Sunday, 20 November 2016

MAKAMU MWENYEKITI WA ZAMANI YANGA AFARIKI DUNIA

ALIYEWAHI kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Yanga, Isaac Shekiondo ‘Clinton’ amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.

Taarifa ya familia imesema kwamba, marehemu amefariki baada ya kuugua kwa muda na msiba upo nyumbani kwake, Ilala Mchikichini Kota.

Shekiondo alikuwa Makamu Mwenyekiti katika Kamati ya Muda ya Yanga chini ya Mwenyekiti, Tarimba Abbas ‘Thabo Mbeki’ na enzi zake anakumbukwa kutokana na ukarimu wake na uwajibikaji mzuri.



Rais wa  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema amezipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Shekiondo.

“Kwa kweli nimezipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Shekiondo. Namfahamu vizuri yule bwana, tumefanya naye kazi Yanga. Na tulikuwa naye kwenye mpira siku zote,”alisema Malinzi kutoka India leo.

Rais wa zamani wa Yanga, Francis Kifukwe naye pia amesema amezipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Shekiondo.

“Kwa kweli ni msiba wetu sote wana Yanga. Shekiondo tulikuwa naye Yanga tena katika kipindi kigumu sana, lakini tulishirikiana vizuri kusukuma mbele gurudumu la timu. Mungu amuweke pema peponi,”amesema Kifukwe.

Bwana ametoa, bwana ametwaa. Mungu ampumzishe kwa amani marehemu Shekiondo.

No comments:

Post a Comment

advertise here