LAYIII
MWANANCHI
NIPASHE
#MAGAZETINI JULY6…Mume kumnyonga mjamzito, wiki ngumu CCM na kompyuta yaibiwa kituo cha kupigakura
Zikiwa zimebakia siku sita kwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kumpata mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa
Oktoba 25, mwaka huu, kura ya maoni iliyoendeshwa na Mpango wa Utafiti
na Elimu ya Demokrasia (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, inamweka kileleni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa changuo la kwanza la wengi kwa kujipatia asilimia 27.0 ndani ya chama hicho.
Wakati Lowassa akiwafunika watia nia wenzake ndani ya CCM, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, anawafunika wenzake kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) akiwa changuo la wengi kwa asilimia 23.1.
REDET wamesema kuwa matokeo ya utafiti
huo yanaweza kuchukuliwa kwa ujumla wake kama maoni ya Watanzania endapo
masuala yaliyoulizwa uchaguzi ungefanyika katika kipindi cha utafiti.
“Sampuli iliyotumika katika utafiti huu kwa kiwango cha kutosha ni wakilishi na ina akisi hali halisi ya Watanzania,” imesisitiza ripoti hiyo iliyojatwa kuwa ni maoni ya wananchi kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 2015, mwaka huu.
Katika utitiri wa watia nia ndani ya
CCM, kati ya wahojiwa 1,250 waliohojiwa, Lowassa alipigiwa kura na watu
338, wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, akipata asilimia 8.2 akichaguliwa na watu 103.
Utafiti wa REDET ulifanyika katika
wilaya moja moja kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara baada ya wahojaji
kukataliwa ruhusa ya kufanya utafiti wao katika mikoa mitano ya
Zanzibar.
Utafiti huo uliokuwa umedhaminiwa na
kampuni ya Business Times Limited, ulifanyika kati ya Juni 23-26, mwaka
huu na kila wilaya ilikuwa na wahojiwa 50.
Kwa upande wa CCM watia nia wengine ni Mizengo Pinda nafasi ya tatu akiwa na asilimia 7.2 akichaguliwa na watu 90; John Magufuli nafasi ya nne akipata asilimia 6.6 akipigiwa kura na watu 83 na Charles Makongoro Nyerere nafasi ya tano akipigiwa kura na watu 54.
Wengine ni Mark Mwandosya nafasi ya sita akipata asilimia 3.1 akichaguliwa na watu 39; Dk. Harrison Mwakyembe nafasi ya saba akiwa na asilimia 1.4 akichanguliwa na watu 18; Frederick Sumaye nafasi ya nane akipata asilimia 1.4 akichaguliwa na watu 17; nafasi ya tisa imekamatwa na Jaji Augustino Ramadhani akiwa na asilimia 1.2 akichaguliwa na watu 15 na nafasi ya 10 amekamata Mwigulu Nchemba akiwa na asilimia 1.0 akichaguliwa na watu 13.
Wengine na idadi ya waliowachagua na asilimia zao kwenye mabano ni January Makamba nafasi ya 11 (asilimia 0.8, watu 10); Dk. Asha-Rose Migiro nafasi ya 12 (asilimia 0.7, watu tisa); Samuel Sitta nafasi 13 (asilimia 0.6. watu wanane); Lazaro Nyalandu nafasi ya 14 (asilimia 0.4, watu watano).
Pia wamo Prof. Sospeter Muhongo nafasi ya 15 (asilimia 0.4, watu watano); Balozi Amina Salum Ali nafasi ya 16 (asilimia 0.2, watu wawili); Dk. Mohammed Gharib Bilal nafasi ya 17 (asilimia 0.2, watu watatu); Stephen Wasira nafasi ya 18 (asilimia 0.2, watu 3) na William Ngeleja nafasi ya 19 (asilimia 0.2, watu wawili).
Wengine ni Balozi Ally Karume nafasi ya 20 (asilimia 0.1, mtu mmoja); Amos Siyantemi nafasi ya 21 (asilimia 0.1, mtu mmoja); Joseph Chagama nafasi ya 22 (asilimia 0.1, mtu mmoja); na Mwele Malecela nafasi ya 23 (asilimia 0.1, mtu mmoja).
Katika kura hiyo, watia nia 14 ambao wamejitosa kwenye urais kupitia CCM hawakutajwa kabisa na watoa maoni ambao ni Balozi Augustine
Mahiga; Boniphace Ndengo; Eldophonce Bihelo; Godwin Mwaipopo; Dk. Hamis
Kigwangalla; Dk. Hans Kitine; Joseph Chagana; Leons Mulenda; Luaga
Mpina; Maliki Marupu; Mathias Chikawe; Monica Mbega; Titus Kamani na Balozi Patrick Chokala.
Kwenye kundi la Ukawa, namba mbili amechukua Prof. Ibrahim Lipumba akiwa na asilimia 13.6 akichaguliwa na watu 170; Freeman Mbowe ameshika nafasi ya tatu akiwa na asilimia 7.2 akichaguliwa na watu 90; James Mbatia amekamata nafasi ya nne akiwa na asilimia 3.2 akichaguliwa na watu 40; Emmanuel Makaidi akishikilia nafasi ya tano kwa asilimia 0.6 akichaguliwa na watu 8, huku George Kahangwa akishika nafasi ya sita kwa asilimia 0.2 akichaguliwa na watu wawili.
Swali la msingi lililokuwa linaulizwa lilisema: “Kama
wewe leo ungeshirikishwa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa
tiketi ya CCM, kati ya wanachama wake 37 waliokwishajitokeza,
ungemchagua nani apeperushe bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba 2015?”
Pia swali kwa Ukawa lilikuwa:
“Kama wewe leo ungeshirikishwa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea
urais kwa tiketi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), kati ya wanachama wake waliokwishakutangaza nia na wanaotarajia
kutangaza nia ungemchagua nani apeperushe bendera ya Ukawa katika
uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba 2015?”
Ripoti ya REDET imesema kuwa kwa maswali
yote, mhoji alitakiwa kutomtajia majina mhojiwa, bali mhojiwa aliombwa
ataje jina alilonalo kichwani mwake.
NIPASHE
Hatma ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, jijini Dar es Salaam, kusoma au kutokusoma hukumu ya kesi
inayowakabili mawaziri waandamizi wa zamani, Basil Mramba, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hazina, Gray Mgonja wanaokabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7 itajulikana leo.
Mahakama hiyo imepiga kalenda kusoma
hukumu hiyo mara mbili tofauti kati ya Juni 30 na Julai 3, mwaka huu
kutokana na sababu tofauti ikiwamo jopo linalosikiliza kesi hiyo
kutokukamilika.
Mapema Juni 30, mwaka huu saa 3:00 asubuhi, jopo la mahakimu wawili, likiongozwa na Mwenyekiti Jaji John Utamwa na Samu Rumanyika walipiga kalenda kusoma hukumu hiyo hadi Julai 3, mwaka huu baada ya mjumbe Hakimu Saul Kinemela kuwa na udhuru wa kikazi.
Hata hivyo, Julai 3, mwaka huu mahakama
hiyo kwa mara ya pili, ilipiga kalenda kusoma hukumu hiyo kwa madai kuwa
Mwenyekiti wa jopo, jaji Utamwa ni mgonjwa.
Katika kesi hiyo washtakiwa hao pia wanadaiwa kutumia madaraka vibaya na kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart (Assayers), Government Business Corporation kufanya ukaguzi wa madini ya dhahabu nchini.
Kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai,
kosa la matumizi mabaya ya madaraka adhabu zake ni kulipa faini ya Sh.
milioni mbili au kifungo cha kati ya mwaka mmoja au miaka mitatu jela
baada ya mshtakiwa kupatikana na hatia.
Katika mashtaka hayo ilidaiwa kuwa
washtakiwa wakiwa watumishi wa serikali, Oktoba 10, mwaka 2003 walikaidi
ushauri wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa kuwataka wasitoe msamaha kwa Kampuni ya Alex Sterwart (Assayers) Government Business Corporation.
NIPASHE
Mbunge wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia, amesema hakuna Spika aliyewahi kuonyesha udhaifu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama alivyoonyesha Anna Makinda.
Amesema Makinda ameligawa vipande vipande Bunge la 10 na kutumiwa na mhimili wa utawala.
Mbatia alisema badala ya Bunge
kuisimamia serikali, lakini Makinda ameshindwa kuliongoza Bunge hilo
kutokana na shinikizo la mhimili wa utawala na kulazimika kufuata
matakwa ya CCM na hivyo kuliongoza kwa ubabe.
Alisema tofauti na ilivyokuwa katika kipindi cha Samuel Sitta na Pius Msekwa
ambao walionyesha weledi na kuliongezea heshima Bunge, lakini Makinda
ameriharibu kutokana na kuacha kusimamia Katiba ya nchi katika
kuliongoza Bunge hilo.
“Siku
zote mwanamke ndiye huwa ni mtu wa mwisho kuligawa Taifa, lakini
limekuwa ni jambo la ajabu sana kuona mwanamke huyo ambaye angekuwa
mstari wa mbele katika kuitetea nchi hii, lakini ameamua lifie mikononi
mwake, hata bila kuficha ameonyesha wazi kwamba anatumika na serikali na
CCM, Makinda yeye siyo kiranja wa bunge ni mratibu tu,” Mbatia.
Aliongeza:
“ Badala ya Bunge kusimamia serikali kama Mhimili unaojitegemea,
limejivua kazi yake na kuwa kiungo cha serikali na inalisimamia, na
ndiyo maana hata juzi mlisikia Serikali inasema imeoliongezea Bunge
siku, badala ya Bunge lijiongezee lenyewe, hii ni fedheha.”
Mbatia alisema suala la kupelekwa
bungeni kwa hati ya dharura na kujadiliwa miswaada mitatu ya mafuta na
gesi ni ajenda ya siri ya kutaka kuiweka gesi kama dhamana ya CCM ya
kupata fedha ya uchaguzi na kwamba hicho ni kiashiria cha kuanza kuiuza
nchi rejareja.
“Raslimali
hizi badala ya kuwa neema kwa Watanzania, sasa inakuwa balaa, watu
wachache wanataka kuwaibia Watanzania, hivi unawezaje kuwekaje miswaada
hii muhimu kujadiliwa kwa pamoja na kuipeleka harakaharaka hivyo, sisi tumesema hatukubali kuona hujuma hizi zinafanyika dhidi ya rasilimali na Taifa,”Mbatia.
Mbatia alisema msimamo wa Wabunge wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) uko wazi, kwamba hawako tayari
kujadiliwa miswaada hiyo kwa hati ya dharura na pia hawatashiriki wakati
wa kuvunjwa bunge hilo Julai 9, mwaka huu.
Pia aliongeza kuwa hata wakiitwa katika meza ya maridhiano na Makinda hawatakuwa tayari kushiriki.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye,
alipoulizwa juu ya taarifa hizo za kwamba chama hicho kina ajenga ya
siri ya kuifanya gesi kusaidia kuwa dhamana katika uchaguzi, alijibu
kwa kifupi kwamba ni uzushi.
HABARILEO
Mlinzi wa usiku katika Ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Florence Kazonde amejinyonga baada ya kumuua kikatili kwa kumkaba koo mkewe aliyekuwa na ujauzito wa miezi tisa, Emilia Mzui.
Chanzo cha mauaji hayo kimeelezwa kuwa
ni wivu wa kimapenzi. Tukio hilo limethibitishwa na Jeshi la Polisi
mkoani Rukwa, majirani na ndugu wa karibu wa familia ya marehemu hao
waliokuwa wanaishi katika Kitongoji cha Namlangwa mjini Matai yalipo
makao makuu ya wilaya ya Kalambo.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Halmashauri hiyo, Ramadhan Juma,
alikiri kuwa Kazonde alikuwa mlinzi wa ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri hiyo zilizopo nje kidogo ya Mji wa Matai, lakini hakuwa
mwajiriwa wa halmashauri hiyo.
“Kazonde alikuwa anatoka katika kampuni moja ya ulinzi…hakuajiriwa na Halmashauri hii,“ alisisitiza Juma.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alieleza kutokuwa na taarifa za mkasa huo kwamba akizipata atazitolea taarifa.
Hata hivyo taarifa kutoka Jeshi hilo la Polisi mkoani humo limethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Kweli kuna hilo tukio limetokea wilayani Kalambo … taarifa zipo tayari
lakini kwa kuwa mie si msemaji wa Jeshi hili siwezi kutoa maelezo zaidi
ya kina lakini nikiri kuwa tukio hilo limetokea …Kwa utaratibu wa Jeshi
letu ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa ndiye msemaji na si vinginevyo.
Baadhi ya majirani na ndugu wa karibu
kwa masharti ya kutoandikwa gazetini walieleza kuwa walibaini vifo hivyo
baada ya kufika nyumbani kwa wanandoa hao ili kuwasabahi lakini
walikuta milango ya nyumba hiyo imefungwa kwa ndani.
“..Tulihisi
labda walikuwa bado wamelala lakini kila tukibisha hodi ni watoto tu
waliokuwa wakiitikia …… “Mazingira hayo yalitutia mashaka makubwa
tukahisi kuwa kwa kuwa mke wake siku zake za kujifungua zilikuwa
zimekaribia tuliamini kuwa walikuwa wamekwenda hospitali na kuwaacha
watoto wakiwa wamejifungia ndani na kushindwa kufungua milango hiyo, “ alisema mtoa taarifa.
Ilielezwa kuwa ndugu na majirani hao waliamua kufungua mlango kwa nguvu ili wawatoe watoto hao wadogo nje ambao walikuwa wawili.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa baada ya
kufungua mlango wa nyumba hiyo kwa nguvu mmoja wa watoto hao aliwaonesha
ishara kuwa chumbani kwa wazazi wao kuna kitu cha kutisha ndipo
walipolazimika kuingia chumbani humo na kuona mwili wa Kazonde ukiwa
umening’inia darini ukiwa na kamba ya katani shingoni ambapo mwili wa
marehemu mkewe ulikuwa kitandani.
“Inatisha
na kusikitisha sana ….tuligundua kuwa wote wawili walikuwa wafu tukatoa
taarifa mara moja katika Kituo cha Polisi hapa mjini Matai …… askari
Polisi walifika na waganga ambao walifanyia uchunguzi miili hiyo na
kuthibitisha kuwa Kazonde alikuwa amejinyonga baada ya kumuua mke wake
kikatili kwa kumkaba koo,” aliongeza mmoja wa ndugu wa karibu.
Taarifa kutoka eneo hilo la tukio
zinaeleza kuwa kwa muda mrefu wanandoa hao walikuwa wakigombana mara kwa
mara ambapo mume alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa na mahusiano ya
kimapenzi na wanaume wengine na kwamba kati ya watoto wao wawili mmoja
sio wake ni wa mwanamume mwingine.
HABARILEO
Kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM -Zanzibar kwa kauli moja imependekeza kwa Kamati Kuu
jina la Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuteuliwa kuwania tena kiti cha Rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai,
kikao hicho maalumu pamoja na mambo mengine, kilipokea na kujadili jina
la Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Zanzibar, Dk Shein.
Kikao hicho kilichoongozwa kwa muda na
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilal kilipokea taarifa ya
jina la Dk Shein ambaye ni mgombea pekee kwa nafasi hiyo.
“Kamati
Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar kwa kauli moja
inapendekeza kwa Kamati Kuu jina la mgombea wa nafasi ya Urais wa
Zanzibar kuwa ni Dk Ali Mohamed Shein kuwania nafasi hiyo kwa kipindi
cha miaka mitano,” Vuai.
Vuai alisema wajumbe kwa kauli moja
wamependekeza jina la Shein kuwania nafasi hiyo baada ya kuridhishwa na
utendaji wake unaotokana na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka
2010/2015 kwa vitendo katika maeneo yote muhimu.
Alisema utekelezaji huo umeiwezesha
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupata mafanikio katika maeneo mbalimbali
ya bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2015-2016 ikiwemo kuweka kipaumbele
kwa miradi ya jamii pamoja na maendeleo.
Akimkaribisha Dk Shein, baada ya
kumalizika kwa kikao hicho, Mwenyekiti wa muda, Dk Bilal, alimkabidhi
kiti, ili kuendelea na mambo mengine.
Naye Dk Shein alishukuru na kukipongeza
kikao hicho, kwa kufanikisha kazi hiyo muhimu na nzito kwa mafanikio
makubwa na kuahidi kuwa ataendelea kuwa mwadilifu na mwaminifu mbele ya
CCM, jamii nzima ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.
HABARILEO
Mahakama ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imemhukumu Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbende, Alei Charles (CHADEMA) kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukiri kumlinda mshtakiwa Wenceslaus Namwanda “Pepea” anayemiliki shamba la bangi.
Mshitakiwa Namawanda ambaye pia ni mkazi wa kijiji cha Mbende anakabiliwa na kosa la kumiliki shamba la bangi.
Hakimu wa mahakama hiyo, Adam Mwanjokolo
alitoa adhabu hiyo baada ya mshtakiwa huyo mwenye miaka 30 kukiri
kutenda kosa hilo mahamakani hapo .
“Nimelazimika
kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa viongozi wengine wenye tabia
kama yako (Alei)… hivyo utatumikia kifungo cha miaka miwili jela,“ Hakimu Mwanjokolo.
Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa
Polisi, Hamimu Gwelo alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa
hilo Mei 14 , mwaka huu katika kijiji cha Mbende , saa 3 usiku.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa usiku huo
wa tukio Alei aliwadanganya maofisa wa polisi kuwa mshtakiwa Namwanda
hakuwa mkazi wa kijiji hicho hivyo aliwaelekeza kwa Mwenyekiti wa kijiji
cha jirani.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka,
maofisa hao walithibitishiwa na Mwenyekiti wa kijiji cha jirani kuwa
mshitakiwa wanayemtafuta anaishi katika kijiji cha Mbende ambapo
aliongozana nao hadi nyumbani kwake.
“Maofisa
wa Polisi walipofika nyumbani kwa mshtakiwa Namwanda walipobisha hodi
ghafla alitoka mtu baada ya kuona askari alitimua mbio, askari
walifanikiwa kumkamata na ikagundulika kuwa ni Mwenyekiti wa Kijiji cha
Mbende ambapo alikiri kuwa alifika nyumbani kwa mshtakiwa na kumtaarifu
atoroke kwa kuwa alikuwa akitafutwa na Polisi,” alieleza Mwendesha Mashtaka.
Akijitetea mshitakiwa huyo aliomba
apunguziwe adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza. Pia ana watoto
wategemezi wawili wa marehemu dada yake ambapo mama mzazi anaishi naye
baada ya mumewe kufariki dunia.
MWANANCHI
Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi ametangaza kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Arfi aliwaeleza wananchi wa Mpanda kuwa uanachama wake ndani ya Chadema utakoma mara tu baada ya kuvunjwa Bunge Julai 9.
Pia, alitumia mkutano huu kuwaaga wananchi wa jimbo hilo akisema hatagombea tena nafasi hiyo aliyoitumikia kwa miaka 10.
Arfi alifafanua kuwa hayuko tayari kugombea jimbo hilo kupitia chama
chochote cha siasa na kauli hiyo imelenga kuondoa uvumi uliokuwa umeenea
kwamba alikuwa na nia ya kugombea kupia ama ACT – Wazalendo au CCM.
Alisema amekuwa akishangazwa na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na
baadhi ya wanachana na wapenzi wa Chadema kuwa hajafanya lolote kwenye
chama hicho.
Alisema kama kuna mtu anayekifahamu vizuri chama hicho ni yeye, hivyo haoni sababu za watu kumbeza.
Alisema alikuwa ameamua kukaa kimya na kuwa akiamua ‘atamwaga mboga’ ili watu wafahamu upungufu ulioko ndani ya chama hicho.
Alisema hagombei katika jimbo hilo na kama kweli chama hicho kina
nguvu, basi kilitetee, akisisitiza kuwa ana uhakika jimbo hilo
litakwenda CCM kwa kuwa wananchi wa Mpanda Mjini walikuwa na mapenzi na
mtu siyo chama.
Arfi aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema kabla kujiuzulu
wadhifa huo, aliwahi kuhusishwa kusuka mpango wa kumwezesha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
kupita bila kupingwa katika kinyang’anyiro uchaguzi wa mwaka 2010
katika Jimbo la Katavi kwa kuwashawishi baadhi ya wagombea kuondoka
majina yao.
Hata hivyo, Arfi amekuwa akikanusha tuhuma hizo, hali ambayo pia
ilisababisha kutokuelewana na baadhi ya viongozi wenzake na kusababisha
kujiuzulu nafasi yake ya umakamu mwenyekiti.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walionyesha
kushtushwa na kauli ya mbunge huyo kujiondoa Chadema lakini wakasema
ametimiza haki yake ya kikatiba kuchagua sehemu iliyo sahihi kwake.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amewataka
viongozi wa dini nchini kuwahimiza waumini wao kuwachagua wanasiasa
wasiokuwa waovu, wasiofanana na uovu au hata kuukaribia.
Amewataka kuepuka makundi ya kisiasa na wasiwape mwanya wanasiasa
wenye dhamira ovu katika kutafuta madaraka kwa thamani yoyote na
wawakemee wale wanaotaka kupata madaraka kwa gharama yoyote.
Alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 125
tangu kuingia kwa injili katika ukanda wa Pwani ya Tanga na Milima ya
Usambara uliofanyika katika Viwanja vya Mbuyukenda jijini hapa.
“Wanasiasa wanaotaka madaraka kwa njia yoyote ile,
muwanyanyapae, wakatalieni kwa macho makavu, hawa si watu wema
watatufikisha pabaya,” Rais Kikwete.
Alisema hayo baada ya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga
kumweleza kwamba akiwa mkuu wa nchi anao wajibu wa kuhakikisha Taifa
linavuka kwa amani na usalama katika kipindi hiki kigumu cha uchaguzi.
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alisema katika kipindi
hiki, viongozi wa madhehebu ya dini wasijiingize katika makundi ya
wanasiasa kwa sababu mambo yakiharibika itakuwa hakuna pa kukimbilia.
Aliwataka viongozi wa dini watumie nyumba za ibada kuliombea Taifa
livuke salama katika kipindi hiki kigumu badala ya kuwapangia vyama au
viongozi wa kuwachagua.
“Tunawategemea kuwahimiza na
kuwakumbusha kutumia haki na wajibu wao vizuri, muwahimize na
kuwakumbusha kuwa watatakiwa kufanya mambo matatu muhimu; Kwanza,
kujiandikisha, pili, kujitokeza kwenda kupiga kura na tatu kuchagua
viongozi wazuri, wasiokuwa waovu, wasiofanana na uovu na kuukaribia
uovu, watakaosukuma mbele gurudumu la maendeleo na kujali masilahi
mapana ya jamii husika na nchi yetu.”
“Viongozi wa dini muwe kama
mimi, nina wagombea wa urais 42, kama nitaonyesha kuwa upande wa mgombea
yeyote kati yao, basi nitakuwa nimeharibu mchakato mzima wa uchaguzi.
“Tusiwape mwanya wanasiasa
wenye dhamira ovu kuwafarakanisha Watanzania. Tuendelee kukemea matumizi
mabaya ya fedha, rushwa, hila, ghiliba na hujuma katika uchaguzi. Tunapaswa kufanya hivyo tena zaidi sasa, wakati wa michakato ya ndani ya vyama vya siasa na baadaye wakati wa uchaguzi,” alisema.
Alisema hiki ni kipindi nyeti na kwamba, viongozi wa dini pamoja na
Watanzania kwa ujumla wanapaswa kufahamu kuwa Tanzania haina kinga ya
milele ya amani na utulivu, kama itavurugwa haitakuwa lulu ya Afrika
tena kama ilivyo sifa yake.
“Tuwakemee wanasiasa wapenda
madaraka kwa gharama yoyote, ambao watataka kutumia fedha kununua
ushindi au ubaguzi wa rangi, kabila, dini na kadhalika, kuwabagua
wapinzani wao na kujijenga kisiasa. Nawaomba msiwasikilize wala
kuwaendekeza kwani mchezo wao ni mauti yetu. Wakatalieni kwa macho
makavu na kwa kweli muwanyanyapae,” alisema.MWANANCHI
Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Jaji mstaafu Augustino Ramadhani amewataka Watanzania kuendelea kumwombea ili mapenzi ya Mungu ya kumfanya kuwa kiongozi wa Taifa yatimie.
Jaji Ramadhani alisema hayo jana wakati wa sherehe za maadhimisho ya
miaka 50 ya Dayosisi ya Dar es Salaam. Katika sherehe hizo, mgombea huyo
alikuwa mgeni rasmi akiambatana na Dk Mwele Malecela ambaye pia
anawania nafasi hiyo.
Jaji Ramadhani, ambaye ni mchungaji wa kanisa hilo alisema haikuwa
mapenzi yake kutangaza nia ya kugombea urais, bali alipata msukumo
kutoka kwa Mungu mwenyewe.
“Kila siku watu wananipongeza
kwa kujitokeza kuwania urais. Ninawaambia safari bado ni ndefu, wazidi
kuniombea ili mapenzi ya Mungu yatimie,”.
Kiongozi huyo alisema rushwa imekuwa tatizo kubwa nchini na kubainisha kuwa yeye anachukia na hata Mungu pia haipendi.
Alisema CCM imekuwa ikipambana na rushwa chini ya msemo wake ‘rushwa
ni adui wa haki’ na kuwataka wananchi wabadilike na kuepuka rushwa.
No comments:
Post a Comment