu.
Hata hivyo, baadhi ya ndugu jamaa na marafiki wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, walionekana kuwa na furaha baada ya mahakama kumwachia huru.
Washtakiwa hao wamehukumiwa baada ya kupatikana na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 yaliyokuwa yanawakabili wote watatu.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jopo la Mahakimu watatu likiongozwa na Hakimu John Utamwa, mahakimu wengine ni Sam Rumanyika na Saul Kinemela.
Akisoma hukumu hiyo iliyowahi kuahirishwa mara mbili, Hakimu Rumanyika alisema Mramba amepatikana na hatia ya mashitaka 11 na Yona kwa mashitaka matano.
Katika adhabu ya Mramba, Hakimu Rumanyika alisema, kuanzia kosa la kwanza hadi la kumi linalohusu matumizi mabaya ya Ofisi kinyume cha sheria, anahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na haina masharti ya kulipa faini.
Katika shitaka la 11 la kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7, alisema Mramba anatakiwa kulipa faini ya Sh milioni tano au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Kuhusu Yona, Hakimu Rumanyika alisema anahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya mashitaka matano kati ya 11 yaliyokuwa yanamkabili.
Alisema amepatikana na hatia ya matumizi mabaya ya Ofisi ikiwa ni kinyume cha sheria, hivyo anahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela aidha mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya fedha hizo, atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh milioni tano.
Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Hakimu Rumanyika alisema, Mgonja hajapatikana na hatia yoyote, hivyo Mahakama inamuachia huru.
Baada ya kusoma hukumu hiyo kwa zaidi ya saa moja na nusu, Mramba na Yona waliwekwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Magereza kabla hawajashuka kizimbani huku baadhi ya ndugu waliofika mahakamani wakiangua kilio na ndugu wa Mgonja wakiwa na furaha huku wakimshukuru Mungu.
Katika kesi hiyo washitakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashitaka 11, mashitaka 10 yanahusu Matumizi mabaya ya madaraka na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
Upande wa Jamhuri uliita mashahidi saba kuthibitisha kesi hiyo ambapo Mahakama iliwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu na katika utetezi wao washitakiwa walijitetea wenyewe na kuita mashahidi wawili.
Kwa mara ya kwanza washitakiwa walifikishwa mahakamani hapo mwaka 2008 ikiwa ni miaka saba iliyopita, wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia Serikali hasara ya kiasi hicho kutokana na msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya dhahabau ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.
Katika utetezi wake Mramba alikiri kuisamehe kodi kampuni hiyo kwa kuwa kulikuwa na mkataba uliosainiwa Juni 2003 kati ya Kampuni hiyo na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao ulikuwa unaonesha malipo yafanyike bila ya kukatwa kodi.
Hata hivyo upande wa Jamhuri ulidai, msamaha huo ulitolewa wakati tayari Wizara ilikuwa imepokea barua za kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo zilikuwa zinakataa kampuni hiyo isisamehewe kodi.
HABARILEO
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza ameshitakiwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki iliyopo jijini Arusha kutokana na hatua yake inayotajwa kukiuka Katiba ya nchi hiyo kwa kuwania kipindi cha tatu cha Urais.
Kesi hiyo, ambayo pia inamjumuisha Mwanasheria Mkuu wa Burundi, Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi kwa nchi ya Burundi pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mujibu wa taarifa maalum kutoka kwenye taasisi ya mawakili wa Kanda ya Afrika (PALU) inayosimamia shauri hilo.
Hii sasa inamaanisha kuwa kiongozi huyo wa Burundi atahitajika wakati wowote kwenda Arusha mahakamani, kuhudhuria kesi yake.
Ripoti hiyo iliyoidhinishwa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha PALU, Jancelline Amsi, imeeleza kuwa shauri hilo namba RCCB 303 la 2015 dhidi ya Nkurunziza liliwasilishwa katika Mahakama ya Jumuiya na Umoja wa mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi na Tanzania chini ya mwamvuli wa taasisi yao ya ‘East African Civil Society Organizations’ Forum (EACSOF).
Mashirika hayo yanamtuhumu Rais Nkurunziza kwa kukiuka katiba ya nchi yake pamoja na kuvunja makubaliano ya Amani ya Arusha katika dhamira yake ya kugombea urais kwa kipindi cha tatu, hatua ambayo imesababisha machafuko nchini Burundi yaliyopelekea vifo vya wananchi wapatao 70 huku wengine zaidi ya 140,000 wakiikimbia nchi yao.
Hatua hiyo inakuja wakati Rais Nkurunziza akiwa amejikita katika kampeni za urais, hivyo kushindwa kujumuika na wakuu wa nchi za EAC wanaokutana Dar es Salaam kujaribu kutafuta ufumbuzi wa tatizo la kisiasa la Burundi.
Msemaji wa Rais Nkurunziza, Gervais Abahiro alieleza kutoka Bujumbura alisema kuwa bosi wake huyo angewasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Alain Aime Nyamitwe kwani Rais wake alikuwa anaendelea na kampeni zake za urais.

No comments:

Post a Comment

advertise here