Monday, 28 March 2016

WALIOKATA TIKETI ZA CHAD KUREJESHEWA PESA ZAO

LAYIII
Taifa StarsWachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania 
Mashabiki wa soka waliokuwa wamenunua tiketi za mechi kati ya timu ya taifa ya Tanzania na Chad ambayo imetibuka watarejeshewa fedha zao.
Rais wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) Jamal Malinzi amesema utaratibu unawekwa kuwarejeshea mashabiki pesa zao.
Timu ya taifa ya Chad ‘Les Sao’ ilijiondoa katika michuano ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) itakayofanyika mwaka 2017 nchini Gabon kutokana na matatizo ya kifedha.

Chad ilikuwa imepangiwa kukutana na Taifa Stars mechi ya marudiano uwanja wa taifa mjini Dar es Salaam leo.
“Kufuatia mechi ya Chad kutokufanyika utaratibu unafanyika ili kesho (Jumanne) watazamaji walionunua tiketi warudishiwe fedha zao,” amesema Bw Malinzi.
Amesema mashabiki watarejeshewa fedha zao kwenye vituo walikonunulia tiketi.
Wanatakiwa kubeba tiketi hizo.
Viingilio vya mchezo huo vilikuwa vimegawanyika katika makundi matatu, ambapo kiingilio cha juu kingekua shilingi 25,000 kwa VIP A, na shilingi 20,000 kwa VIP B, na kwa viti vya rangi ya bluu, kijani na orange itakua shilingi 5,000.
Tiketi za mchezo huo zilikuwa zimeanza kuuzwa Jumapili saa 2 asubuhi katika vituo vinne ambavyo ni kituo cha mafuta Buguruni (Buguruni), Ubungo Oilcom (Ubungo) na Dar Live (Mbagala) kabla ya habari za kujitoa kwa Chad kutokea.
Chad ilikuwa kwenye kundi G pamoja na timu za Tanzania, Nigeria na Misri.
CHad
Samatta alifungia Tanzania bao mechi iliyochezewa N'Djamena  
Katika mchezo wa awali uliochezwa uwanja wa Idriss Mahamat Ouya, Taifa Stars iliibuka na ushindi wa bao 1- 0 , bao lililofungwa na nahodha Mbwana Samatta dakika ya 30 ya mchezo.
Kufuatia kujitoa kwa Chad, matokeo ya michezo yote iliyoihusisha timu hiyo yamefutwa.
Kundi hilo kwa sasa linaongozwa na Misri yenye pointi 4, Nigeria pointi 2 na Tanzania pointi 1.

 

No comments:

Post a Comment

advertise here