Sunday 27 September 2015

MAGUFULI AIGEUZIA KIBAO TUME YA TAFITI ILIYOMPA USHINDI WA URAIS

LAYIII

By Peter Elias, Mwananchi
Kahama. Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema waliofanya utafiti wamempunja asilimia kwani ana uhakika wa kushinda kwa asilimia 95 na si 65 kama zilivyotajwa kwa kuwa wananchi wanampenda, naye yuko tayari kufanya kazi ili kuwaletea maendeleo.

Akizungumza jana mjini Kahama, Dk Magufuli alisema: “Wapo wanaosema nimeshinda kwa asilimia 65, mimi ninasema nitashinda kwa asilimia 95, ninachoomba mjitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura ili nitangazwe mshindi, ninawaahidi kwamba nitawatumikia na kujenga Tanzania mpya.”
Hivi karibuni, taasisi ya Twaweza ilitoa utafiti wake uliompa nafasi ushindi wa asilimia 65 huku mpinzani wake, Edward Lowassa akipata asilimia 25 na mgombea wa ACT –Wazalendo akipata asilimia 0.3.
Baadaye, taasisi ya Ipsos (Synovate) ilitoa utafiti wake ukionyesha kwamba alishinda kwa asilimia 62 huku Lowassa akipata asilimia 31 na Anna Mghwira akipata asilimia 0.3.

Akizungumza jana kwenye mkutano wa kampeni, Dk Magufuli alisema akiwa rais, atafikiria kuufanya mji wa Kahama kuwa mkoa kwa sababu una watu wengi wanaozidi milioni moja. Aliahidi kilomita 10 za barabara ya lami katika mji huo na kuwataka wananchi kumchagua Jumanne Kishimba kuwa mbunge wao.
Dk Magufuli alianza kampeni zake katika Kata ya Nyarugusu, Geita na kuwahakikishia wakazi wa eneo hilo ambao ni wachimbaji wadogowadogo kwamba atapeleka maji na umeme katika eneo hilo.

Alisema atasimamia ilani ya chama chake inayolenga kupeleka maji vijijini kwa asilimia 85. Alisema katika mradi huo, atapeleka maji pia katika Kijiji cha Bugogo ili wachimbaji hao waishi vizuri na familia zao.
“Nitahakikisha ninalinda pia usalama wa albino, ninajua wanauawa kwa sababu ya shughuli hizi za uchimbaji madini. Huwezi kupata utajiri kwa kuua albino, lazima tubadilike watu wa Nyarugusu,” alisema.

Mkazi wa Kata ya Burungwa – Ushetu, Bahati James alisema kero kubwa inayowakabili ni unyanyasaji unaofanywa na askari wa wanyamapori.
Kabla ya mkutano huo, viongozi wa CCM ‘walimvaa’ aliyekuwa mbunge wa Kahama, James Lembeli wakidai kwamba alikuwa kikwazo cha maendeleo.
Lembeli ambaye amehamia Chadema na kuteuliwa kuwania ubunge wa Kahama Mjini, pia alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira.

Akizungumza katika Kijiji cha Mseki, Burungwa alikozaliwa Lembeli, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Abdallah Bulembo ‘alimshtaki’ akidai kwamba alikimbia Jimbo la Ushetu kwa kuhofia kunyimwa kura.

Alisema Lembeli alikuwa ni mbunge wa kwenda Marekani na Uingereza badala ya kuwatumikia wananchi wake kwa kuwapatia huduma mbalimbali za kijamii ikiwamo maji, hospitali na umeme.
Msafara wa Dk Magufuli ulipofika katika Kijiji cha Mwabomba, Ushetu, mgombea huyo alipokewa na mjumbe wa Kamati ya Ushindi ya CCM Samwel Sitta ambaye alisema amedhamiria kishinde katika nafasi zote Mkoa wa Shinyanga, kuanzia urais, ubunge na udiwani. Alisema ilani ya chama chake ni bora kuliko za vyama vingine, jambo linalowapa matumaini ya kushinda.

Alisema ahadi zilizopo kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM zimefafanuliwa vizuri na Dk Magufuli.
“Ukimsikiliza mgombea urais wa Chadema, anasema atatoa huduma ya afya bure, ukimuuliza atapata wapi fedha anasema kupitia gesi. Wataalamu wanatuambia tutaanza kunufaika na gesi yetu baada ya miaka saba, kwa hiyo huyu anawadanganya,” alisema Sitta.

No comments:

Post a Comment

advertise here