Sunday, 15 November 2015

LOWASSA NA SIRI NZIRO, M’KITI WA CHADEMA AUAWA, USPIKA,

layiii
MWANANACHI
Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa jana hakuhudhuria mkutano wa kampeni za ubunge mjini Arusha kwa maelezo kuwa anajiandaa kutoa tamko kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar.
Maelfu ya wafuasi wa Chadema jana walifurika kwenye Uwanja wa Ngarenaro mjini hapa kuhudhuria kampeni za ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini ambao uliahirishwa kutokana na kifo cha mgombea kutoka chama cha ACT Wazalendo, lakini wakakumbana na tangazo kuwa Lowassa hataweza kuhutubia na badala yake atakuja siku ya kufunga kampeni hizo.

Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia(NCCR­ Mageuzi) naye alisema kuwa Lowassa yupo katika maandalizi ya kikao cha leo kutangaza hatma ya uchaguzi mkuu uliopita.
“Tulikuwa tumepanga Lowassa aje katika mkutano huu, lakini kutokana na kufanya maandalizi muhimu ya mkutano na waandishi wa habari kesho saa 5:00 asubuhi, ameshindwa kuja” alisema James Mbatia, mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vinne vya Chadema, CUF, NLD na NCCR Mageuzi.
CHUKUA MUDA WAKO KUMWANGALIA ADAMORE “Lowassa atakuja siku ya kufunga kampeni za ubunge katika Jimbo la Arusha hivyo tunaomba radhi,” alisema Mbatia, ambaye pia ni mbunge mteule wa Jimbo la Vunjo na mwenyekiti wa NCCR­Mageuzi.
Lowassa, ambaye juzi alikuwa na mazungumzo ya saa moja na nusu na mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif, anatarajiwa kutoa tamko kuhusu hali ya kisiasa visiwani humo ambayo imekuwa tete baada ya Tume ya Uchaguzi (ZEC) kufuta matokeo.
“Mheshimiwa anaandaa mambo muhimu atakayozungumza kesho,” alisema Aboubakar Liongo, msaidizi wa Lowassa alipoulizwa kuhusu waziri huyo mkuu wa zamani jana mchana.
Liongo alisema, mbali na suala la Zanzibar, Lowassa pia ataeleza msimamo wake kuhusu Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, ambao yeye na chama chake cha Chadema wanaamini kuwa matokeo ya kura za urais yaliyokuwa yanatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni tofauti na waliyokuwa nayo.
Tayari Lowassa ameshaeleza kuwa kumalizika kwa uchaguzi wa mwaka huu ni mwanzo wa awamu ya pili ya safari yake ya kuelekea Ikulu, akiwataka wanaomuunga mkono kutokata tama. “Unaweza kuchelewesha bahati ya mtu, lakini huwezi kuiondoa,” alisema Lowassa, ambaye alishika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 6.07.
Kwenye mkutano wa kampeni mjini Arusha, makamu mwenyekiti wa Chadema­Bara, Profesa Abdalah Safari alisema Lowassa pia atazungumzia tamko la polisi la kuzuia mikutano ya Ukawa na maandamano licha ya kuwa hiyo ni haki yao.
Ukawa ndoto Kaimu mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima alisema kwenye mkutano huo kuwa Ukawa haitakubali uchaguzi kurejewa kwa kuwa Maalim Self alishinda.
Alisema kinachoondelea Zanzibar sasa ni kuua uchumi wa nchi kwani, mambo mengi yamesimama, watalii wamegoma kwenda Zanzibar na serikali inashindwa kutambua kuwa dunia nzima inajua kilichotokea.
Simanzi mkutano Arusha Jana kwenye Uwanja wa Ngarenaro, vilio na simanzi ya kifo cha mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alfonce Mawazo vilitawala mkutano huo, huku mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Godbless Lema akishindwa kuomba kura na kuishia kulia.
Hata hivyo, aliwataka wakazi wa Arusha kuacha kulia na badala yake wajiandae kuchukua hatua kwa kuwa ameuawa Mawazo na mwingine anafuatia kwa kuwa ana taarifa za kupangwa kwa mpango huo.
Mawazo, ambaye alikuwa swahiba mkubwa wa Lema, alikuwa mmoja wa wanasiasa maarufu jijini Arusha. Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Bondeni inayomilikiwa na Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata) na baadaye aligombea udiwani wa kata ya Sombetini na kushinda.
Taarifa za kifo chake zilitangazwa na mwenyekiti wa Chadema wa mkoa, Aman Golugwa. Akizungumzia kifo hicho, Mbatia alisema wote wanaoendelea kuhusika na mauaji, hata kama ni viongozi wa juu serikalini au wastaafu, watafikishwa Mahakama za Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa kuwa hakuna kitu chenye thamani kama uhai wa mtu.
Polisi waimarisha ulinzi Kabla ya mkutano huo kuanza, polisi waliweka ulinzi kwa kutumia magari na mbwa katika barabara za kuelekea uwanja wa shule hiyo ya Ngarenaro.

MWANANCHI
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna, Suleiman Kova amesema kati ya masuala ambayo yaliliumiza kichwa Jeshi la Polisi ni maagizo yaliyokuwa yakitolewa na viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa wafuasi wao.
Kova alisema suala ambalo liliwanyima zaidi usingizi ni maagizo ya maandamano baada ya uchaguzi pamoja na wananchi kutakiwa kulinda kura zao mita 200, kutoka katika vituo vya kupigia kura.
“Lakini tunashukuru kwa kumaliza Uchaguzi Mkuu salama na hakuna aliyeyapokea maagizo hayo,” alisema.
Katika hafla maalumu ya kuwapongeza askari wake kwa kusimamia vema kampeni na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, Kova alisema maagizo ya kulinda kura mita 200 na suala la maandamano bila kikomo yaliumiza vichwa jeshi hilo.
Kova alisisitiza kwamba japokuwa usimamizi wa uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa mgumu na wa hatari tofauti na mwingine wowote uliowahi kufanyika nchini tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, walitoa nafasi sawa za ulinzi na uongozaji wa misafara ya wagombea wote bila kutoa upendeleo, hivyo kuonyesha mfano.
Alisema kwa mara ya kwanza uchaguzi umemalizika salama bila kuwapo kwa vifo au majeruhi yaliyosababishwa na polisi, kutokana na askari kutambua wajibu wao kwa wananchi na kutumia muda mwingi kutoa elimu zaidi bila ya kutumia nguvu.
Kova alieleza kuwa japokuwa kulikuwa na mazingira ya kuchokozwa kwa makusudi, polisi waliweza kuvuka kizingiti hicho na kusimamia vema uchaguzi huo.
Alisema hatua inayofuata ni kuhakikisha askari hao wanalipwa stahili hasa posho zao ambazo hawakulipwa wakati wote wa kampeni na kusimamia uchaguzi.
Alisema agizo hilo amelitoa kwa wahusika na kwamba limeanza kufanyiwa kazi. Kamanda Kova alisema sasa wanajielekeza kupambana na uhalifu.
MWANANCHI
Kasi aliyoanza nayo Rais John Magufuli ya kupambana na watumishi wasiowajibika kwenye ofisi za umma, kutoa maagizo na kuchukua hatua mbalimbali, isitumiwe kama kipimo cha utendaji wake kwa kuwa ni mapema, wasomi wamesema.
Kwa mujibu wa wasomi hao, muda mzuri wa kumpima ni baada ya kufikisha angalau siku 100 Ikulu. Walisema kila rais ana staili yake ya utendaji wa kazi na kwamba anaweza kuanza kwa nguvu, baadaye akapoa na anaweza kuanza taratibu na akawa moto baadaye.
Leo ni siku ya 10 tangu Dk Magufuli aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na tayari ameshatoa maagizo kadhaa likiwamo la kusitisha safari za nje za viongozi na kuagiza shughuli zote nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi hizo.
Pia, aliiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi kwa wafanyabiashara wakubwa bila woga, kutoa wiki moja kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuhakikisha mashine za uchunguzi za CT­SCAN na MRI zinafanya kazi.
Agizo hilo lilitekeleza ndani ya siku nne tu, kwa mashine ya MRI kuanza kufanya kazi. Alipoulizwa kuhusu hatua hizo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema si sahihi kuanza kumpima sasa. “Kiutamaduni muda sahihi wa kupima utendaji wazi wa mtu ni siku 100.
Hapo utaweza kuorodhesha mambo aliyoyafanya na siku 10 za Rais ni mwanzo wa kuzifikia siku 100,” alisema.
Alisema kikatiba Rais wa nchi ana jukumu kubwa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha taasisi ambayo itasimamia mambo aliyoyaahidi au anayotaka kuyatekeleza, jambo alilodai kuwa Dk Magufuli anaweza kulifanya ili kuweza kutekeleza na kufuatilia ahadi alizozitoa kwa wananchi.
“Siasa hufananishwa na uongo na ndiyo maana mtu ukizungumza jambo fulani watu wanaweza kumwambia ‘acha siasa nyingi’, nadhani anachokifanya Dk Magufuli ni kubana matumizi ili aweze kutekeleza ahadi yake ya elimu bure. “Nampongeza kwa kuanza kufanya mambo tofauti. Rais (Jakaya) Kikwete wakati akiingia madarakani kuna mambo alifanya ila hayakuwa na uzito kama haya aliyoanza nayo Magufuli,” Mbunda.
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk Benson Bana aliungana na Mbunda, huku akisisitiza kuwa ni mapema kumpima Magufuli wakati hata baraza la mawaziri hajaunda.
Anatoa maagizo na sehemu nyingine analazimika kwenda mwenyewe ni jambo zuri. “Kwa dalili hizi za mwanzo kabisa anaonyesha kuwa amedhamiria na hasa pale alipobana matumizi ya fedha kwa kufuta safari za nje maana zilikuwa ni safari ambazo watu wanajipatia fedha kienyeji,” Bana.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema:“Tumpe muda zaidi huu ni mwanzo tu. Kila rais ana staili yake, wapo wanaoanza kwa kusoma mazingira kwanza na kujipanga na kisha kuanza kazi na wapo wanaoanza kazi kwa kishindo.”
Alisema anachokifanya Magufuli ni kutaka kuwaonyesha Watanzania kuwa ahadi alizozitoa zinatekelezwa, kwamba hilo linaonekana kupitia mambo aliyoyafanya hadi sasa. “Binafsi, naona Magufuli anahitaji apate wataalam wa kufanya utafiti katika sekta mbalimbali.
Akipata majibu ya tafiti hizi anaweza kuzishirikisha taasisi za Serikali kufanya uamuzi wa kuleta mabadiliko,” alisema. Alisema lazima utafiti ufanyike ili kubaini tatizo la kuzorota na kusuasua kwa sekta mbalimbali nchini.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Gratian Mukoba alisema, “Siku 10 ni ndogo sasa nadhani baada ya siku 100 tutaweza kupima utendaji kazi wa rais.”
HABARILEO
Athari za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, zimeanza kujitokeza Zanzibar ambapo jumla ya wanawake wanane wamepoteza ndoa zao baada ya kulazimishwa kupiga kura kinyume na matakwa yao, kinyume na demokrasia ya mfumo wa vyama vingi.
Wakizungumza na gazeti hili wanawake hao walidai kwamba wamepewa talaka na waume zao ambao walikuwa wanataka pamoja na kuwalazimisha kufahamu wanakweda kumpigia mgombea gani ambaye wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba ambao ulifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar(ZEC).
Mkazi wa Kijiji cha Kandwi, mkoa wa Kaskazini, Jimbo la uchaguzi la Nungwi Unguja Tatu Mkombe alisema alikatazwa na mume asiende kupiga kura kwa sababu kura yake inaweza kusababisha fitina kubwa katika nchi.
“Mimi ni mfuasi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) na mume wangu anatoka Chama cha Wananchi (CUF), alinikataza nisiende kupiga kura kwa madai kwamba kura yangu inaweza kusababisha fitina kubwa katika nchi hii, lakini nilipomuuliza fitina gani alishindwa kuniambia,” alisema na kuongeza kuwa alipinga uamuzi huo na alikwenda kupiga kura na ndipo aliporudi alikuta tayari talaka yake imewekwa katika kabati na kukabidhiwa.
Hata hivyo, Tatu alisema amepokea ombi la mumewe akimtaka warudiane na kwamba na yeye amekubaliana na maamuzi hayo ingawa kwa shingo upande zaidi kwa ajili ya kulinda matunzo ya watoto wake wanaofikia sita ambapo katika kipindi cha wiki mbili walichotengana malezi yote yalikuwa juu yake.
“Nimeamua kurudi kwa mume wangu sina ujanja kwa sababu malezi yote ya watoto katika kipindi cha wiki mbili yameniangukia mimi huku mume wangu hana habari na jambo lolote,” alisema.
Salma Ibrahim Sultani (40), mkazi wa Kivunge alisema talaka aliyopewa sasa ni ya pili ambapo awali alipewa katika kipindi cha uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na mumewe kwa kumshutumu kuleta ndugu zake kuandikishwa katika jimbo la Mkwajuni ili kuiunga mkono CCM.
Alisema mara baada ya kupewa talaka ya pili amechukua uamuzi na kusema kamwe hawezi kurudi tena katika ndoa yake hiyo kwani hawezi kuishi kwa shinikizo la kisiasa. Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) Zanzibar, Mzuri Issa alikiri kupokea taarifa hizo zinazohusu matukio ya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake dhidi ya waume zao, ikiwemo utoaji wa talaka kutokana na tofauti za kisiasa.
Akifafanua zaidi Mzuri alisema Tamwa kupitia watendaji wake wameanza kulifanyia kazi suala hilo kwa kina kufahamu ukweli wake ukoje.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Suleiman ameeleza kusikitishwa na tabia hiyo iliyofanywa na baadhi ya wanaume ambao wamesahau ubinadamu na kuweka mbele tofauti za itikadi za kisiasa.
HABARILEO
Utafiti wa aina yake kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, uliohoji wanawake hasa wanandoa, umebaini taasisi hiyo muhimu katika jamii, inakabiliwa na migogoro inayochangiwa zaidi na wivu wa waume, huku wanaume wa Morogoro wakiongoza nchini kwa kuonea wivu wake zao.
Kutokana na mazingira magumu ya upatikanaji wa taarifa zake, ripoti ya utafiti huo imeeleza kuwa watafiti husika, walilazimika kuhakikisha ulinzi wa faragha kwa watoa taarifa na pale mazingira ya utoaji wa taarifa yalipokuwa yakitishia faragha hiyo, watafiti walilazimika kumuacha mtoa taarifa bila kumhoji.
Aidha watoa taarifa waliruhusiwa kuwa huru kukataa kujibu baadhi ya maswali na kabla ya kuanza kuhojiwa, watoa taarifa waliarifiwa kuwa maswali hayo ni binafsi, kwa kuwa yanatafuta majibu kuhusu masuala ya uhusiano ndani ya ndoa, huku wakihakikishiwa usiri mkubwa wa majibu yao, kwamba hakuna mtu yeyote atakayeoneshwa.
Katika hilo, watafiti walienda mbali zaidi ya unyanyasaji wa kijinsia unaotokana na vipigo, tena zaidi ya unyanyasaji wa kingono na kutafuta masuala kama kutukanwa, kuzuiwa kutembelea watu au kwenda mahali, kunyimwa mapato au vyanzo vya mapato.
Wanawake waliohojiwa na utafiti huo uliofanywa hivi karibuni wakati wa kuandaa Taarifa ya Afya ya Tanzania (DHS), walitakiwa kuelezea pia tabia za waume, au washirika wao wa kiume, za kujaribu kudhibiti sehemu ya uhuru wao, kwa kuwa zimebainika kuwa chanzo kikuu cha unyanyasaji wa kijinsia.
Maswali kwa wake Baadhi ya maswali hayo, ni pamoja na kama mume amekuwa na wivu au hasira wakati mke akiwasiliana na wanaume wengine, kama mume mara kwa mara amemtuhumu mke kwa kukosa uaminifu na kama mume amemzuia mke asikutane na marafiki zake wa kike.
Mengine ni kama mume amejaribu kuzuia mke asiwasiliane na ndugu wa upande wa mke, kama mume amekuwa akisisitiza kutaka kujua alipo mke wake wakati wote na kama mume hamuamini kabisa mke wake katika masuala ya fedha.
Matokeo ni shida Majibu ya utafiti huo uliofanyika nchi nzima, yalibaini kuna tabia inayojirudia kwa wanaume kujaribu kudhibiti sehemu ya uhuru wa wake zao, ambayo imetajwa na asilimia 66 ya wake waliohojiwa na sababu kubwa imetajwa kuwa ni wivu au hasira za waume, wakati wake zao wakizungumza na wanaume wengine.
Aidha karibu asilimia 49 ya wake hao walisema kuwa waume wao wamekuwa wakisisitiza kutaka kujua kila wanapokwenda, au walipo wakati wote, asilimia 16 wakisema waume zao hawawaamini na fedha, huku asilimia 32 wakisema kuwa waume zao wamekuwa wakiwatuhumu kwa kukosa uaminifu.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, asilimia 20 ya wanaume wametajwa kwamba wamekuwa wakizuia wake zao kukutana na marafiki zao wa kike, huku asilimia 18 ya wake wakizuiwa hata kuwasiliana na familia zao.
Matokeo zaidi yanaonesha asilimia 50 ya wanawake walioachika, waliopewa talaka, au wajane, wamesema waume waliowaacha au waliowaoa baada ya kuachika, wamekuwa na tabia hizo za kuwadhibiti.
Aidha wanawake walioolewa zaidi ya mara moja, ndio wanaotajwa kudhibitiwa zaidi na waume zao kuliko wanawake walio katika ndoa yao ya kwanza. Morogoro kwa wivu Asilimia 79 ya wanawake waliohojiwa wa Mkoa wa Morogoro, wamesema waume zao wamekuwa na wivu na mara nyingine wakikasirika kuona wao wakizungumza na wanaume wengine.
Mkoa wa pili kwa kuwa na wanaume wenye wivu kwa wake zao ni Dodoma, asilimia 77.7, Pwani (77.6%); Mara (75.9); Rukwa (75.6); Ruvuma (74.5%); Tanga (74.0%); Dar es Salaam (72.6%); Manyara (71.0%) na mkoa wa kumi ni Iringa (70.7).
Mikoa mitano ambayo wanaume hawana wivu kwa wake zao ni Pemba Kusini (38.8%); Pemba Kaskazini (42.1%); Unguja Kusini (45.8%); Mjini Magharibi (48.4) na Unguja Kaskazini (49.6%).
Vipigo wajawazito Katika utafiti huo wanawake hao waliulizwa kama wamewahi kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia, unaohusisha kupigwa au kutishwa na mume wakati wa ujauzito.
Matokeo yalionesha kuwa asilimia tisa ya wanawake hao wamewahi kukabiliwa na mazingira hayo ya unyanyasaji wa kijinsia wakati wa ujauzito kutoka kwa waume zao. Uchambuzi wa matokeo hayo, umebainisha kuwa wanawake waliobeba ujauzito mara nyingi, kwa maana ya kujaliwa watoto wengi, wamekabiliwa na mazingira hayo ya unyanyasaji wa kijinsia kuliko wanawake waliobeba ujauzito mara chache, kwa maana ya kujaliwa watoto wachache.
Aidha wanawake waliokosa elimu, kwa maana ya ambao hawajapata elimu ya sekondari na kuendelea na wasio na mali, wamekabiliwa na mazingira hayo ya kupigwa au kutishwa na waume zaidi, kuliko wajawazito walio na elimu ya kuanzia sekondari na kuendelea na wenye mali.
Kimkoa, Dodoma imeongoza kwa kuwa na waume waliotisha au kupiga wake zao wakati wakiwa wajawazito kwa asilimia 20 na kufuatiwa na mkoa wa Mara (19.8%). Mingine ni Kagera (17.4%); Kigoma (17.3%); Ruvuma (15.8%); Mbeya (13.3%); Iringa (9.5%); Morogoro (9.0%); Shinyanga (8.5%) na wa kumi ni Arusha kwa asilimia 8.1.
Mikoa mitano ambayo matukio ya wake wenye ujauzito kupigwa au kutishwa na waume wao ni nadra ni Pemba Kaskazini (1.2%); Unguja Kusini (2.9%); Kigoma (3.4%); Dar es Salaam (3.6%) na Lindi na Mtwara ambako kote matukio hayo yameripotiwa kwa asilimia 4.6.
Vipigo kwa wake Mbali na kupiga wajawazito, Mkoa wa Dodoma pia umetajwa kuongoza kwa waume kutisha au kupiga wake zao, ambapo asilimia 70.5 ya wake zao wameripotiwa kukabiliana na mazingira hayo, ukifuatiwa na Mkoa wa Mara tena kwa asilimia 66.4.
Mingine ni Ruvuma (50.8%); Morogoro (50.1%); Kagera (49.4%); Mbeya (48.8%); Rukwa (48.2%); Singida (46.8%); Mwanza (43.6%) na wa kumi ni Iringa ambako kumeripotiwa tabia hizo kwa asilimia 42.3.
Mikoa ambayo matukio ya waume kutisha na au kupiga wake zao ni nadra kutokea ni Pemba Kaskazini (6.3%); Pemba Kusini (7.5%); Unguja Kaskazini (8.2%); Mjini Magharibi (12.7%) na Tanga (15.7%).


No comments:

Post a Comment

advertise here