layiii
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wamemzuia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kuhudhuria shughuli ya kuvunja Baraza hilo itakayoongozwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein leo.
Uamuzi huo ulitolewa baada ya Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho
kutoa utangulizi kwa wajumbe akiwataka watengue kanuni ili viongozi wa
kitaifa watakaohudhuria shughuli hiyo waweze kuingia ukumbini badala ya
kukaa sehemu ya kawaida ya wageni waalikwa.
Baada ya kutoa utangulizi, Spika Kificho
alianza kuwahoji wajumbe wanaokubali viongozi wa kitaifa waruhusiwe
kuingia ndani ya Ukumbi wa Baraza kwa kuwataja wakiwamo Rais wa
Zanzibar, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, mpambe wa Rais na kuungwa mkono kwa kupigiwa makofi na sauti za ndiyo.
Hata hivyo, alipomtaja Makamu wa Kwanza
wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad wajumbe wote waliokuwapo katika Baraza
hilo, ambao wote ni wa CCM, walikataa wakisema kwa sauti “hapana,” kitendo ambacho kilimfanya Spika kurudia kutamka jina hilo kwa zaidi ya mara tatu na majibu yalikuwa hapana.
Hatua ya wawakilishi kumkataa Maalim
Seif, imekuja siku moja baada ya mawaziri na wajumbe wa CUF kutoka nje
ya Baraza wakisusa kujadili na kupitisha muswada wa sheria wa bajeti kuu
ya matumizi ya Serikali ya mwaka wa fedha 2015/16 wakipinga pamoja na
mambo mengine, mchakato unaoendelea sasa wa uandikishaji wapigakura
katika Daftari la Kudumu.
“Mnakubali
kutengua kanuni kuruhusu viongozi wa kitaifa kuhudhuria katika shughuli
yetu ndani ya ukumbi? Wageni wetu ni Rais wa Zanzibar, mpambe wake,
Jaji Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais,” alihoji Spika Kificho lakini alipingwa baada ya kulitaja jina la Makamu wa Kwanza wa Rais.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed aliwasilisha hati ya Serikali kuhusu marekebisho ya kanuni za Baraza.
Waziri Aboud alisema, Rais wa Zanzibar
atakagua gwaride maalumu la Polisi kabla ya kuhutubia Baraza hilo saa
9.30 alasiri na kuwataka wajumbe wote kufika kabla ya kuwasili kwa Rais.
Kuhusu uamuzi wa kumkataa Maalim Seif,
Aboud alisema upo katika mamlaka ya wajumbe kwa mujibu wa kanuni za
Baraza hilo na kwamba hatua itakayofuata ni Spika kumwandikia barua
Maalim Seif ya kutohudhuria shughuli hiyo ili kulinda uamuzi wa baraza
hilo.
MWANANCHI
Mtafiti binafsi na kada wa CCM, Helena Elinawinga,
amejitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama chake kuwania
urais na kusema amefikia uamuzi huo ili kupunguza kujirudiarudia kwa
adhabu za vifo kwa viongozi.
Helena anakuwa kada wa 40 wa CCM kuomba ridhaa ya chama hicho kuteuliwa kupeperusha bendera yake katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Kada huyo ni mwanamke wa sita kuchukua
fomu za kuomba kuwania nafasi hiyo katika chama hicho akitanguliwa na
Balozi Amina Salum Ali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya
Binadamu (NIMR), Dk Mwele Malecela, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro, Monica Mbega na Ritta Ngowi.
Helena alifika katika ofisi za Makao
Makuu ya CCM saa saba mchana akiwa ndani ya bajaji lakini tofauti na
wenzake, akiwa amevalia shati la rangi ya zambarau, suruali nyeusi na
kofia yenye rangi za Taifa.
Akiwa na Katibu wa Oganaizesheni,
Muhammed Seif Khatib, kada huyo ambaye pia hakuwa na wapambe kama ilivyo
kwa wagombea wengine, alikataa ombi la wapigapicha kuvua kofia. “…nitawaambia kitu kizuri baadaye kwa nini sitaki kuvua hii kofia,” alisema huku Khatib akiwasihi waandishi kutoendelea kumtaka avue au asogeze kofia hadi atakapomaliza kuchukua fomu.
Aidha, wakati akichukua fomu hiyo, kada
huyo ambaye mkononi alikuwa amebeba begi lililotengenezwa kwa kitambaa
cha nguo aina ya batiki, alilazimisha kupigwa picha pamoja na bango lake
huku akisisitiza umuhimu wa picha hiyo kupigwa hata kabla ya kumaliza
shughuli ya kukabidhiwa fomu.
Bango hilo, licha ya kuwa na maneno
ambayo yalikuwa hayaeleweki vizuri na michoro ya watu waliovalia mavazi
ya kifalme, moja lilionyesha akiwa amebeba mizani inayotumiwa na
mahakama kuonyesha usawa wa sheria na mkono mwingine akiwa amebeba
jambia.
Bango hilo pia lilikuwa na gari aina ya shangingi, picha za marais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor, Mohammed Morsi wa Misri na wanawake wengine wawili ambao hawakufahamika.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, huku akicheka, Helena alisema: “Nilikataa kuvua kofia kwa sababu sikuchana nywele.”
Kuhusu kutovaa sare za CCM, Helena
alisema aliwaambia viongozi wa chama chake kuwa wanatakiwa kufanya
mafunzo ya pamoja ya wagombea wote ili kuelewa hadhi ya sare.
Alipoulizwa kama siku saba zitamtosha kukusanya wadhamini katika mikoa
15 alisema; “Huwezi kujua nini kitatokea kama utakuwa hai au utakufa.”
MWANANCHI
Watoto wawili wenye umri wa kati ya
miaka miwili na mitano wameuawa na fisi katika Kijiji cha Mnkola, Kata
ya Ibihwa wilayani Bahi Mkoa wa Dodoma katika matukio mawili tofauti.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Teya Kata ya Ilindi wilayani hapa, Paul Mwaja alisema kuwa watoto hao wameuawa katika matukio mawili ndani ya kipindi cha wiki moja.
Mwaja alisema tukio la kwanza lilitokea
juzi ambapo mtoto mmoja wa kiume mwenye aliuawa na fisi wakati akiwa na
wenzie wawili wamelala. “Alikwenda fisi katika eneo hilo na kumvuta (mtoto mmoja) na kumtafuna hadi akamuua,”Mwaja.
Alisema usiku wa kuamkia jana, fisi huyo
alirudi tena katika kijiji hicho na kumnyang’anya mama mmoja mtoto wake
mdogo mwenye umri wa miaka miwili.
Mwaja alisema fisi huyo alimla mtoto huyo na kumbakisha kichwa na utumbo tu, hali iliyozua taharuki katika kijiji hicho.
Hata hivyo, alisema baada ya tukio hilo wananchi waliamua kufanya msako na kumkamata fisi huyo na kumuua.
Baba mzazi wa mtoto aliyeuawa usiku wa
kuamkia jana aliyejitambulisha kwa jina moja la Mchamingi, alisema
hawana imani kama fisi huyo kama ni wa kawaida kwani katika tukio la
kwanza kabla ya kuuawa, alikimbilia katika kijiji jirani cha Bahi Makulu
na kupotelea kwenye nyumba za watu.
MWANANCHI
Wakati Muswaada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2015 ukipitishwa jana bungeni, Spika, Anne Makinda ameitaka Serikali na wabunge kuwa na nidhamu kwenye matumizi ya fedha za umma, kwani itawajengea heshima.
Akihitimisha mjadala huo uliopitishwa kwa kifungu kwa kifungu, Makinda alisema: “Mkiwa na nidhamu ya matumizi ya fedha mtaheshimika na mkionyesha njaa, mtajishushia heshima.”
Hata hivyo, Makinda aliipongeza Kamati
ya Bajeti kwa kazi waliyoifanya, huku akisisitizia kuwa Spika ajaye
atakuta tayari kuna sheria ya fedha ambayo inasisitizia nidhamu ya
matumizi yake.
Awali, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya
aliwasilisha Muswada huo ili Bunge liliruhusu matumizi ya fedha za
bajeti zilizopitishwa hivi karibuni pamoja na tozo za kodi
zilizopendekezwa.
Katika michango yao, wabunge wengi
walionyesha hofu kuwa hata kama Serikali itajitahidi kukusanya fedha,
bado matumizi yake hayaridhishi hali inayoifanya ionekane kama
‘inatwanga maji kwenye kinu’.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCS Mageuzi), David Kafulila alisema tatizo kubwa linaloikabili Tanzania ni Serikali kushindwa kudhibiti matumizi ya rasilimali zake.
Kafulila alilalamikia pia suala la
matumizi ya bidhaa feki ambazo alidai zinaipunguzia hadhi Serikali, kwa
madai kuwa haina ubavu wa kuwadhibiti watu wanaozingiza nchini.
“Pamoja
na hayo, nimelalamikia na kuomba miongozo mara kadhaa hapa lakini
sijapata majibu ya kutosha kuhusu kiasi cha Sh238 bilioni ambazo
zinahusishwa na kuagizwa kwa mabehewa hewa na bando 1,000 za mabati
bandia lakini hakua anayejali,” alilalamika na kuongeza:
“Mimi
naamini hakuna uthubutu ndani ya Serikali, mnaishia kuwaogopa watu na
hasa kampuni kubwa mnaziogopa sana, igeni mfano wa Mkurugenzi wa Bahati
Nasibu (Abbas Tarimba) ambaye akikamata mashine bandia, anazichomwa moto
hadharani,” Kafulila.
Kwa upande wake, Rajabu Mohamed Mbarouk
(CUF), alisema kuna mianya mingi inayotumika katika ukwepaji wa kodi
inayowapa nafuu wafanyabiashara wakubwa wakati wadogo wakiendelea
kubanwa.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola
(CCM), aliiambia Serikali iache kigugumizi kwani wafanyabiashara
wanaokwepa kodi inawajua na ndiyo maana imekuwa ikipiga kelele kuwa wako
wakwepa kodi wakubwa.
Godbless Blandes
(Karagwe – CCM), aliitaka Serikali kuondoa ushuru na kodi katika maji.
Mbunge huyo alisema binadamu yeyote lazima anywe maji na hiyo siyo
starehe, hivyo kuyawekea kodi ni sawa na kutaka kuwaumiza wananchi wake.
NIPASHE
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na
Waziri aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya
fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, Prof. Sospeter Muhongo, jana aliumbuka baada ya Chama chake kukataa kupokea lundo la makasha ya CD (santuri) zenye picha za wadhamini wake 675.
Badala yake, alielezwa kwamba, hakuna kipengele kinachoruhusu kuwa na kumbukumbu hiyo.
Profesa Muhongo, alirejesha fomu yake ya
kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa
mwaka huu, saa 9:57 asubuhi na kumkabidhi Katibu wa Halmashauri Kuu ya
Taifa ya CCM (NEC) na Oganaizesheni, Mohamed Seif Khatibu kwenye makao
makuu ya chama hicho mjini Dodoma.
Baada ya kukabidhi fomu za wadhamini
wake katika mikoa 15 aliyopita, Profesa Muhongo alitoa pia makasha 15
yenye CD za picha ambazo alidai amefanya hivyo ili kuonyesha hajapita
njia ya mkato akidai anaamini mtu sahihi atakayeweza kuwavusha
watanzania kwa sasa, ni yeye na si mgombea mwingine kati ya makada wote
waliojitokeza kutaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Alipomaliza kuzungumza na kisha kukabidhi CD hizo, Khatibu alisema:”Bahati
mbaya katika Daftari la kurejesha fomu za CCM za kugombea kiti cha
Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2015 hakuna mahala
panapoonyesha kwamba utapaswa kukabidhi CD ulizonipa…wanaangua
(vicheko).”
Baada ya kuelezwa hivyo, aliondoka na kuziacha CD hizo kwa Khatibu.
Profesa Muhongo alijiuzulu uwaziri wa
Nishati na Madini, baada ya kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa zaidi
ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu
ya Tanzania (BoT) na baadaye kutangaza nia ya kugombea urais.
Kwa upande wake, Leonce Mulenda
ambaye naye alirejesha fomu yake ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea
urais, aliiga mfumo uliotumiwa na watangulizi wake, Waziri wa Ujenzi,
Dk. John Magufuli na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe,
kugoma kuzungumzia safari yake ya kusaka wadhamini mikoani na kurejesha
fomu kimya kimya.
Mulenda alirejesha fomu hiyo saa 5:35
asubuhi na kumkabidhi Khatibu na kumweleza kwamba amepata wadhamini
katika mikoa 15 ikiwamo mitatu ya Zanzibar na baadaye kuagana na
kuondoka huku akikwepa kuzungumzia safari yake.
NIPASHE
Wanafunzi wawili wa mafunzo ya awali wa
Jeshi la Kujenga Taifa Kambi ya Chita mkoani Morogoro, wamefariki dunia
na wengine 14 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka
eneo la mto Wami Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Wanafunzi hao walikuwa wakienda kambi ya Oldjoro mkoani Arusha kwa ajili ya kumalizia mafunzo yao ya awali.
Marehemu hao wametajwa kuwa ni Edgar Kapunga na Adam Nassoro.
Kwa mujibu wa taarifa ilitolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani jana, Jafar Ibrahim, ajali hiyo ilitokea juzi saa 12:00 jioni katika tarafa na kata ya Msata barabara ya Chalinze – Segera.
Kamanda Ibrahim alisema katika taarifa
yake hiyo kuwa wanafunzi hao walikuwa katika gari la kukodi lenye namba
za usajili T510 Alu aina ya Scania likitokea Chita kwenda Oldjoro
kumalizia mafunzo yao.
Alifafanua kuwa gari lililokuwa
limewabeba askari hao wanafunzi, liliacha njia baada ya breki zake
kufeli katika mteremko na kona za mto Wami na hivyo kupinduka.
Kamanda Ibrahim alisema majeruhi hao 14
wanaendelea kupatwa matibabu katika Hospitali Kuu nya Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) Lugalo jijini Dar es Salaam.
Aidha, alisema dereva wa gari hilo
alikimbia baada ya ajali hiyo na polisi wanaendelea kumtafuta huku miili
ya marehemu ikiwa imehifadhiwa katika Hosipitali ya Lugalo.
NIPASHE
Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi,
amewaacha njia panda wapiga kura wa jimbo hilo kutokana na kushindwa
kuweka wazi atagombea katika jimbo gani kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka
huu.
Dk. Nchimbi amekuwa akitajwa kuwa huenda
atagombea katika Jimbo la Mbinga Magharibi lililopo wilayani Nyasa
ambalo lilikuwa likishikiliwa na marehemu Kapten John Komba ambaye alifariki dunia mapema mwaka huu.
Dk. Nchimbi alisema uchaguzi mkuu wa mwaka huu huenda asigombee ubunge katika Jimbo la Songea Mjini.
“Nawashukru
viongozi wenzangu wa chama na serikali mliopo hapa na wale ambao
wamepita ndani ya miaka hii 10 ya uongozi wangu kwani walikuwa chachu ya
maendeleo, hivyo natamani kutogombea tena jimbo hili ingawa wananchi wa
Jimbo la Nyasa nao wanataka nikagombee ubunge baada ya mbunge wao
mpendwa Kapteni John Komba kufariki dunia,” alisema.
Dk. Nchimbi alisema katika kipindi cha
miaka 10 ya ubunge wake amefanikisha kuleta maendeleo kwenye sekta ya
elimu, maji, afya, barabara, kilimo, ushirika, mifugo, uvuvi, ardhi,
maliasili, umeme, mawasiliano, biashara, masoko, utawala bora na
michezo.
Alisema anapata wakati mgumu kueleza
kwamba hatagombea Jimbo la Songea Mjini, lakini jambo la msingi ni
kwamba ametekeleza kwa ukamilifu ahadi alizoahidi.
Mbunge huyo alimshukuru Rais Jakaya
Kikwete kwa kumuamini wakati wa kipindi chake cha ubunge na kumteua kuwa
naibu waziri na baadaye kuwa waziri kamili.
Dk. Nchimbi aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na baadaye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Aliondolewa katika Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi mwishoni mwa mwaka juzi kwa sababu za uwajibikaji kufuatia
sakata la operesheni Tokomeza sambamba na mawaziri wengine watatu.
Kwa upande wao, viongozi waliohudhuria
mkutano huo walionyesha masikitiko kwa hatua ya Dk. Nchimbi kuwaaga na
pia kutoweka wazi atakwenda kugombea jimbo gani la uchaguzi.
Mmoja wa viongozi hao, Alfonce Haule
alisema hatua hiyo imewachanganya na imewaacha njia panda wapigakura wa
Jimbo la Songea Mjini na kwamba wazee wamejipanga kwenda kuzungumza
naye ili abaki kugombea tena katika jimbo hilo kwani mchango wake kwa
maendeleo ya jimbo hilo bado unahitajika.
“Dk. Nchimbi tumezoea na hata alipokosea tulimuonya na alijirekebisha sasa leo ghafla anatuacha,” alisema.
Haule alisema kuwa timu ya wazee
iliyoundwa kwenda kumshauri Dk. Nchimbi agombee tena jimbo hilo imepewa
hadi Juni 28, mwaka huu iwe imerudisha jibu.
Kada wa CCM kutoka wilaya ya Nyasa, Anuciata Ngatunga,
alisema Dk. Nchimbi Juni 19 na 20 mwaka huu alikuwa wilayani humo na
alikutana na makundi mbalimbali na kuwakaribisha kwenye hafla fupi ya
uzinduzi wa nyumba yake ambayo ameijenga kijijini kwao Mbaha.
Ngatunga alisema kitendo hicho
kimewashtua viongozi mbalimbali wa chama na wananchi kwani hawaelewi nia
yake kwasababu amewaita na kuwashukuru kwa kwenda kwao kujumuika nae
kwenye hafla hiyo bila kueleza nia yake hasa.
Hata hivyo, Dk. Nchimbi alipotafutwa jana kutoa ufafanuzi kuhusiana na suala hilo hakupatikana.
HABARILEO
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi) ameitaka Serikali kuwasilisha bungeni taarifa ya kashfa ya ununuzi wa mabehewa feki katika Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kusababisha hasara ya Sh bilioni 230.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu
bungeni jana, mbunge huyo alisimama kuomba muongoza wa Spika kwamba
kutokana na unyeti wa jambo hilo, ikiwa ni pamoja na madai kwamba
Kampuni iliyopewa zabuni ya kuagiza mabehewa hayo haikuwa na uwezo huo,
kwa nini suala hilo lisipelekwe bungeni kujadiliwa.
Mbunge huyo alihoji kwamba si vyema
suala hilo likazungumzwa na kuishia nje ya Bunge badala ya kujadiliwa na
kupata ufumbuzi, lakini akijibu muongozo huo Spika wa Bunge, Anna
Makinda alisema jambo hilo ni la kisekta na kwamba lilitakiwa lianzie
kwenye kamati inayohusika.
Hata hivyo, akichangia muswada wa Sheria
ya Fedha ya Mwaka 2015 wenye lengo la kuzifanyia marekebisho sheria 16
zinazohusu masuala ya fedha, kodi, ushuru na tozo mbalimbali nchini
uliowasilishwa jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, mbunge huyo
alirudia suala hilo la TRL akisema kuna haja ya jambo hilo kufanyiwa
kazi kwani matumizi mabovu ya sh bilioni 230 hayawezi kufumbiwa macho.
Alisisitiza taarifa ya jambo hilo
ipelekwe bungeni na kuhoji kampuni hiyo iliyohusika na kuagiza zabuni
hiyo imelipwaje fedha zote hizo kabla ya kutimiza masharti na kumuomba Spika Makinda aagize taarifa iwasilishwe bungeni na sio kuwalinda.
Kauli hiyo ya kuwalinda ilimfanya Spika
Makinda kusimama na kusema halindi mtu na kumtaka mchangiaji ajielekeze
katika hoja husika.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta
wakati akifanya majumuisho ya bajeti yake Mei mwaka huu, alisema
maofisa watano wa serikali wanatarajiwa kupandishwa kizimbani hivi
karibuni, kutokana na kashfa ya uagizaji wa mabehewa 274 kutoka India,
huku wengine wakitarajiwa kuchukuliwa hatua za kiutawala.
Aprili mwaka huu, Sitta alimsimamisha
kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Kipallo
Kisamfu na wengine wanne, ili kupisha uchunguzi wa kashfa ya uingizaji
wa mabehewa feki ya mizigo.
Wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa
Mitandao, Ngosomwile Ngosomiles, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, Mkaguzi
Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand
Soka.
Mungu ajalie mchakato wa uchaguzi uende vizuri kwani hali inaonekana si mzuri sana kuelekea Oktober.
ReplyDeletePia nafikiri ni busara iwapo viongozi wataangalia zaidi maslahi ya wananchi wao kwa kuzingatia amani inawepo kabla wakati na baada ya uchaguzi.Vinginevyo ikiwekwa siasa mbele tusije tafuta mchawi baadae.