Wednesday, 19 August 2015

KIPINDU PINDU CHATISHIA DAR

LAYIII

10
HABARILEO
Mbunge wa Mpwapwa aliyemaliza muda wake na kushindwa katika kura za maoni alipoomba ridhaa ya wanachama wa CCM kuwania tena ubunge wa jimbo hilo, Gregory Teu, amesema hatakuwa
tayari kumuunga mkono mgombea aliyepitishwa na chama hicho tawala kuwania katika uchaguzi mkuu ujao, akidai ushindi huo alioupata ni wa mizegwe.
Aliyepitishwa ni mbunge wa zamani wa jimbo hilo, George Lubeleje ambaye aliangushwa na Teu mwaka 2010. Teu alipoingia bungeni aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha na baadaye alihamishiwa Wizara ya Viwanda na Biashara akiwa na nafasi hiyo hiyo.
Teu alisema kumuunga mkono mgombea huyo ni kukubali kubanwa kwa demokrasia ndani ya CCM na hivyo kusababisha makundi yasiyoisha na hivyo kuwa katika nafasi ya kutishiwa na vyama vya upinzani.
Alisema kama CCM kikizidi kuwakumbatia wagombea waliotolewa malalamiko kitasababisha wanachama wengi kukihama chama na hivyo kusababisha chama kuishiwa na rasilimali zake, yaani wanachama.
Akijibu tuhuma za mizengwe, Mkurugenzi wa Uchaguzi wilaya ya Mpwapwa ambaye pia ni Katibu wa CCM wilaya, Ndaluone Mbogo alisema vitendo vya wanachama vya kuhama vimekuwa kama maisha ya kawaida.
HABARILEO
Wakazi wengi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, mkoani Simiyu, wameingiwa na hofu baada ya kuwepo kwa matukio mfululizo ya watu kushambuliwa na fisi hadi kufa katika maeneo mbalimbali mjini hapa.
Matukio hayo yameelezwa kuendelea kutishia maisha ya wananchi katika wilaya hiyo, ambapo wengi wao walidai yanahusishwa na imani za kishirikina na kuiomba serikali kuchunguza kwa kina tatizo hilo.
Katika tukio la kusikitisha la mwanamke ambaye hakutambuliwa jina wala anapoishi, alikutwa amekufa katika eneo la mtaa wa Kidinda, kata ya Bariadi baada ya kuvamiwa na fisi na kumsababishia mauti.
Katika eneo la tukio wananchi walisema kuwa hali kwa sasa katika mji huo imekuwa ya taharuki na hofu kutokana na kile walichodai kutokea kwa matukio hayo mara kwa mata.
Walisema kwa nyakati tofauti kuwa katika kipindi cha mwezi, kumeripotiwa matukio manne ya aina hiyo.
“ Tunaishangaa ofisi ya maliasili wilaya hakuna, jambo ambalo wamelifanya wakati watu wanaendelea kupoteza maisha… Tunaomba waingilie kati. Angalia jamani ndugu zetu wanapoteza maisha, mbona zamani hawa fisi walikuwepo lakini hali hii haikuwepo? Ama si fisi wa kawaida hawa?” Elizabeth Mgema.
Akizungumzia hali hiyo pamoja na ofisi yake kulalamikiwa kutochukua hatua, Ofisa Maliasili wa halmashauri hiyo, Hellena Lintu alisema ofisi yake imeshindwa kutatua, hali hiyo kutokana na kutokuwa na uwezo wa kupambana na wanyama hao.
HABARILEO
Wafanyabiashara na watu wengine wanaotumia njia za mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART) kwa shughuli zao wameamriwa kuondoka mara moja kwenye maeneo hayo.
Agizo hilo lilitolewa jana, ikiwa ni siku moja tangu kuanza kwa mafunzo kwa madereva ambao watatoa huduma katika kipindi cha mpito kwenye barabara hizo za mfumo wa mabasi yaendayo haraka.
Mkurugenzi wa UDA-Rapid Transit (UDA-RT), Sabri Mabruk, alisema ni vyema wananchi wakaacha kufanya shughuli zisizotakiwa katika barabara hizo ili kupisha kutekelezwa kwa mradi huo.
“Barabara hiyo iachwe wazi kwa vile tayari barabara zimeshaanza kutumika kwa ajili ya kufundishia madereva,” alisema.
Mabasi yatakayotumika katika mafunzo hayo yalizinduliwa juzi kabla ya kipindi cha mpito kuanza Oktoba mwaka huu kwa ajili ya kuzoesha wananchi jinsi mradi huo unavyofanya kazi.
“Patakuwa hakuna kusukumana, hakuna wapiga debe na patakuwa na usafi wa kutosha na usalama,” alisema na kuongeza kuwa madereva watakuwa na weledi mkubwa.
Alisema mradi huo utawezesha wananchi kutumia muda mfupi kufika maeneo wanayokwenda kwa vile mabasi hayo yatatumia muda maalumu.
Mhandisi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka, Moses Nyoni alisema, “Katika kipindi cha mpito vituo vilivyokamilika ndivyo vitakavyotumika”.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete amehakikishia wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuwa Tanzania itafanya uchaguzi huru na wa haki Oktoba mwaka huu.
Katika hotuba yake ya kufunga mkutano wa 35 wa wakuu wa nchi za SADC, Rais Kikwete alisisitiza atafanya kila linalowezekana kuhakikisha hilo linafanikiwa na anakabidhi madaraka kwa Rais ajaye nchi ikiwa salama.
Aliyasema hayo akiwaaga wakuu wa nchi na marais wa nchi za SADC, kwani kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, muhula wake wa utawala utakamilika Oktoba mwaka huu.
Ameiongoza Tanzania kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Rais Kikwete ameelezea matumaini yake kuwa, uchaguzi mkuu ujao utakuwa wa mafanikio.
“Nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru, wa haki, kwa amani na kutawaliwa na uwazi kama ilivyokuwa katika chaguzi nyingine tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa Botswana, Namibia, Msumbiji, Mauritius, Zambia na Lesotho kwa kufanya uchaguzi wa amani na wenye mafanikio makubwa katika nchi zao hivi karibuni.
“Ni matarajio yangu kwamba uchaguzi ujao wa Tanzania utaongeza idadi ya nchi za SADC zilizofanya uchaguzi wenye mafanikio,” alisema.
Rais Kikwete alitumia fursa hiyo kuwaeleza wajumbe wa mkutano huo shughuli ambazo Tanzania ilishiriki kuipaisha SADC kiuchumi, kijeshi na kimkakati katika kipindi cha miaka 10 aliyokuwa madarakani.
Pinda aasa SADC Naye Waziri Mkuu, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mkutano huo, alisema nchi za SADC hazina budi kuweka mkakati utakaohakikisha kuwa nchi wanachama zinakuwa na mpango mahsusi wa kuendeleza viwanda kama ambavyo imekubaliwa kwenye kikao chao kilichomalizika leo.
“Jumuiya ya SADC kupitia sekretarieti yake itabidi iweke mkakati maalumu wa kufuatilia kama nchi wanachama imeandaa mpango wa kuendeleza viwanda kulingana na makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao cha leo (jana),” alisema Waziri Mkuu ambaye ameshiriki kikao hicho kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete.
Alisema yeye binafsi amefurahishwa na kupitishwa kwa azimio la uendelezaji wa viwanda katika nchi za SADC kwani unaendana na juhudi za Serikali ya Tanzania za kukuza uchumi kupitia uendelezaji wa viwanda vya usindikaji.
HABARILEO
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) wameulalamikia uongozi wa mamlaka hiyo upande wa Tanzania kwa kujilipa malimbikizo ya marupurupu ya miezi minne, huku ukijua kuwa watumishi wengine hawajalipwa malimbikizo ya mshahara wa Januari mwaka huu.
Wakitoa malalamiko yao, Dar es Salaam kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyakazi hao walisema tatizo la mishahara bado ni tete kwa mamlaka hiyo, kwani kuanzia Januari hadi sasa watumishi wengi hawajalipwa stahiki zao ipasavyo.
“Ni kweli tulikuwa hatujalipwa mshahara kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa, ila tulipoona mambo yanazidi kuwa magumu, tulizungumza na chama cha wafanyakazi (Trawu), ambao walifuatilia na serikali iliingilia kati baadhi yetu wakalipwa Juni mwaka huu,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Akizungumzia hilo, Kaimu Mwenyekiti wa TRAWU wa Kanda, Yasin Mleki alisema ni kweli kuna matatizo ya malimbikizo ya malipo ya mshahara, ambao kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa, asilimia kubwa ya watumishi wanadai stahiki zao.
Mleki alisema kutokana na tatizo hilo, chama hicho kilizungumza na uongozi wa Tazara ambao waliwalipa asilimia 20 ya watumishi wote mshahara wa Januari. Wengi wa watumishi waliolipwa ni wa makao makuu, karakana na idara ya ufundi.
“Ni kweli kuna tatizo la mishahara kutolipwa kwa wakati, mfano Juni mwaka huu, Tazara waliwalipa baadhi ya watumishi mshahara wa Januari, ilihali leo ni mwezi Agosti, sasa unategemea watumishi wanaishije,” Mleki.
Alisema baada ya malipo hayo ambayo hayakuweza kulipwa kwa watumishi wote, wafanyakazi walilalamika ndipo uongozi ukafanikiwa kupata fedha serikalini Sh bilioni 2.5 ambazo zililipa malimbikizo ya mshahara kuanzia Februari hadi Mei mwaka huu kwa wafanyakazi wote.
Alisema katika malipo hayo serikali ililipa mshahara pekee bila marupurupu mengine na kwamba ilipofika Agosti 12, mwaka huu uongozi wa Tazara ulipata fedha zitokanazo na uendeshaji wa mamlaka hiyo.
Inadaiwa kwamba uongozi walijilipa fedha hizo za malimbikizo ya marupurupu ya kuanzia Februari mwaka huu hadi Mei wakati watumishi wengine wengi hawajalipwa mshahara wa Januari.
“Ni jambo la ajabu, watumishi karibu asilimia 80 tunadai mshahara wa Januari ambao wenzetu wakiwemo viongozi walishajilipa, sasa kwa nini hizo fedha zilizopatikana za ndani wasingetulipa kwanza sisi tunaodai mshahara wa nyuma halafu marupurupu ambayo tunadai wote yaendelee kuwa deni la wote?” alihoji Mleki.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tazara, Dk Betram Kiswaga alisema ni kweli kuna matatizo ya ndani ya mamlaka hiyo ambayo uongozi umekaa pamoja na Trawu na kujadili jinsi ya kuyashughulikia
NIPASHE
Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU) kimesema kitasitisha huduma za usafiri wiki ijayo na kufanya semina nchi nzima.
Naibu Katibu Mkuu wa Tadwu na Msemaji,  Rashidi Saleh, alisema jana kuwa kutokana na kukaa vikao na kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,  na kutosikilizwa, hawatagoma tena bali watakuwa na semina kwa ajili ya madereva wote nchi nzima.
Alisema semina hiyo itakayofanywa, kikanda itajumuisha madereva wa malori, daladala na mabasi yaendayo mikoani na kuwa itafanyika kwa siku moja.
Alisema kanda hizo ni Pwani na Dar es Salaam, kanda ya Kaskazini Arusha, Kanda ya Kusini Mtwara pamoja na Nyanda za juu Mbeya.
Aliongeza kuwa lengo la  semina hiyo ni kutokana na kulalamikiwa kila mara wanapokutana kwenye vikao vya pamoja.
Pia katika semina hiyo madereva wataelimishwa namna ya kujaza mkataba mpya, sheria za usalama barabarani na sheria za kazi na ajira walizoagizwa na Wizara ya Kazi na Ajira  wawafundishe madereva.
Alisema pamoja na serikali kutoa siku saba  kwa kamati hiyo kushughurikia matatizo ya madereva hao, hadi leo hawaoni kinachoendelea kwenye kamati hiyo zaidi ya wao kulaumiwa.
“Madereva tuna kero nyingi  pamoja na baadhi ya madereva kupigwa na waajiri wao, posho za safari, lakini tumekuwa tukipuuzwa wakati tunapokuwa tunajadiliana katika vikao,” Saleh.
Alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kukutana na kamati hiyo bila kusikilizwa madai yao ingawa kamati hiyo iliundwa kwa ajili ya kushughulikia matatizo yao.
Dereva wa mabasi yaendayo Dar es Salaam Tunduma, Erasto Mdendemi, alisema utaratibu ambao wamekubaliana na viongozi wao ni kutotoa huduma ya usafirishaji  wiki ijayo na kwenda kuhudhuria semina hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Michael Kisaka, alisema madereva wameingia mkataba na waajiri wao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, ambaye ni mlezi wa madereva hao, alisema watakuwa wamekaa vikao wakafikia hayo maamuzi. “Mimi siwezi sema chochote hadi nipewe taarifa ya tamko hilo,” alisema.
JAMBOLEO
Watu watatu zaidi wamethibitika kufa kwa ugonjwa wa kipindupindu jijini Dar es Salaam, hivyo kufanya waliokufa kwa ugonjwa huo kufikia watano, huku wagonjwa waliolazwa katika hospitali mbalimbali za wilaya ya Kinondoni wakifia 34.
Akitoa taarifa hiyo Dar es Salaam jana, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alisema wagonjwa hao wanatoka katika maeneo ya Kijitonyama, Kimara, Manzese, Tandale, Saranga, Makumbusho, Kimara na Mwananyamala.
Makonda alisema hadi kufikia watu watano walikuwa wamekufa, huku 34 wakilazwa, ambapo 18 walikuwa wamelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala na wengine 16 katika Hospitali ya Sinza. “Kati ya wagonjwa 18 waliolazwa Mwananyamala, wakubwa ni wanne na watoto 14.
Kati ya 16 waliolazwa Sinza watatu ni wanawake na 13 ni wanaume, vifo ni vitatu,” alisema. Kutokana na ugonjwa huo, Serikali ya Kinondoni imejipanga kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo dawa, vifaa tiba vya kutosha ili kuweza kukabiliana na ugonjwa huo.
“Tumefungua kambi yetu katika zahanati ya Kijitonyama ambayo ina dawa na vifaa tiba vyote vinavyohitajika ili kuhudumia wagonjwa hao ipasavyo,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya alisema wagonjwa wengi ambao wameripoti hospitalini walifika wakiwa wamechelewa hivyo kuwa vigumu kuokoa maisha yao.
Naye Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo, Dk Aziz Msuya alisema wagonjwa wote waliokufa walicheleweshwa kufika hospitalini, hivyo kushauri mara mgonjwa anapoona dalili hizo awahi haraka kwenye kituo cha afya. Pia alisema wamehamisha kambi ya wagonjwa waliokuwa Sinza na kuwapeleka kwenye kambi mpya eneo la Mburahati.
MTANZANIA
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepitisha majina ya wagombea ubunge wa chama hicho katika mikoa mbalimbali chini ya mwamvuli wa Ukawa.
Katika uteuzi huo, baadhi ya wanasiasa na wanahabari wamefanikiwa kupenya katika chekeche la mchujo wa chama hicho na kufanikiwa kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika, iliwataja wanachama mbalimbali walioteuliwa na vikao vya maamuzi.
Mara
Katika majimbo ya Mkoa wa Mara walioteuliwa na majimbo yao katika mabano ni Steven Owawa (Rorya),  Esther Matiko(Tarime Mjini), John Heche (Tarime Vijijini), Zakaria Chiragwile (Musoma Vijijini) na  Yusuph Kazi (Butiama).
Wengine ni aliyekuwa mbunge wa viti maalumu kupitia CCM, aliyejiunga na Chadema hivi karibuni, Esther Bulaya (Bunda Mjini),  Harun Chiroko (Mwibara), Vicent Nyerere (Musoma Mjini) na Suleiman Daudi (Bunda Vijijini).
Simiyu
Katika majimbo ya Mkoa wa Simiyu walioteuliwa ni Godwin Simba (Bariadi), Abdalah Patel (Maswa Magharibi),  Sylvester Kasulumbayi (Maswa Mashariki),  Masanja Manani (Kisesa),  Meshack Opulukwa (Meatu) na Martine Magile (Itilima).
Shinyanga
Wanachama walioteliwa ni Paulo Malaika (Msalala),  James Lembeli ( (Kahama Mjini),  Simon Isaya (Ushetu), Patroas  Paschalk (Shinyanga Mjini) na Fred Mpendazoe (Kishapu).
Mwanza
Walioteuliwa ni Joseph Mkundi (Ukerewe), Kalwinzi Ngongoseke (Magu), Ezekia Wenje (Nyamagana), Martine Kaswahili (Buchosa),  Hamis  Tabasamu (Sengerema), Highness Kiwia (Ilemela) na Leonidas Kondela (Misungwi)
Geita
Mkoa wa Geita Profesa  Kulikoyela Kahigi (Bukombe), Alphonce Mawazo (Busanda),  George Mabula (Nyang’wale),  Dk Benedict Lukanima (Chato) na Nicodemus Maganga (Mbogwe).
Kagera
Mkao wa Kagera ni Prince Rwazo (Karagwe), Benedict Mtungirehi (Kyerwa), Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini) Ansbert Ngurumo (Muleba Kaskazini),  Alistides Kashasila (Muleba Kusini) na Dk. Anthony Mbassa (Biharamulo).
Mbeya
Wagombea waliopitishwa ni Njelu Kasaka (Lupa), Mpoki Mwankusye (Songwe), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Abraham Mwanyamaki (Kyela), John Mwambigija (Rungwe), Boniphace  Mwamukusi (Busokelo), Paschal Haonga (Mbozi), David Silinde (Momba), Adam Nzela (Mbeya Vijijini), Frank Mwakajoka (Tunduma) na Fanuel Mkisi (Viwawa).
Iringa
Waliopitishwa ni Patrick Ole Sosopi  (Isimani), Mussa Mdede (Kalenga),  Jumanne Makonda (Mufindi Kaskazini), Peter Msigwa (Iringa Mjini), Brian Kikoti (Kilolo) na Wille Mungai (Mafinga Mjini.
Njombe
Katika Mkoa wa Njombe ni Emmanuel Masonga (Njombe Kusini),  Edwin Swale(Lupembe), Dismas Luhwago (Wanging’ombe), Jackosn Mogela (Makete), Athromeo Mkinga (Ludewa), na Oraph Mhema (Makambako).
Rukwa
Waliopitishwa Mkoa wa Rukwa ni  Alfred Sotoka (Nkasi Kusini),  Daniel Ngogo (Kwela),  Kessy Soud (Nkasi Kaskazini),  Sadrick Malila (Sumbawanga Mjini) na Victor Mateni (Kalambo).
Tanga
Waliopitishwa Mkoa wa Tanga ni Jeradi Mrema (Kilindi), (Muheza), Ernest Msingwa ( Korogwe) na Emmanuel Kimea (Korogwe Vijijini).
Kilimanjaro
Katika Mkoa wa Kilimanjaro waliopitishwa kugombea ubunge ni Joseph Selasini (Rombo),  Christopher Mbajo (Same Magharibi),  Nagenjwa Kaboyoka (Same Mashariki) Jafary Michael (Moshi Mjini),  Freeman Mbowe (Hai) na Godwin Mollel (Siha).
Mkoa wa Arusha ni Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Gibson Mesiyeki (Arumeru Magharibi), Godbless Lema (Arusha Mjini), Onesmo Ole Nangole (Longido) Julius Kalanga (Monduli), Wille Qambalo, (Karatu) na Elias Ngorisa (Ngorongoro).
Manyara
waliopitisha na chama hicho ni James Millya (Simanjiro), Mikel Aweda (Mbulu Vijijini), Magoma Derick (Hanang’), Pauline Gekul (Babati Mjini), Laurent Tarra (Babati Vijijini), Kidawa Athumani (Kiteto) na Paulo Sulle (Mbulu Mjini).
Dar es Salaam                
Waliopitishwa Mkoa wa Dar es Salaam     ni  Saed Kubenea (Ubungo), Halima Mdee (Kawe), Mwita Waitara (Ukonga), Muslim Hassanali (Ilala) na John Mnyika (Kibamba).
Pwani
Kwa upande wa majimbo ya Mkoa wa Pwani ni Mathayo Torongey (Chalinze), Michael Mtaly (Kibaha Mjini)  na Editha Babbeiya (Kibaha Vijijini).
Morogoro
Walioteuliwa Mkoa wa Morogoro ni Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay (Mikumi), David Lugakingira (Morogoro Kusini), Peter Lijualikali (Kilombero), Suzan Kiwanga (Mlimba), Oswald Mlay (Mvomero), Alphonce Mbassa (Ulanga Magharibi), Pancras Kongoli (Ulanga Mashariki) na Marcossy Albanie(Morogoro Mjini).
Dodoma
Waliopitishwa Mkoa wa Dodoma ni Esau Ngombei (Kongwa), Benson Kigaila (Dodoma Mjini), Mathias Lyamunda (Bahi) na John Chogongo (Chilonwa).
Singida      
Waliopitishwa ni Jesca Kishoa (Iramba Magharibi), Oscar Kapalale (Mkalama), Davis Jumbe (Singida Kaskazini), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Marco Allute (Singida Magharibi), Lupaa Donald (Manyoni Magharibi) na Allute Emmanuel (Manyoni Mashariki).
Tabora
Kwa majimbo ya Mkoa wa Tabora waliopitishwa ni Charles Mabula (Nzega Mjini), Ngwigulu Kube (Igunga), Samweli Ntakamalenga (Urambo), mbunge anayemaliza muda wake kupitia CCM,  Said Nkumba (Sikonge), Deus Ngerere (Ulyankulu) na Ally Nguzo (Manonga).
Katavi
Waliopitishwa Mkoa wa Katavi ni Jonas Kalinde(Mpanda Mjini), Mussa Masanja (Mpanda Vijijini), George Sambwe (Katavi),  Gerald Kitabu (Nsimbo) na Laurent Mangweshi (Kavuu).
Kigoma
Waliopitishwa Mkoa wa Kigoma ni Dk. Yared Fubusa(Kigoma Kaskazini) na Daniel Lumenyela(Kigoma Mjini).
Ruvuma
Waliopitishwa Ruvuma      ni Elasmo Mwingira (Peramiho) na Cutherth Ngwata (Mbinga Magharibi), Edwin Kitanda (Mbinga Vijijini), John Fuime (Songea Mjini) na Edson Mbogoro(Madaba).
Kutokana na uteuzi huo Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema Bara, John Mnyika orodha ya majimbo yaliyobaki itatolewa baada ya kukamilika kwa mashauriano katika  vikao vya Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA).
MTANZANIA
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeteua vigogo 32 kuunda kamati ya kampeni za mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli katika kuhakikisha kinashinda Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Hatua ya kuteuliwa kwa kamati hiyo ambayo itakuwa chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, inaelezwa kuwa ni njia ya kukabiliana na nguvu za mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa.
Kamati hiyo inadaiwa kuwa itakoleza mnyukano wa hoja kati ya CCM na upande wa timu ya Ukawa, ambayo juzi imehitimisha kazi ya kusaka wadhamini mikoani kwa mgombea wao.
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kuundwa kwa kamati hiyo ya kampeni kitaifa kutafuatiwa na uundwaji wa kamati za ushindi katika ngazi za mikoa na wilaya kwa nchi nzima.
Alisema kutokana na kuimarika na kujiamini kwa CCM, kikao cha Kamati Kuu (CC), kilichoketi juzi Dar es Salaam kimefanya uteuzi wa wajumbe wa kamati hiyo huku kundi la waliokuwa wagombea urais katika mchakato wa chama hicho nao wakiteuliwa.
Walioteuliwa kuingia katika kamati hiyo ambao pia walikuwa wagombea urais ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, pamoja na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Wengine ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wajumbe wengine kwenye kamati hiyo ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rajab Luhwavi ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti Bara, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai atakayekuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Sophia Simba, Muhamed Seif Khatib, Issa Haji Ussi, Nape, Amina Makillagi na Christopher Ole Sendeka.
Mbali na hao, pia wapo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazizi wa CCM, Abdallah Bulembo, Hadija Aboud, Mohamed Aboud, Waride Bakari Jabu, Mahmoud Thabit Kombo, Shamsi Vuai Nahodha, Maua Daftari, Stephen Masele, Dk. Pindi Chana, Shaka Hamdu Shaka, Sadifa Juma Khamis, Antony Diallo, Livingston Lusinde pamoja na Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Ummy Mwalimu.
Nape alisema uamuzi huo ulifanywa na kikao cha CC chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete.
Kamati Kuu imewateua wagombea hao kushiriki katika kamati hiyo itakayoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana,” alisema.

No comments:

Post a Comment

advertise here