Spika wa zamani wa bunge la Tanzania Samwel Sitta amefariki dunia akipokea matibabu nchini Ujerumani.
Bw Sitta alikuwa mbunge mstaafu wa jimbo la Urambo lililopo mkoani Tabora.Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, Bw Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani.
Amekuwa akipokea matibabu tangu mwezi uliopita.
Rais wa Tanzania John Magufuli ametuma salamu za rambirambi na kusema amepokea kwa mshtuko taarifa za kifo cha spika huyo.
"Nitamkumbuka Mzee Sitta kwa uchapakazi wake, uzalendo wake na tabia yake ya kusimamia ukweli katika kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali za siasa na Serikali," amesema Rais Magufuli.
Sitta alikuwa Spika wa Bunge kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2010 na alikuwa pia Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba.
Aliwahi kuwa waziri katika wizara mbalimbali kwa vipindi tofauti.
Bw Sitta alikuwa miongoni mwa wanachama zaidi ya 42 wa CCM waliochukua fomu za kugombea urais mwaka jana.
No comments:
Post a Comment