RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, amechukizwa na mwenendo wa utendaji kazi wa vyombo vya habari hususan magazeti, akiwaonya wamiliki wa vyombo hivyo vya habari katika hali inayotafsirika kuwa kulenga “kuwashughulikia”.
Rais Magufuli ametoa onyo hilo katika mazingira yanayojibainisha kuwa ni kukerwa na ripoti za habari kuhusu aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, katika kurasa za mbele za magazeti ya jana, Machi 24, 2017. Nape aliondolewa katika uwaziri juzi, Machi 23, 2017 uamuzi uliozua mjadala mkali, wengi wakimtaja mwanasiasa huyo kijana kama shujaa katika kusimamia ukweli.
Katika kurasa za mbele za magazeti mengi, ikiwa ni pamoja na gazeti la Mtanzania na Mwananchi, Nape amepewa nafasi kubwa zaidi ya kuripotiwa, karibu robo tatu ya kila ukurasa wa mbele wa magazeti hayo, huku Rais Magufuli akipewa nafasi finyu iliyopachikwa habari inayomhusu kuzuia makontena ya mchanga wa madini pamoja na kukamata magari yaliyomo kwenye makontena yaliyoingizwa nchini kwa taarifa za uongo.
Akizungumza baada ya kuwaapisha mawaziri, Dk. Harisson Mwakyembe anayekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Profesa Palamagamba Kabudi anayekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Machi 24, 2017, Rais Magufuli alisema; “…angalieni wamiliki wa habari.”
Rais Magufuli alionya kwamba vyombo vya habari katika baadhi ya nchi, akiitaja moja kwa moja Rwanda, vimekuwa chanzo cha machafuko na kutokana na hali hiyo, akarejea tukio lililofanywa na mtu anayedhamiwa kuwa askari polisi dhidi ya Nape.
Mtu huyo alichomoa bastola kiunoni mwake na kumtishia Nape akimuamuru asingumze na waandishi wa habari na badala yake aingie ndani ya gari na kuondoka. Magazeti yaliyonesha picha ya askari huyo hatua kwa hatua, namna anavyochomoa bastola na kumuelekezea Nape, na uamuzi huo wa kitaaluma wa magazeti kupitia wahariri wa kuchapisha picha hiyo kurasa za mbele, umemkera Magufuli.
Picha hiyo kwa namna fulani inafanana na ile ya tukio la kuuawa kwa mwanahabari Daudi Mwangosi, ambayo ilichapishwa katika gazeti la Mwananchi na mpiga picha wake kushinda tuzo ya mwaka ya mpiga picha bora, kupitia mashindano ya taaluma ya uandishi wa habari yanayoandaliwa na wadau mbalimbali wa habari, chini ya uratibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Kutokana na kukerwa huko, Magufuli alisema namna picha hiyo ilivyochapishwa imetoa ujumbe kuwa ni kama serikali inaunga mkono tukio hilo. Alimtaka Mwakyembe kwenda kufanya kazi, kazi ambayo hata hivyo, hakufafanua ni kama inalenga kuminya zaidi vyombo vya habari ama la.
“Mwakyembe nenda kafanye kazi, tofauti na wengine ambao walikuwa wakiogopa kuchukua hatua,” aliamuru Rais Magufuli, katika maelezo ambayo yanaweza kutafsiriwa kumlenga Nape Nnauye ambaye naye akiwa waziri, alifungia baadhi ya redio na magazeti. Katika maelezo yake hayo vile vile Rais Magufuli alivitaka vyombo vya habari kuandika masuala ya maendeleo.
Uamuzi wa kumwondoa Nape katika uwaziri msingi wake unatajwa kuwa ni tukio la mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds Media Group na kutokana na tukio hilo, Nape, akiwa waziri anayesimamia tasnia ya habari, aliunda kamati ya watu watano kuchunguza sakata hilo, kamati hiyo ilimkabidhi ripoti ambayo naye aliahidi kuiwasilisha kwa mamlaka za juu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Hata hivyo, siku moja baada ya kupokea ripoti hiyo, Nape aliondolewa kwenye baraza la mawaziri.
No comments:
Post a Comment