Salamu za pongezi zimeendelea kumiminika kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr), Dk Mwele Malecela baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika vya Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika.
Pia, Dk Mwele aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Mpango wa Maalumu wa WHO wa kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele (Espen) na sasa atahamia kituo chake cha kazi Congo-Brazaville.
Mradi wa Espen ulianza kutekelezwa mwaka 2016 hadi 2020, una lengo la kumaliza magonjwa yasiyopewa kipaumbele kwa kutoa vifaa tiba, elimu na dawa.
Magonjwa yasiyopewa kipaumbele ni pamoja na matende, mabusha, kichocho, minyoo ya tumbo na usubi.
Miongoni mwa waliomtumia pongezi ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya ya Sikika, Irenei Kiria ambaye aliandika katika ukurasa wake wa Twitter: “Hongera Mwele kwa kupata nafasi hiyo ina maana ulipangwa kulisaidia Taifa letu ukiwa nje.”
Mwingine ni Mhadhiri wa Saikolojia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo aliyeandika katika ukurasa wake wa twitter akisema: “Nina furaha kwa uteuzi wa Dk Mwele kuwa Mkurugenzi wa WHO.Nahisi kusamehewa kwa kuikosoa Serikali baada ya kumuondoa Nimr.”
Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile yeye aliandika katika ukurasa wake akimpongeza Dk Mwele na kusema, “Nimezidiwa na furaha baada ya kupata taarifa kuwa umepata kazi kubwa katika ogani ya kimataifa. Mlango mmoja ukifungwa mwingine hufunguliwa. Katumikie vyema.”
Dk Mwele aliondolewa kuwa Mkurugenzi wa Nimr na Rais John Magufuli Desemba 17 mwaka jana.
Kuondolewa kwake katika nafasi hiyo kulifanyika siku moja baada ya kutoa ripoti ya utafiti wa magonjwa, ndani yake ikiwamo taarifa ya virusi vya ugonjwa wa Zika katika maeneo ya Morogoro, Geita na Magharibi mwa Tanzania.
Taarifa ya Dk Mwele, ilieleza kuwa kati ya watu 533 waliopimwa, asilimia 15.6 walibainika kuwa na virusi hivyo.
Siku moja baada ya kutoa takwimu hizo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwa na Dk Mwele aliitisha mkutano na waandishi wa habari kukanusha taarifa hizo kwamba ugonjwa huo bado haujaingia nchini.
No comments:
Post a Comment