Saturday, 29 April 2017

FREEMASON: HUU NDIO UTAJIRI ALIOUACHA KIONGOZI WA FREEMASON SIR CHANDE


MTANDAO maarufu wa Wikipedia umedai kwamba hayati Jayantilal Keshavji Chande (Sir Andy Chande) ameacha utajiri wa kiasi cha dola milioni 892; unaomfanya kuwa na utajiri mkubwa kuliko ule wa Said Bakhresa, ingawa watu waliokuwa karibu naye wanakana kuwa na utajiri wa aina hiyo.

Kwa mujibu wa mtandao huo, Bakhresa ana utajiri wa thamani ya dola milioni 560 (shilingi trioni 1.2) akiwa nyuma ya Mohamed Dewji aliyetajwa na jarida la Forbes kuwa na utajiri wa dola bilioni 1.1
(shilingi trilioni 2.2) na Rostam Aziz ambaye Forbes imedai utajiri wake unakadiriwa kufikia kiasi cha dola bilioni moja (shilingi trilioni mbili).
Utajiri wa akina Dewji, Rostam na Bakhresa umekuwa ukifahamika katika jamii ya Watanzania, lakini taarifa hizi mpya kuhusu Chande, aliyefariki dunia mapema mwezi huu, ni mpya katika masikio ya wengi.

Familia ya Chande ndiyo ilikuwa ikitawala biashara ya usagishaji hapa nchini kabla ya ubinafsishaji wa mwaka 1967 na kuwa Shirika la Taifa la Usagishaji (NHC) lililobinafsishwa na kupewa Bakhresa ambaye sasa ndiye mwekezaji mkubwa zaidi mzawa hapa nchini.

Kuna kipindi, katika miaka ya 1970 na 1970, Chande alikuwa mmoja wa wakurugenzi katika bodi takribani 25 za mashirika mbalimbali ya umma hapa nchini – akidaiwa kuaminiwa na Baba wa Taifa, Julius Nyerere, kwa umahiri wake wa masuala ya kibiashara.

Kwa sasa, Chande hakuwa anamiliki biashara yoyote kubwa na maarufu hapa nchini, zaidi ya shughuli za kutoa misaada na nyingine ambazo kwa kawaida hazina uhusiano na utajiri wa namna hiyo ulioelezwa na Wikipedia.

kwamba mke wa Chande ni dada wa familia maarufu ya Madhvani, ambayo ni mojawapo ya familia tajiri za jamii ya kihindi nchini Uganda.

Mmoja wa waliokuwa marafiki wa karibu wa Chande, Hamza Kasongo, ambaye pia ni mwana habari maarufu hapa nchini, alisema haiwezekani kwamba swahiba yake huyo wa zamani anaweza kuwa na utajiri wa namna hiyo.

“ Mimi nimeanza kumfahamu Chande mwaka 1960 wakati akiwa kijana kabisa nami tayari nikiwa mtu mzima. Kwa namna ninavyofahamu, hawezi kuwa na utajiri huo.

“ Labda nikupe mfano. Siku chache kabla hajafariki dunia, nilimpigia simu kupitia namba yake ya simu ya mkononi na aliyeipokea akasema yeye ni fundi simu na alikuwa anaitengeneza.

“ Sasa jiulize, kuna tajiri wa dola milioni 900 ambaye anaweza kupeleka kutengeneza simu yake uswahilini? Basi kama ni kweli ina maana rafiki yangu alikuwa bahili sana. Lakini hapana. Haiwezekani. Hiyo ni ishara ya mtu wa kawaida.

“ Nimekwenda kwa mzee Chande kula chakula mara nyingi tu na nikwambie ukweli kwamba samani za ndani kwake ni zile za muda mrefu. Meza tuliyokuwa tunalia chakula ndiyo ileile iliyokuwepo kwa muda wa miaka 40.

“ Nyumba yake ni ileile na ukiona kuna marekebisho kwa nje ni kwa sababu alikuwa anatembelewa na wageni wengi maarufu na familia yake ikaona ni bora patengenezwe mahali pa kuzungumzia na wageni wake.

“ Hata ofisi yake walimtengenezea shemeji zake wa Madhvani. Baadaye wakaamua kumuwekea hata mahali pa kupumzikia pale ofisini. Hii ni kwa sababu alikuwa anatumia muda mrefu sana kufanya kazi bila kupumzika,” alisema Kasongo.

Kasongo ambaye kwa sasa amestaafu shughuli za utangazaji, alisema Tanzania inapaswa kumuenzi Chande kwa sababu alionyesha uzalendo na utaifa wa aina yake kwa taifa hili.

Alisema ni watu wachache wangeweza kukubali kufanya kazi na serikali ambayo imetaifisha mali zote za familia ya mtu husika, na kuitumikia kwa uaminifu bila kinyongo.

“ Kwa miaka 35, Chande alifanya kazi bila kupumzika kwenye Shirika la Usagishaji na kwingineko alikohitajika bila kinyongo. Ni Watanzania wangapi wanaweza kuwa na moyo wa aina hii. Kwangu, mzee Chande ndiyo alama ya uzalendo,” alisema Kasongo ambaye alikuwa maarufu kwa kipindi chake cha televisheni cha The Hamza Kasongo Hour.

Pamoja na mafanikio yake hayo katika utumishi, katika siku zake za mwisho duniani, Sir Andy alifahamika zaidi kwa uhusiano wake na jamii ya siri ya Freemason na taarifa hii mpya ya Wikipedia imeibua maswali kuhusu utajiri wake huo.

Chande ambaye familia yake ilihamia Tanzania ikitokea India na baadaye Kenya, anatoka katika jamii ya kihindi ambayo japo idadi yake ya watu haifiki asilimia moja ya Watanzania wote, inadaiwa kumiliki asilimia 75 ya uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa hivi karibuni na mtafiti-mwana habari, Shamlal Puri, utajiri huo wa sehemu ndogo ya watu wa jamii ya kiasia ni mojawapo ya chanzo cha uhusiano wenye shaka kati yao na wengine.

“ Watu wenye asili ya kiasia ni wachache lakini wanamilia asilimia 75 ya uchumi wa Tanzania. Tabia yao ya kutochanganyika na jamii nyingine na kukaa wenyewe kwenye jamii zao, ni moja ya changamoto kubwa za uhusiano wao na wengine,” ilisema ripoti hiyo iliyopewa jina la Asians in Tanzania: Saboteurs or Saviours (Wahindi nchini Tanzania: Wahujumu Uchumi au Wokozi).

Jayantilal Keshavji Chande alizikwa jijini Dar es Salaam kwa taratibu zote za mazishi kwa mujibu wa imani yake ya Kihindu.

Kwa kawaida, si taarifa zote za mtandao wa Wikipedia ni za kuaminika kwa asilimia 100 –kwa sababu huandikwa na watu binafsi na si taasisi zinazojulikana, mara nyingi huwa na taarifa za kweli.

Kwa mfano, Bakhresa anaaminika kuwa ndiye mtu tajiri zaidi hapa Tanzania; lakini uhalisi wa mali zake haujulikani sana kwa sababu si mtu anayependa kuandikwa kwenye vyombo vya habari kama ilivyo kwa Mo Dewji. Kwenye mtandao wa Wiki, Bakhresa ameelezwa kama mfanyabiashara msiri ambaye taarifa zake hazijulikani wazi.

No comments:

Post a Comment

advertise here